Ubelgiji yarudisha jino la Patrice Lumumba kwa DRC
20 Juni 2022Ubelgiji imelirudisha jino la mpiganaji wa Uhuru wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo Patrice Lumumba kwa familia yake wakati wa hafla iliyofanyika leo mjini Brussels. Afisa mmoja wa serikali ya kifalme ya Ubelgiji, alimkabidhi kisanduku cha rangi ya samawati kilichokuwa na jino hilo, mabaki pekee ya Patrice Lumumba anayechukuliwa kama shujaa, kwa familia yake katika kasri ya Egmont katikati mwa Brussels.
Roland Lumumba, mmoja kati ya watoto wa Lumumba, ameliambia shirika la habari la RTBF kwamba, hatimaye wameridhika baada ya miaka kadhaa. Lumumba alikuwa Waziri Mkuu wa kwanza kuchaguliwa kwa njia ya kidemokrasia katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo baada ya nchi hiyo kujipatia uhuru mnamo mwaka 1960 kutoka kwa Ubelgiji, lakini alionekana kuzikasirisha nchi za Magharibi kwa kuwa na uhusiano wa karibu na Urusi katika kilele cha vita baridi. Aliikasirisha Ubelgiji pia baada ya kutoa hotuba ya kukosoa kutawaliwa kwa nguvu kwa nchi hiyo ya Kiafrika.