Uchaguzi Japan wafungua ukurasa mpya
31 Agosti 2009Kwa upande mwingine chama cha "Democratic Party of Japan" DPJ kitakuwa na wajumbe 308 katika bunge lenye viti 480.
Uchaguzi wa jana nchini Japan umefungua ukurasa mpya katika historia ya nchi hiyo baada ya chama LDP kushindwa vibaya na kungolewa madarakani kufutia utawala wa zaidi ya miaka hamsini. Kiongozi wa chama hicho Waziri Mkuu Taro Aso akikubali kushindwa kwa chama chake alisema:
"Ninabeba dhamana kwa kushindwa kwa chama cha LDP. Chama changu na miye hatuna budi kukubali na kuutia maanani uamuzi wa umma. Tunapaswa kuanza upya. Na kama mwanachama wa kawaida wa LDP nitafanaya kila niwezalo kutekeleza kazi hiyo."
Waziri Mkuu Taro Aso amesema atajiuzulu kama kiongozi wa chama cha LDP baada ya chama hicho kushindwa vibaya kabisa kwa kiwango ambacho hakijawahi kushuhudiwa tangu kuundwa kwake zaidi ya miaka hamsini iliyopita. Amesema kuwa serikali yake imeshindwa kupata suluhu kwa matatizo yaliyokuwa yakikabiliwa na umma kwa miaka mingi. Hata mawaziri wake wamekiri kuwa sasa wameadhibiwa na wapiga kura.
Chama hicho kimelaumiwa na wananchi kuhusu mwanya wa pato uliozidi kuwa mkubwa,mfumo wa malipo ya uzeeni uliosambaratika na kashfa mbali mbali zilizokiandama chama cha LDP. Vile vile chama hicho kimelaumiwa kwa hali mbaya ya uchumi inayoshuhudia kwa mara ya kwanza nchini humo tangu Vita Vikuu vya Pili.
Kwa upande mwingine, kiongozi wa chama DPJ Yukio Hatoyama akiwashukuru wapiga kura amesema imechukua muda mrefu lakini sasa wameshawasili. Huu ni mwanzo kwani kuna kazi zinazongojea kufanywa.Amesema:
"Kwa mara ya kwanza katika historia ya katiba yetu wananchi wameleta mabadiliko barabara na wamechagua serikali mpya kwa ujasiri.Kama mjumbe wa chama cha DPJ natoa shukrani zangu. Sasa tutaanza kufanya kazi yetu kwa kuzingatia maslahi ya umma na kuheshimu wananchi."
Chama cha DPJ kimeahidi kufufua uchumi wa Japani kwa mfano kwa kupunguza matumizi ya serikali yasio ya lazima na kuongeza pato la wafanyakazi ili kuhimiza matumizi. Uchumi utapewa kipaumbele na Yukio Hatoyama anaetazamiwa kuchaguliwa waziri mkuu mpya wa Japan katika mkutano maalum utakaofanywa katikati ya mwezi ujao wa Septemba.
Mwandishi:P.Kujath/ZPR/ P.Martin/RTRE
Mhariri:M.Abdul-Rahman