1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAsia

Ubalozi mdogo wa Marekani wafungwa mjini Chengdu,China

Saleh Mwanamilongo
27 Julai 2020

Bendera ya Marekani imeteremshwa jumatatu katika ubalozi wake mdogo uliopo mjini Chengdu nchini China.Beijing inajibu hatua ya Marekani siku chache zilizopita.

China inaishutumu Marekani kwa kuingilia vibaya masuala yake ya ndani ya nchi.
China inaishutumu Marekani kwa kuingilia vibaya masuala yake ya ndani ya nchi. Picha: Reuters/T. Peter

Bendera ya Marekani imeteremshwa leo katika ubalozi mdogo wa nchi hiyo uliopo mjini Chengdu nchini China, siku chache tangu Beijing ilipoamuru kufungwa kwa ubalozi huo ikijibu hatua ya Marekani ya kuufunga ubalozi mdogo wa China mjini Houston. Mahusiano baina ya nchi mbili hizo yamezorota kufuatia lawama za kila upande kwa kuhatarisha usalama wa taifa.

Picha za video zilizorushwa na shirika la habari la utangazaji la China CCTV zimeonesha bendera ya Marekani ikiteremshwa mapema leo asubuhi baada ya kuzidi mvutano wa kidiplomasia kati ya mataifa hayo mawili yenye nguvu. Kila upande unaulaumu mwingine kwa kuhatarisha usalama wa taifa na mahusiano baina ya nchi hizo mbili yamepwaya katika siku za karibuni.

Mvutano baina ya Marekani na China unakuchukua mkondo wa makabiliano ya enzi ya vita baridi. Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Uchina, Wang Wenbin aliwambia waandishi habari mjini Beijing kwamba Marekani ndio inatakiwa kulaumiwa kutokana na  hali ya hivi sasa.

''Hali ya mahusiano baina ya China na Marekani siyo yale ambayo China ilitaka kuyaona.Na Marekani ndio inabeba dhamana ya hali hii.Kwa mara nyingine tena tunaitaka Marekani kurekebisha hatua yake na kuhakikisha mazingira bora ya kurejesha uhusiano mzuri''.

Shutuma za Marekani

Marekani na China pia zimekua na vita vya ushuru tangu mwaka 2018Picha: Getty Images/AFP/N. Celis

Muda wa mwisho kwa Wamarekani kuondoka kutoka mji wa Chengdu bado haujulikani lakini wafanyakazi wa ubalozi mdogo wa China mjini Houston, Marekani walipewa muda wa saa 72 kufunga ubalozi huo na kuondoka.Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Mike Pompeo alisema kuwa serikali ya Marekani mjini Washington iliamua kuchukua hatua hiyo kwa sababu Beijing ilikuwa inaiba haki miliki ya kazi za uvumbuzi. 

 Serikali ya Beijing ilijibu na kusema hatua ya Marekani ni mchanganyiko wa uongo na chuki dhidi ya China.

China ilipoteza ubalozi wake mdogo wa Houston wiki iliyopita, lakini bado ina balozi ndogo nne nchini Marekani na ubalozi wake mkuu uliopo katika mji mkuu wa Marekani Washington DC. Marekani pia ina balozi ndogo nne nchini China.

Ubalozi mdogo wa Chengdu ulianzishwa mwaka 1985 na uliwakilisha maslahi ya Marekani katika eneo kubwa la Kusini-Magharibi mwa China,likiwemo jimbo linalojitawala la Tibet, ambako kumekuwa na shinikizo la muda mrefu la kutaka uhuru.

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi
Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW