1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uasi miongoni mwa wabunge wa vyama ndugu vya CDU/CSU

Oumilkheir Hamidou
26 Septemba 2018

Kishindo kinachomkaba kansela Merkel, hotuba ya rais wa Marekani Donald Trump mbele ya hadhara kuu ya Umoja wa mataifa na kashfa ya kunajisiwa watoto na maaskofu wa kanisa katoliki ni miongoni mwa mada magazetini.

Unionsfraktion im Bundestag, Bundeskanzlerin Angela Merkel (CDU)
Picha: picture-alliance/dpa/K.Nietfeld

Wabunge wa vyama ndugu vya kihafidhina CDU na CSU waliokutana kwa kikao maalum jana wamempokonya wadhifa wake mwenyekiti wao, Volker Kauder, baada ya miaka 13 madarakani, mwanasiasa anaeaminiwa mno na kansela Merkel. Badala yake wamemchagua bila ya kutarajiwa Ralph Brinkhaus aliyekuwa hadi wakati huu msaidizi wake. "Uasi wa vyama ndugu dhidi ya Angela Merkel" ndio kichwa cha maneno cha Gazeti la "Kölner Stadt Anzeiger "linaloandika:"Tangu zamani watu walikuwa wakisema Merkel anasubiri wakati muwafak tu aondoke. Wakati muwafak wa kuondoka kwa hishma. Sasa lakini ni dhahiri, sio pekee Kauder aliepitwa na wakati  huo.

Badala ya kulitatua suala la nani ataridhi wadhifa wake, alitaka kung'ang'ania madaraka. Licha ya kukosa haiba, Brinkhaus anaonyesha kung'ara akilinganishwa na Kauder na  mtindo wake"tuendelee hivyo hivyo" . Wakati huo huo Seehofer na Merkel wanabidi watambue na wao pia wameipoteza fursa ya kuondoka kwa hishima. Hujuma dhidi yao hazitapungua hata kidogo. Hasa kwasababu vyama ndugu vya CDU/CSU vinatapa tapa kuona jinsi wapiga kura wanavyozidi kuelemea upande wa chama cha siassa kali za mrengo wa kulia AfD na wao hawajui wafanye niini kuzuwia vyama vao visizidi kupoteza imani ya wapiga kura."

Trump aitumbukiza katika hali ya ukiwa Marekani

Mkutano wa hadhara kuu ya Umoja wa Mataifa umefunguliwa jana mjini New York. Rais wa Marekani Donald Trump ameitumia fursa hiyo kushadidia msimamo mkali wa nchi yake dhidi ya Iran. Lakini kinyume na mwaka jana, Donald Trump anajikuta" katika hali ya ukiwa "linaandika gazeti la "Mittelbayerische Zeitung." "Miaka takriban miwili tangu enzi za "America First" zilipoanza, dalili zimechomoza katika hadhara kuu ya umoja wa mataifa za kujaza pengo lililoachwa na ikulu ya Marekani inayoongozwa na wanaopigania siasa za kizalendo. Ulimwengu unaanza kujisimamia bila ya kuitegemea Marekani.Trump ameitosa Marekani katika hali ya ukiwa. Walimwengu wanapofika hadi ya kumcheka rais wa Marekani basi kweli maji yamezidi unga."

Kashfa ya kunajisiwa watoto na maaskofu wa kanisa katoliki Ujerumani

Mada yetu ya mwisho magazetini inamulika uchunguzi uliofanywa kuhusu kadhia za kunajisiwa watoto na maaskofu wa kanisa katoliki nchini Ujerumani-kashfa iliyokuwa ikiendelea kwa takriban miaka 70 sasa. Gazeti la "Westfalen-Blatt" linachambua uchunguzi huo na kuandika: "Viongozi wa kanisa katoliki hawakukosa matamshi ya huzuni na masikitiko miaka iliyopita. Muhimu zaidi lakini ni nini kitafuatia. Ndo kusema kanisa litawasikiliza wahanga wote na kujibu kilio chao cha kudai haki? Ndo kusema majina yatafichuliwa, nani ametumia vibaya madaraka yake, na nani ameficha yaliyotokea kwa namna ambayo pengine wahanga zaidi watapata moyo na kuelezea yaliyowasibu ili angalao kuanza kutoa ndonge la moyoni."

 

Mwandishi: Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse

Mhariri: Mohammed Khelef

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW