1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mbinu za Putin

16 Machi 2016

Kuondolewa baadhi ya wanajeshi wa Urusi nchini Syria,na mzozo wa wakimbizi Idomeni ni miongoni mwa mada zilizochambuliwa zaidi na magazeti ya Ujerumani.

Ndege ya kivita ya Urusi ikijiandaa kuondoka SyriaPicha: Reuters/Russian Defense Ministry

Tuanzie Moscow ambako uamuzi wa rais Vladimir Putin wa kuondowa baadhi ya vikosi vya nchi yake kutoka Syria unaangaliwa kwa namna tofauti na wahariri wa magazeti. Kuna wanaoashiria uamuzi huo unamdhoofisha rais Bashar na utawala wake na wengine wanaohisi uamuzi huo ni fursa nzuri kwa mazungumzo ya amani ya Geneva. Lakini gazeti la "Thüringische Landeszeitung linaandika:"La hasha,kilichomkaa zaidi moyoni Putin sio kuimarisha amani,kilichomkaa zaidi moyoni ni kufaidisha mwenyewe. Anaweza ikilazimika kumwacha mkono Assad,ili aokoe masilahi ya nchi yake. Mnamo miezi ya hivi karibuni imedhihirika kwamba masilahi ya Urusi na yale ya Syria hayalingani hata kidogo. Assad angependelea vita viendelee,Putin anaonyesha lakini hataki kuisaidia serikali ya Damascus ishinde kijeshi.

Mbinu za Vladimir Putin

Gazeti la "Thüringer Allgemeine linajiuliza kuondoka Urusi Syria inamaanisha kazi imekwisha?"Bado. Wanamgambo wa dola la kiislam hawajashindwa bado. Lakini Moscow inataka kumpa wasaa wa kuvuta pumzi mshirika wake Assad. Moscow inataka kumpa nguvu kijeshi Assad ili apate kuregeza kamba katika mazungumzo ya amani. Kwa namna hiyo ni sawa Kremlin ikijipiga kifua kufuatia makubaliano ya kuweka chini silaha na mazungumzo ya amani yanayoendelea.

Wakimbizi wakata tamaa Idomeni

Mzozo wa wakimbizi katika eneo la Idomeni la Ugiriki karibu na mpaka na Macedonia unaendelea kugonga vichwa vya habari vya magazeti ya Ujerumani. Gazeti la "Hannoversche Allgemeine" ni miongoni mwa magazeti hayo."Picha za wakimbizi wanaolazimika kuvuka mto wa maji ya barafu yanayowafika mpaka shingoni zimemhuzunisha kila mmoja. Watu hawa hawaji kwasababu kansela wa Ujerumani amewaalika. Wanakuja kwasababu hawajui wende wapi. Kambi 3000 za Libnan zimesheheni wakimbizi milioni mbili,na Jordan pia inashindwa kuwahudumia wakimbizi milioni moja na laki tano. Huo ndio ukweli na sio propaganda ya upande huu au ule.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse

Mhariri : Mohammed Abdul-Rahman

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW