1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchaguzi Guinea

Halima Nyanza28 Oktoba 2010

Duru ya pili ya uchaguzi wa rais nchini Guinea, kufanyika Novemba 7.

Mgombezi mkuu wa urais Guinea Cellou Dalein Diallo.Picha: AP

Duru ya pili ya Uchaguzi wa Rais, ulioahirishwa nchini Guinea, sasa utafanyika Novemba 7, badala ya ilivyopangwa awali Oktoba 31.

Akitangaza tarehe hiyo kupitia televisheni ya Taifa, Mkuu wa Tume ya Uchaguzi nchini Guinea Siaka Sangare amesema wamefikia uamuzi huo baada ya mashauriano ya kina na pande zote katika serikali ya mpito.

Amesema tarehe hiyo ndiyo iliyokubaliwa na kwamba ana uhakika kuwa haitabadilika, pia ni ya mwisho kupangwa kwa ajili ya uchaguzi huo, ambao raia wa nchi hiyo wamekuwa wakiusubiri kwa shauku kubwa.

Sangare ambaye ni raia wa mali aliyeitwa maalumu kwa ajili ya kuongoza tume hiyo ya uchaguzi, amesema uchaguzi huo uliahirishwa kwa lengo la kuwapisha viongozi wa kisiasa kurudisha utulivu miongoni mwa wafuasi wao katika pande zote.

Mwanamke apiga kura mjini Conakry, Guinea.Picha: picture alliance/dpa

Jana jioni, Rais wa serikali ya mpito ya nchi hiyo Sekouba Konate alikutana na wagombea wawili Cellou Dalein Diallo na Alpha Conde, ambao watachuana katika duru hiyo ya pili ya uchaguzi, pamoja mkuu huyo wa tume ya uchaguzi na ujumbe maalumu wa Rais wa Burkina Faso Blaise Compaore, ambaye alitumika kama mpatanishi katika mzozo huo wa kisiasa nchini Guinea.

Duru hiyo ya pili ya uchaguzi huo wa rais ambao utawezesha kumalizika kwa takriban miaka miwili ya utawala ya kijeshi,  imekuwa ikiahirishwa mara kwa mara, tangu awamu ya kwanza ilipofanyika mwezi June mwaka huu kutokana na ghasia kati ya kambi zinazopingana kisiasa na ukosefu wa maandalizi ya kutosha.

Wakati huohuo, wagombea hao wawili wanaochuana katika kinyang'anyiro hicho cha duru ya pili ya urais,  wakisindikizwa na viongozi wa kidini na serikali, leo watatembelea mikoa ambayo imeathiriwa vibaya na ghasia za uchaguzi.

Akizungumzia kuhusiana na tarehe hiyo ya uchaguzin iliyopangwa, Alpha Konde alisema hana kipingamizi chochote, kwani kwake kipaumbele ni kufanyika kwa uchaguzi na baadaye kuendelea na mchakato wa kitaifa wa usuluhishi kutokana na kwamba nchi hiyo kwa sasa inakabiliwa na mivutano, matatizo ya kiuchumi na kwamba wamekuwa hawapati msaada wowote tangu nchi hiyo ilipowekewa vikwazo, baada ya mapinduzi yaliyotokea mwaka 2008.

Hata hivyo wapiga kura ambao wanamuunga mkono mgombea wa urais Cellou Dalein Diallo, ambaye katika duru ya kwanza ya uchaguzi alipata asilimia 43 dhidi ya mpinzani wake Alpha Conde aliyepata asilimia 18, awali walionya kuwa pendekezo la tarehe ya kufanya uchaguzi ni ya karibu mno, kutokana na watu pengine kutoweza kushiriki katika uchaguzi huo, kutokana na wengi kuyakimbia makaazi yao, kutokana na machafuko yaliyotokea nchini humo, hivi karibuni.

Na katika hatua nyingine mashirika ya haki za binadamu nchini Guinea, yametoa taarifa juu ya wasiwasi wa kutokea kwa ghasia kati ya wafuasi wa wagombea hao wawili wa urais, kutokana na uvumi kwamba wafuasi wa Bwana Diallo wameweka sumu katika maji yanayotolewa kwa wafuasi wa bwana Conde.

Mwandishi: Halima Nyanza(afp, reuters)

Mhariri:   Ramadhan Yusuf Saumu

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW