Uchaguzi katika jimbo la North Rhine Westfalia
14 Mei 2012Wahariri wengi wanahisi hilo ni pigo pia kwa kansela Angela Merkel. Gazeti linalosomwa na watu wengi la Bild linaandika:
"Mkuu wa wahafidhina katika jimbo la North Rhine Westfalia, ambae pia ni waziri wa mazingira wa serikali kuu mjini Berlin, Norbert Röttgen, anabebeshwa pia dhamana ya pigo hilo. Hatochaguliwa kamwe kuwa kansela na ashukuru kama Merkel atamuachia aendelee kuwa waziri wa mazingira.
Mannheimer Morgen linalinganisha pigo la wahafidhina katika uchaguzi wa jimbo la North Rhine Westfalia na lile walilolipata Bayern Munich katika kombe la Shirikisho la Ujerumani na kuandika:
"Aibu iliyomfika waziri wa mazingira wa serikali kuu ya Ujerumani mtu anaweza kuilinganisha na balaa la magoli matano kwa mawili waliyobebeshwa Bayern Munich na Borussia Dortmund. Na pigo la Röttgens linahuzunisha zaidi unapoona jinsi anavyonawiri waziri mkuu Hannelore Kraft na serikali yake ya muungano wa chama cha Social Democrat na walinzi wa mazingira, Die Grüne. Amelenga nyoyo za wapiga kura, wamemuamini na kumuitikia. Hata hivyo, kabla ya mwenyekiti, Sigmar Gabriel kuotea kukiona chama chake cha SPD kinaongoza serikali kuu mjini Berlin, anapaswa atambue kwamba ushindi wa SPD katika jimbo la North Rhine Westfalia unatokana na juhudi za Hannelore Kraft. Hakuna uhakika kama Gabriel, Frank-Walter Steinmeier au Peer Steinbrück watafanya vyema kama yeye."
Gazeti la Die Welt, licha ya kukiri ni mapema mno kushangiria miezi 16 kabla ya uchaguzi mkuu, linahisi, hata hivyo, wana CDU wanatetemeka. Gazeti linaendelea kuandika
"Wasocial Democrat wanahisi wanaweza kulenga muungano pamoja na walinzi wa mazingira, Die Grüne, uchaguzi mkuu utakapoitishwa mwaka 2013. Matumaini hayo hayana msingi, kwasababu hawawezi kuunda muungano kutokana na udhaifu wa Norbert Röttgen. Karata za Angela Merkel ni tofauti."
Maoni sawa na hayo yametolewa pia na gazeti la mrengo wa shoto "Die Tageszeitung " linalohisi:
""Ushindi wa SPD na Hannelore Kraft ni timamu,bayana na mkubwa, lakini hautoi picha ya kile wanachoweza kufanya washirika wa SPD na walinzi wa mazingira dhidi ya Angela Merkel mnamo mwaka 2013.
Na hatimae Frankfurter Rundschau linajaribu kuwalinganisha mshindi wa uchaguzi wa North Rhine Westfalia, Hannelore Kraft, na kansela Angela Merkel na kuandika:
"Hannelore Kraft ni kijana kidogo kumshinda Angela Merkel. Ana msimamo tofauti wa kisiasa, na hasa katika suala la fedha. Merkel anataka kuiepushia nchi balaa la madeni, Kraft anahisi madeni si tatizo. Hata hivyo, mengi ni sawa kati ya viongozi hao wawili. Wote wawili wana moyo wa kiutu- moyo wa mama. Hawawatishi wapiga kura,wanajaribu kuwapa matumaini katika wakati huu wa shida.
Na kwa ripoti hiyo ya Frankfurter Rundschau ndio na sisi tunazifunga kurasa za magazeti ya Ujerumani hii leo.
Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Inlandsprese/AFP
Mhariri: Miraji Othman