1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uasi wa wanajeshi Guinea Bissau:

Mohammed Abdulrahman7 Oktoba 2004

Mnadhibu mkuu wa majeshi ya nchi hiyo auwawa.

Wanajeshi waliomuuwa mnadhimu mkuu wa majeshi ya Guinea Bissau katika uasi jana jioni, leo wamekua na mazungumzo na maafisa wa kiraia, jinsi ya kumaliza uasi huo.Wanajeshi hao walimuuwa Mnadhimu mkuu Mkuu wa majeshi Jenerali Verissimo Seabra, ambaye aliongoza mapinduzi yaliofaulu bila kumwaga damu mwaka jana, yaliouangusha utawala wa Rais Kumba.

Taarifa kutka mji mkuu Bissau zilisema, wanajeshi waasi walirejea kambini baada ya tukio hilo na hali hivi sasa ni shwari. Waziri mkuu Carlos Gomes Junior alisema anaamini kwamba wanajeshi waasi ni wale waliorudi nyumbani kutoka Liberia ambako walishiriki katika shughuli za kulinda amani kama sehemu ya kikosi cha umoja wa mataifa na kitendo chao ni hasira juu ya kucheleweshwa kwa mishahara yao.

Inadaiwa walilipwa miezi ya mitatu ya kwanza tu kati ya tisa waliokuweko Liberia Mishahara yao ilikua ni dola 1,000 za Kimarekani kwa mwezi.Lakini kumekua na wasi wasi kwamba huenda matatizo ni makubwa zaidi, hasa kufuatia kuuwawa kwa Mnadhimu mkuu wa majeshi na kushindwa kupatikana makubaliano baada ya zaidi ya saa 7 za mazungumzo kati ya waasi na serikali jana usiku.

Haikuweza kufahamika mapema ni wanajeshi wangapi waliohusika katika uasi huo, lakini idadi ya wale walikua Liberia ni karibu 500. Wizara ya mambo ya nchi za nje ya Ureno-mkoloni wa zamani nchini Guinea Bissau , imesema kilicho nyuma hasa ya uasi huo bado hakijulikani wazi.Tukio hili imeirejesha tena nchi hiyo ya Afrika magharibi katika hali ya msuko suko, mwaka mmoja tu baada ya uchaguzi wa bunge na kutawazwa kwa serikali mpya mwezi Machi. Uchaguzi wa Rais umepangwa kufanyika mapema mwaka ujao.

Juhudi za kibalozi zimeanza , ili kujaribu kuirejesha hali kuwa ya kawaida. Maafisa wa Ureno wamesema wanawasiliana na maafisa wa Guinea Bissau na nchi jirani pamoja na mashirika ya kimataifa.Jumuiya ya mataifa manane yanayozungumza Kireno, inatuma mjumbe kuzungumza na pande hizo. Mjumbe huyo ni Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Timor Mashariki na mshindi wa tunzo ya fasihi ya Nobeli Jose Ramos Horta.

Guinea Bissau-taifa la wakaazi milioni 1.3 na ambalo ni miongoni mwa nchi 10 masikini kabisa duniani, limeandamwa na vurugu za kijeshi za mara kwa mara ikiwa ni pamoja na mapinduzi. Ilikumbwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe baina ya 1998 na 1999 . Tangu uhuru 1975 kumetokea mapinduzi matatu ya serikali nchini humo

Mchana leo ilithibitishwa kwamba tukio la jana ni uasi na mazungumzo yamekua yakifanyika katika makao makuu ya jeshi la majini mjini Bissau ,kati ya ujumbe wa serikali ukiongozwa na Waziri wa mambo ya nchi za nje Soares Sambu na wanajeshi walioasi, huku yakisimamiwa na muakilishi wa umoja wa mataifa nchini humo Joao Bernardo Honwana.Wanajeshi watiifu kwa serikali sasa wanazilinda barabara muhimu pamoja na uwanja wa ndege wa Bissau.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW