Uchaguzi jimboni North-RheinWestphalia
9 Mei 2010Uchaguzi huu ni unafanyika ikiwa ni miezi michache tangu Kansela Angela Merkel aanze muhula wake wa pili serikalini.
Chama cha Kansela Merkel cha CDU pamoja na chama shirika cha FDP kinachounga mkono masuala ya biashara sharti vipate ushindi katika uchaguzi wa leo ndipo viweze kuwa na wingi wa kura katika baraza la wawakilishi wa majimbo, Bundesrat.Uchaguzi huu unatazamwa kama kura ya maoni inayoitathmini serikali ya Angela Merkel iliyoingia madarakani yapata miezi sita iliyopita.Kwa mujibu wa mdadisi wa masuala ya siasa katika chuo kikuu cha hapa mjini Bonn,Gerd Langguth,uchaguzi huu una umuhimu mkubwa kwani unamtathmini Kansela Merkel mwenyewe.
Muungano wa mrengo wa shoto na kati
Uchumi wa jimbo la North-Rhein Westphalia ni mkubwa na ni sawa na ule wa mataifa ya Poland na Jamhuri ya Czech kwa pamoja.Endapo vyama shirika vya CDU na FDP vilivyo madarakani havitashinda katika uchaguzi wa leo,ukosefu wa uwakilishi mkubwa katika baraza la wawakilishi wa majimbo Ujerumani, Bundesrat huenda ukasababisha utekelezaji wa sera kusuasua zikiwemo hatua za kupunguza kodi zilizoafikiwa baada ya uchaguzi wa shirikisho uliofanyika mwezi Septemba mwaka uliopita. Endapo muungano wa vyama vya mrengo wa shoto na kati vitaibuka washindi,mageuzi katika sekta ya afya huenda yasifanyike kama ilivyoahidi serikali ya Angela Merkel pamoja na suala la kuyapunguza matumizi ya nishati ya nuklia.Kulingana na kura za maoni,vyama hivyo viwili shirika vina kibarua kigumu cha kuwashawishi wapiga kura kuwachagua katika jimbo hili la magharibi la North-Rhein Westphalia. Uongozi wa jimbo la North-Rhein Westphalia unavishirikisha vyama vya mirengo ya kati na kulia,kama ilivyo katika serikali kuu ya shirikisho na hali imekuwa hivyo tangu miaka mitano iliyopita.Ni katika jimbo hilo kunapatikana eneo la Ruhr lililo na viwanda ambavyo vinatatizika kiuchumi kwasababu ya hali mbaya ya fedha.
Mikopo kwa Ugiriki
Kwa upande mwengine Kansela Merkel amekosolewa na wanasiasa wa vyama vya upinzani kwasababu ya suala la kuipa Ugiriki msaada hasa baada ya kutoiidhinisha mwanzoni kwasababu ya mitazamo tofauti.Baada ya kuiunga mkono hatua ya kuikopesha Ugiriki,Bibi Merkel alisema wiki iliyopita kuwa mpango huo lazima ufanikiwe la sivyo mataifa mengine ya Ulayahuenda yakatumbukia kwenye tatizo kama hilo. Siku ya Ijumaa ,Chama cha upinzani cha kisoshalisti cha SPD kiliisusia kura ya kuupitisha uamuzi wa kuipa Ugiriki msaada.Hatua hiyo huenda ikawabadili mawazo wapiga kura hii leo.Bibi Merkel kadhalika amewarai waangalizi wa masuala ya fedha kuwatuliza wawekezaji kwa lengo la kuimaliza misukosuko katika masoko ya hisa ya mataifa yanayotumia sarafu ya euro.Uamuzi huo kamwe haukuridhiwa na raia wengi wa Ujerumani
Itakumbukwa kuwa miaka mitano iliyopita,chama kilichokuwa madarakani cha Kansela wa Ujerumani wa zamani Gerhard Schroeder kilishindwa katika uchaguzi wa jimbo hili laNorth-Rhein Westphalia,hali iliyosababisha uchaguzi wa mapema kufanyika naye kuupoteza wadhifa huo.Hata hivyo hali kama hiyo haitarajiwi kushuhudiwa safari hii ila endapo Waziri Mkuu wa chama cha CDU,Jürgen Rüttgers,atashindwa;siasa za Ujerumani huenda zikabadilika kwa kiasi kikubwa na chama chake kikapoteza ushawishi wake.Katika muongo mmoja uliopita,chama cha CDU kimekuwa na ushawishi mkubwa kisiasa nchini Ujerumani.Matokeo yoyote ambayo hayatavipa vyama shirika vilivyo madarakani vya CDU-FDP ushindi yatakuwa pigo kubwa kwa Kansela Angela Merkel.
Vituo vya kupigia kura vinatarajiwa kufungwa mwendo wa saa kumi na moja jioni na matokeo kutangazwa muda mfupi baada ya hapo.
Kwa sasa vyama hivyo vina viti 37 kati ya vyote 69 bungeni.Endapo vyama hivyo vitashindwa katika uchaguzi huu wa leo,muunganohuo utapoteza viti sita bungeni.Kwa mujibu wa sheria, ili kuwa na turufu sharti muungano wowote ule upate viti visivyopungua 35 bungeni.Kwa mujibu wa ratiba,hakuna uchaguzi mwengine wa jimbo uliopangwa kufanyika mwaka huu hapa Ujerumani.
Mwandishi:Thelma Mwadzaya-RTRE/AFPE
Mhariri: Grace Patricia Kabogo