1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kombe la dunia la wanawake ifikapo mwaka 2027

19 Oktoba 2020

Ubelgiji, Uholanzi na Ujerumani  kwa pamoja zimetangaza azma ya kuwa mwenyeji wa michuano ya kombe la dunia la wanawake ifikapo mwaka 2027.

FIFA Frauenfußball WM 2019 Finale USA - Niederlande Sari van Veenendaal
Kipa wa Uholanzi Sari van Veenadaal katika michuano ya kombe la dunia la wanawake 2019, UfansaPicha: Getty Images/AFP/J. P. Ksiazek

Katika taarifa kwa vyombo vya habari wawakilishi wa mashirikisho ya soka ya mataifa hayo jirani wameeleza azma yao kupitia kauli mbiu "mataifa matatu lengo moja" wamesema wataeleza zaidi mikakati yao katika hati rasmi itakayotolewa mwishoni mwa mwaka kabla ya kuanza mazungumzo na serikali za kitaifa kuhusu miji maalum itakayotumika kwa kinyang'anyiro hicho.

Kufikia sasa bado tarehe ya mwisho ya kutaja nchi mwenyeji wa michuano hiyo haijawekwa na shirikiksho la soka duniani, FIFA.

"Tunataka uwenyeji wa kombe la Dunia la wanawake, mashindano makubwa zaidi ulimwenguni ya wanawake katika michezo, ifikapo mwaka 2027, " alisema mkuu wa shirikisho la soka la Ubelgiji, Peter Bossaert .

Bossaert ameongeza kuwa katika miaka ya hivi karibuni, michuano iliyofanyika Uholanzi mnamo 2017 na Kombe la Dunia huko Ufaransa mwaka 2019, imedhihirisha tija kubwa kuanzia mechi nzuri, viwanja vilivyojaa mashabiki, idadi kubwa ya watazamaji kupitia runinga na wageni kutoka kote duniani.

Shirikisho la uholanzi lilikuwa na azma  ya kuandaa kombe la dunia la wanawake 2027

Kombe la dunia la michuano ya wanawake 2019Picha: Getty Images/AFP/F. Fife

Miaka miwili iliyopita, shirikisho la Uholanzi lilikuwa tayari limetangaza azma yake ya kuandaa mashindano hayo ifikapo 2027 na mpango ulipokelewa na kuungwa mkono na bunge.

Uholanzi ambayo ilikuwa mwenyeji wa michuano ya kombe la EURO la wanaume pamoja na Ubelgiji 2000 na kuandaa peke yake mashindano ya EURO 2017, ilikuwa imetaka washirika kuwania nafasi ya kuandaa kombe la dunia.

Ujerumani iliandaa mashindano hayo mara mbili, mnamo 1989 na 2001. Ujerumani pia iliwahi kuwa mwenyeji wa michuano ya Kombe la Dunia la wanawake 2011. Iliandaa mashindano ya kombe la dunia la wanaume 1974 na 2006, na kombe la EURO mwaka wa 1988 na itafanya hivyo tena 2024.

Australia ikishirikiana na New Zealand watakuwa mwenyeji wa michuano ya kombe la dunia kwa wanawake mwaka 2023.