1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
UchumiZambia

Uchimbaji Shaba wazidisha uchafuzi wa mazingira Zambia

Michael Kwena
25 Februari 2026

Uchafuzi wa mazingira umeongezeka nchini Zambia kufuatia shuguli za uchimbaji wa shaba katika miji ya Kitwe, Luanshya, Mufulira na Chingola.Hali hiyo imechangiwa na hitaji kubwa la soko la kimataifa la Shaba.

Uchimbaji wa shaba nchini Zambia
Uchimbaji wa shaba nchini Zambia 2009Picha: Imago Images/Zumapress

Tangu Februari mwaka jana wakati tindikali katika kiwanda cha Sino-Metals Leach kinachomilikiwa na Wachina kilipomwagika na kuchafua Mto Kafue unaounda mtiririko wa maji, uchafuzi wa mazingira umeongezeka na kuhatarisha maisha ya wananchi nchini humo.

Mbali na kuharibu mazao na kuua samaki, tukio hilo lilifufua upya hofu kuhusu usalama wa maji, hatari za kiafya na uharibifu wa muda mrefu wa mazingira unaosababishwa na sekta ya uchimbaji madini.

Kwa mujibu wa mkazi kwa jina Lloyd Mwakwa, madini hayo yenye sumu yamekuwa kitisho kikubwa kwa afya za raia. Anasema kwamba "baada ya lile tukio la kumwagika kwa tindikali, sumu iliingia mtoni na hizo ni hatari sana, na zitatuaathiri kwa muda mrefu."

Wanaharakati wa mazingira nchini humo wanasema,uchafuzi na mfiduo wa metali nzito unaendelea kuathiri maeneo ya uchimbaji madini, ambayo mara nyingi yanapakana na mashamba ya watu.

Wachimbaji wa madini wakisubiri katika lifri kabla ya kushuka chini ya ardhi huko Konkola, ZambiaPicha: Reuters/S. Henry

Kwa mujibu wa mtetezi wa haki za wanawake nchini humo Agnes Tembo, uharibifu wa mazingira unaoathiri kilimo,kwa kiasi kikubwa unaathiri maisha ya wanawake vijini. " Wasichana na wanawake wengi wanategemea kilimo kukidhi mahitaji yao ya kila siku na wakati ardhi inachukuliwa kwa ajili ya uchimbaji wa madini,vyanzo vyao vya kujipatia riziki vinapungua."

Mageuzi ya kiviwanda yanavyochangia hali hiyo

Kadri viwanda duniani vinavyohamia kwenye matumizi ya nishati safi, sekta ya shaba nchini Zambia ambayo imekuwepo kwa muda mrefu,imekuwa rasilimali muhimu katika mabadiliko ya kimataifa ya nishati.

Madini hayo ni muhimu katika utengenezaji wa betri, mitandao ya umeme na mifumo ya nishati na kuifanya taifa hilo la kusini mwa Afrika kuwa kitovu muhimu cha rasilimali asilia huku mahitaji yake yakiongezeka.

Uchimbaji wa shaba nchini ZambiaPicha: picture-alliance/Construction Photography/D. Gillie

Waziri wa Madini nchini humo Paul Kabuswe katika kikao na waandishi wa habari hivi karibuni,alisema Zambia ni mzalishaji wa pili wa shaba barani Afrika ikijiandaa kuzalisha tani milioni moja mwaka huu na tani milioni 3 kufikia mwaka 2031.

Ikumbukwe, Rais Hakainde Hichilema alitangaza mpango wa usawazishwaji wa uchumi na mazingira na kusisitiza shuguli za uchimbaji madini sharti iunge mkono maendeleo ya jamii na biashara za ndani ya taifa hilo.

Hata hivyo, vyama vya wafanyakazi vinatahadharisha kwamba mafanikio ya kiuchumi hayawanufaishi watu kwa usawa nchini humo wakati Kampuni nyingi za uchimbaji madini zikianza kutegemea zaidi wafanyakazi wa kandarasi kutoka makampuni ya nje.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW