1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ubaguzi wa rangi waja juu Italia

15 Julai 2013

Makamu wa Rais wa Baraza la Seneti la Italia amemfananisha waziri wa kwanza mweusi nchini Italia, Cecile Kyenge, na nyani katika tukio la hivi karibuni linaloonyesha chuki zenye misingi ya rangi nchini humo.

Picha: picture alliance/AP Photo

Siku ya Jumamosi (tarehe 13 Julai), Makamu wa Rais wa Baraza la Senate, Roberto Calderoli, akiwa katika mkutano wa hadhara uliofanyika mjini Treviglio alisema kuwa anapenda wanyama lakini akimuona Kyenge katika fikra zake, anaona mfano wa aina fulani ya nyani ajulikanaye kama Orangutan.

Kyege, raia wa Italia aliyezaliwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, ni waziri wa utangamano nchini Italia, nafasi aliyoteuliwa Aprili 2013, na tangu wakati huo amejikuta akilengwa mara kwa mara kwa mashambulizi yatokanayo na ubaguzi wa rangi.

Katika mkutano huo, Calderoli aliongeza kusema kuwa mafanikio ya Kyenge yamechochea wahamiaji haramu kuingia nchini Italia wanaoota kuwa wataikuta Marekani nchini Italia na kwamba anastahili kuwa waziri katika nchi yake ya Congo.

Mbunge wa Italia Roberto Calderoli aliyetoa matamshi ya ubaguzi wa rangiPicha: AP

Wanasiasa wakiwemo hata wa kutoka katika chama chake wamemshutumu Calderoli huku wengine wakimtaka ajiuzulu kama makamu wa rais wa Senate.

Calderolii ashutumiwa vikali

Waziri Mkuu wa Italia, Enrico Letta, kupitia mtandao wake rasmi wa Twitter amemshutumu Calderoli na kuyataja matamshi yake yasiyokubalika,kwani yanavuka mipaka yote na kuongeza kuwa anamuunga mkono Kyenge anapoendelea na kazi zake na za taifa.

Calderoli alisema hana nia ya kujiuzulu na kuomba msamaha, akidai kuwa hakumaanisha kumuudhi Kyenge, lakini matamashi yake yalikuwa ni hotuba ya kisiasa inayomulika kwa mapana sera anazosimamia waziri huyo ambazo ndizo alizokuwa akizishutumu.

Lakini baada ya kushutumiwa kutoka kila pande na sio Italia pekee, kwani hata vyombo vya habari vya kimataifa vimeangazia matamshi hayo ya ubaguzi wa rangi, Calderolli alimpigia simu Waziri Kyenge na kumuomba radhi.

Kyenge anapigania sera zitakazorahisisha mfumo wa wahamiaji kupata uraia na anaunga mkono sheria itakayomfanya kila mtoto anayezaliwa Italia kuwa mara moja raia wa nchi hiyo.

Waziri Cecile Kyenge(Kushoto) katika sherehe ya kuapishwa kwa mawaziri wa Italia Aprili 2013Picha: VINCENZO PINTO/AFP/Getty Images

Mwezi uliopita, Kyenge ambaye amekuwa akiishi Italia tangu mwaka 1983, alipokea vitisho dhidi ya maisha yake kabla ya kuzuru eneo la kaskazini mwa nchi hiyo ambayo ndiyo ngome ya chama cha Calderoli.

Si mara ya kwanza Kyenge kutishiwa

Chama hicho cha Nothern League kilimpiga marufuku mwanasiasa mmoja baada ya kupendekeza kupitia Facebook kuwa mtu anapaswa kumbaka Kyenge ili afahamu jinsi waathiriwa wa uhalifu wanavyohisi. Viongozi wa chama hicho chenye misimamo mikali wanawalaumu wahamiaji kwa uhalifu wa kimabavu nchini Italia.

Hii si mara ya kwanza kwa Calderoli, ambaye alihudumu mara mbili kama waziri katika serikali ya Silvio Berlusoni, kuzua tafrani kutokana matamshi yake. Mwaka 2006 alilazimika kujiuzulu baada ya kuvalia fulana iliyokuwa ikimdunisha Mtume Muhammad katika kituo cha televisheni cha kitaifa.

Mwaka huo huo, wakati Italia iliposhinda Kombe la Dunia la Soka aliibeza timu ya soka ya Ufaransa kwa kudai kuwa walishindwa kwa sababu wachezaji wake ni watu weusi, Waislamu na Wakomunisti.

Kyenge, ambaye ni daktari na ameolewa na Muitaliano, amesema Italia inapaswa kuanzisha sheria dhidi ya ubaguzi wa rangi kwani ni chuki na woga wa kilicho tofauti na kumtaka Calderoli kutafakari kile anachotaka kuwakilisha kupitia matamshi yake kwani ni kiongozi.

Mwandishi: Caro Robi/AP/Reuters
Mhariri: Yusuf Saumu