Uamuzi wa rais Obama wakosolewa
8 Januari 2013Baada ya uteuzi huo wa Chuck Hagel kuwa sasa ataongoza wizara ya ulinzi nchini Marekani, Mara moja chama cha Republican kilipinga hilo huku wademokrats nao wakizuia hisia zao hadi pale Hagel atakapoelezea wazi mtazamo wake juu ya Israel na Iran.
Kulingana na wanachama wa Republican ni kuwa Chuck mtizamo wake unaonesha wazi kuwa anaikosoa sana Israel kuliko anavyoiangalia Iran.
"Moyo wake wa kutoa maoni yake, hata kama yanaudhi na kwa namna hiyo kujikuta dhidi ya maneno ya walio wengi, ndio kile nnachokitegemea katika tume ya maswala ya usalama. kwa sababu linapohusika swala la kulinda nchi sisi sio democrats wala republican sisi ni wamarekani" Alisema rais Obama juu ya uteuzi wa Chuck Hagel
Obama pia alimteua aliyekuwa akishughulikia maswala ya kigaidi John Brennan kuongoza taasisi ya ujasusi nchini humo CIA. Brenan ambaye amefanya kazi katika taasisi ya ujasusi nchini Marekani kwa zaidi ya miaka 25 hajakumbwa na upinzani wowote japo anatarajiwa kuulizwa maswali magumu juu ya mateso na kuvuja habari za ndani za kiutawala ambazo zilihitajika kuwa siri.
Hata hivyo Brenen amesema iwapo ataidhnishwa atahakikisha kuwa taasisi ya ujasusi ya Marekani inafanya juhudi zote za kuwepo usalama nchini Marekani na kwamba kazi yake itaonesha haki, uhuru na thamani ya wamarekani.
Mataifa mengine yatoa sauti juu ya uteuzi wa Chuck
Awamu hii ya pili ya rais Obama kuteau kundi lake la usalama ilitarajiwa kuungwa mkono na wengi bungeni lakini inaonekana kuwa warepublican walio wengi wameuamua kuufanya uteuzi huo kuwa mgumu kwa Chuck Hagel hata kama anatoka katika chama chao.
Hata hivyo Israel imepongeza uteuzi wa chuck huku naibu waziri wa mambo ya nchi za kigeni wa Israel Danny Ayalon, akiliambia gazeti la nchini humo kwamba amewahi kukutana na chuck kwa mara kadhaa na kwamba Hagel anaichukulia israel kama mshirika wa kweli wa Marekani.
Iran kwa upande wao kupitia wizara ya mambo ya nchi za nje imesema inaamini kuwa uteuzi wa Chuck utasaidia katika kuleta mahusiano mema kati ya Iran na Marekani.
Mwandishi Amina Abubakar/AP/AFP/Reuters
Mhariri Yusuf Saumu