1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchafuzi wa hewa wasababisha vifo 300,000 Ulaya

15 Novemba 2021

Shirika la Mazingira la Ulaya limesema kuwa miongozo mipya ya ubora wa hewa kutoka katika Shirika la Afya Duniani, WHO ingeweza kuyaokoa maisha ya takriban watu 180,000 kwa mwaka 2019 barani Ulaya.

Deutschland Blick auf die  Industrielandschaft Prosper bei Bottrop
Picha: picture-alliance/blickwinkel/S. Ziese

Hayo yameelezwa katika ripoti ya shirika hilo la EEA iliyochapishwa siku ya Jumatatu na kuongeza kuwa zaidi ya nusu ya vifo visivyotarajiwa 307,000 viliyotokana na hewa chafu katika Umoja wa Ulaya vingeweza kuzuiwa iwapo miongozo hiyo ingefuatwa. Ripoti hiyo imesema karibu vifo 178,000 visivyotarajiwa au asilimia 58 vingeweza kuzuiwa kinadharia iwapo nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya zingefuata kanuni mpya za mwongozo zilizowekwa na WHO.

Kwa mujibu wa EEA, ubora wa hewa uliopimwa na kiwango cha chembe chembe ndogo, nitrogen dioxide na ozoni ya kiwango cha chini cha hewa, ulikuwa umeimarishwa kutoka mwaka 2018 hadi 2019 na hilo lilikuwa na matokeo mazuri kwa afya.

Ubora wa hewa waimarika

Takwimu za EEA pia zimehusisha vifo visivyotarajiwa 40,000 kutokana na sumu ya nitrogen dioxide ya muda mrefu na 16,8000 kutokana na ozoni. Utafiti umeonesha kuwa takwimu za uchafuzi huo wa hewa wa aina tatu hauwezi kuongezwa pamoja kwani kuna kiwango cha uwiano kati yao.

Mwezi Septemba WHO iliweka mapedekezo yake ya miongozo mikali ya uchafuzi wa hewa. Katika utafiti mpya, shirika la EEA lenye makao yake Copenhagen, Denmark limebaini, ubora wa hewa barani Ulaya uliimarika sana kwa mwaka 2019 ikilinganishwa na 2018.

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Mazingira la Ulaya, EEA, Hans BruyninckxPicha: EEA

Uchafuzi wa hewa ndiyo sababu kuu ya hatari kubwa ya kimazingira kwa afya ya binadamu barani Ulaya. Inaweza kusababisha magonjwa ya moyo na kiharusi, sababu kuu ya vifo visivyotarajiwa, pamoja na ugonjwa wa mapafu na saratani ya mapafu. Ripoti hiyo imeweka wazi kwamba kuyafikia mapendekezo ya ubora wa hewa ya WHO yanaweza kuusaidia Umoja wa Ulaya kufikia lengo lake la kupunguza vifo visivyotarajiwa kwa asilimia 55 kutokana na kuathiriwa na chembe chembe ndogo ifikapo mwaka 2030.

Takwimu hizo zimetokana na utafiti uliofanywa kwenye nchi 41 zikiwemo 27 nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya na nchi nyingine za Ulaya. Kwa mujibu wa WHO, watu milioni saba ulimwenguni kote wanakufa kutokana na vifo visivyotarajiwa kila mwaka kutokana na uchafuzi wa hewa.

WHO yatoa pongezi

Mkurugenzi wa WHO barani Ulaya, Hans Henri Klugge ameipongeza ripoti hiyo na amesema kuvuta hewa safi inapaswa kuwa haki ya msingi ya binadamu. ''Ni sharti la lazima kwa jamii zenye afya na tija,'' alifafanua Klugge. Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Mazingira la Ulaya, EEA, Hans Bruyninckx amesema kuwekeza katika joto safi, uhamaji, kilimo na viwanda, kunaleta afya bora, tija na ubora wa maisha kwa watu wote wa Ulaya na hasa walioko hatarini zaidi.

Ripoti hiyo imechapishwa siku chache kabla ya viongozi wa Ulaya kukutana kwa ajili ya jukwaa la Umoja wa Ulaya kuhusu hewa safi. Pia imetolewa baada ya kumalizika kwa mkutano wa kilele wa kimataifa kuhusu mazingira wa COP26, ambao matokeo yake yametiliwa shaka na wanasayansi na wanaharakati wa hali ya hewa.

(DPA, AFP, DW https://bit.ly/3Cok3P2)

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW