1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ubelgiji yawakumbuka wanajeshi waliokufa Rwanda

8 Aprili 2019

Ubelgiji imewakumbuka wanajeshi wake kumi waliouawa jijini Kigali Rwanda kwenye mauaji ya kimbari yaliyofanyika kwenye nchi hiyo miaka 25 iliyopita. Waziri Mkuu wa Ubelgiji, Charles Michel ameongoza shughuli hiyo.

Ruanda 25. Jahrestag Völkermord | Zeremonie in Kigali
Picha: Getty Images/AFP/Y. Chiba

Waziri Mkuu huyo wa Ubelgiji Charles Michel amesema kwamba mauaji ya askari wake yanazifanya Rwanda na Ubelgiji kuwa na historia moja. 

Akionekana mwenye kusononeka pamoja na jamaa za maaskari hao, Waziri Mkuu wa Ubelgiji, Charles Michel ameweka shada la maua kwenye eneo maalum la makaburi ya maaskari hao kwenye kambi ya zamani ya kijeshi katikati mwa mji mkuu wa Rwanda, Kigali.

Hii imekuwa ni ishara ya heshima ya kuwakumbuka wanajeshi wa nchi yake waliouawa na majeshi yaliyokuwa tiifu kwa rais wa zamani wa Rwanda Juvenali Habyarimana walipokuwa wakijaribu kuyaokoa maisha ya waziri mkuu wa zamani wa Rwanda hayati Agathe Uwiringiyimana.

Ni zoezi ambalo limehudhuriwa pia na ndugu na jamaa wa maaskari hao kutoka Ubelgiji.

Mabaki ya vichwa vya wahanga wa mauaji ya kimbari. Rwanda inaadhimisha miaka 25 tangu kutokea kwa mauaji hayo. Picha: Getty Images/AFP/S. Maina

Michel amesema kwamba licha ya uchungu ulioko miongoni mwa Wabelgiji na Wanyarwanda kwa ujumla, miaka 25 iliyopita imekuwa ni fursa ya kujenga mustakabali wa maisha ya baadaye ya wakazi wa nchi hizo mbili. Alisema "Nasimama mbele yenu kuiwakilisha nchi yangu Ubelgiji kwenye historia ya nchi kama Rwanda, leo nimezungumza na walionusurika, nimezungumza pia na jamaa za wanajeshi wa Ubelgiji waliopoteza maisha yao hapa wote hao wameonyesha matumaini makubwa ya kupiga hatua kwenda mbele. Kwa mantiki hiyo nadiriki kusema kwamba sisi kama jamii ya Wabelgiji tunapongeza juhudi, ujasiri, ukakamavu ambao umeonyeshwa na watu wa Rwanda ndani ya miaka 25 iliyopita.''

Junker asema ni maadhimisho yanayoashiria kushindwa kwa jamii ya kimataifa.

Hili ni zoezi lililofanyika siku moja baada ya Rwanda kuanza maadhimisho ya wiki nzima ya kuwakumbuka wahanga wa mauaji hayo yaliyowalenga watu wa jamii ya Watutsi.

Maadhimisho hayo yalianza jana Jumapili ambapo marais wa nchi mbalimbali za Afrika pamoja na wale kutoka Ulaya na Canada walihudhuria.

Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya, Jean-Claude Juncker, amesema kwamba kumbukumbu za mauaji haya ni ushahidi tosha wa jinsi ya jamii ya kimataifa ilivyoshindwa kutekeleza wajibu wake wa kusaidia palipohitajika msaada wa hali na mali.

Rais wa Rwanda, Paul Kagame alisema kwamba miaka 25 iliyopita imekuwa msingi bora wa umoja na maridhiano miongoni mwa Wanyarwanda, lakini akaonya kuna viashiria vinavyohatarisha maridhiano hayo. Alisema ''Wacha niseme kitu ambacho kwa kawaida huwa sipendi kukisema na ambacho tutafanya kila linalowezekana kukiepuka. Kwa wale wanaodhani nchi yetu haijaumia vya kutosha na kuamua kuingilia mambo yetu, nasema wawe ni kutoka ndani au nje, wakiamua kutusumbua wajue tutawasumbua zaidi.''

Kwa muda wa wiki nzima shughuli za maombolezo zitaendelea, lakini hata baada ya hapo Wanyarwanda wataendelea na vitendo vya kuwakumbuka wahanga hao wa mauaji ya kimbari hadi mwezi wa saba baada ya siku mia moja kuanzia sasa muda ambao ni sawa na ule uliotumiwa kutekeleza mauaji hayo.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW