1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uamuzi wa Rais Trump wa kusitisha ufadhili WHO wakosolewa

15 Aprili 2020

Ujerumani inapendekeza kuwa agizo la watu kutokaribiana kuendelea kutekelezwa hadi Mei 3. Pendekezo hilo limetolewa kwa njia ya simu na ofisi ya Kansela Angela Merkel kwa majimbo yote 16 hapa Ujerumani.

China Peking | Xi Jinping trifft WHO Direktor Tedros Adhanom Ghebreyesus
Mkurugenzi mkuu wa WHO Tedros Adhanom akiwa na Rais Xi JinpingPicha: picture-alliance/Photoshot/J. Peng

China imeitaka Marekani kutekeleza jukumu lake kwa shirika la afya duniani WHO baada ya Rais Donald Trump kusitisha ufadhili katika shirika hilo, akikosoa jinsi  lilivyoshughulikia janga la virusi vya Corona.

Msemaji wa wizara ya mambo ya nje wa China Zhao Lijian amesema kuwa janga la virusi vya Corona limefika katika hatua ya kutisha na hivyo basi uamuzi wa Rais Trump wa kusitisha ufadhili katika shirika la afya duniani utaathiri mataifa yote duniani.

Marekani ndio mfadhili mkubwa wa WHO, ikichangia zaidi ya dola milioni 400 mwaka 2019 ambayo ni asilimia 15 ya bajeti ya shirika hilo la afya lenye makao yake Geneva.

Rais Donald Trump ameishutumu WHO  kuficha ukweli kuhusu mlipuko wa virusi vya Corona na badala yake kuamini kila taarifa iliyotolewa na China kuhusu virusi hivyo.

Hata hivyo, aliyekuwa mkuu wa idara ya ujasusi nchini Uingereza John Sawers amesema itakuwa bora China kubebeshwa lawama badala ya WHO.

Sawers amesema kuwa anafahamu hasira iliyo nayo Marekani kutokana na taarifa walizokuwa wamezificha kuhusu virusi vya Corona.

Heiko Maas aukosoa uamuzi wa Rais Trump

Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Heiko MaasPicha: picture-alliance/dpa/B. von Jutrczenka

Hapa Ujerumani, waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Heiko Maas ameukosoa uamuzi wa Rais Trump akisema kuwa kinachohitajika sasa ni kuliimarisha shirika la afya duniani.

Kupitia ukurusa wake wa Twitter, Maas ameandika:

"Lawama hazisaidii. Virusi vya Corona havijui mipaka. Tunahitajika kushirikiana katika vita hivi dhidi ya COVID-19 hasa kuimarisha shirika la WHO"

Huku hayo yakiarifiwa, hapa Ujerumani Ofisi ya Kansela Angela Merkel imependekeza kwa majimbo yote 16 ya nchi kuendelea na utekelezwaji la agizo la watu kutokaribiana hadi Mei 3 ili kuzuia kuenea kwa virusi vya Corona.

Mapendekezo hayo yatajadiliwa na baraza la mawaziri mjini Berlin baadaye hii leo.

Kuhusu maambukizi ya Corona hapa Ujerumani, Lothar Wieler ambaye ni mkuu wa taasisi ya utafiti ya Robert Koch amesema:

"Kwa sasa tuna uwezo wa kutosha katika hospitali zetu, hasa vitanda katika chumba cha wagonjwa mahututi na vifaa ya kusaidia wagonjwa kupumua."

Naye katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema kuwa huu si wakati mzuri wa kupunguza ufadhili katika shirika la afya duniani.

Katibu mkuu wa Umoja wa mataifa Antonio GuterresPicha: picture-alliance/Kyodo

Kupitia taarifa, Guterres amesema kuwa sio tu shirika la afya duniani bali mashirika yote ya kibinadamu yanayopambana na janga la virusi vya Corona hayafai kupunguziwa ufadhili hasa wakati huu.

Katibu mkuu huyo ametoa wito wa mshikamano baina ya jamii ya kimataifa katika vita dhidi ya janga la virusi la Corona.

 

Vyanzo dpa, reuters, afp

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW