1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchaguzi Kenya 2022: Kampeni za uchaguzi zamalizika leo

6 Agosti 2022

Wagombea katika uchaguzi wa rais nchini Kenya wanamalizia shughuli za kuomba kura huku kampeni zikifikia mwisho leo hii Jumamosi.

Kenia Wahlen 2022
Picha: Tony Karumba/AFP

Wagombea hao Naibu Rais William Ruto na Raila Odinga, kiongozi mkongwe wa upinzani ambaye sasa anaungwa mkono na chama tawala, wanapigania nafasi ya kuliongoza taifa hilo la Afrika Mashariki.

Rais wa Kenya, Uhuru KenyattaPicha: Philbert Rweyemamu/EAC

Wapiga kura wapatao milioni 22.1 wiki ijayo siku ya Jumanne tarehe 9 watamchagua rais ajaye, atakayechukua nafasi ya rais Uhuru Kenyatta anayemaliza muda wake baada ya kuliongoza taifa la Kenya kwa mihula miwili. Kwa mujibu wa katiba Uhuru Kenyatta haruhusiwi kugombea muhula wa tatu baada ya kumaliza mihula miwili. Vilevile wakenya watawachagua maseneta, magavana, wabunge, wawakilishi wa wanawake na idadi ya maafisa 1,500 wa kaunti.

Soma zaidi:Wagombea wa uchaguzi Kenya na kampeni za mwisho 

Kenya ni nchi yenye watu takriban milioni 56 na ni kitovu cha uchumi wa Afrika Mashariki. Japo nchi hiyo ina historia ya chaguzi zenye misukosuko hata hivyo nchi hiyo ni tulivu.

Ahadi za Wagombea Wakuu ni zipi?

William Ruto, Mgombea UraisPicha: Simon Maina/AFP

William Ruto mwenye umri wa miaka 55 anajitangaza kwa vijana na watu maskini kama mtu anayewakilisha tabaka la wasaka njia - ``hustler'' aliyekulia kwenye maisha ya kawaida na aliyewahi kuwa muuzaji wa kuku tofauti na asili ya familia za rais Kenyatta na Raila Odinga ambao wanatoka katika tabaka la wanasiasa walioitawala Kenya tangu nchi hiyo ilipojipatia uhuru wake mnamo mwaka 1963. Ruto ameahidi kuleta tija kubwa katika kilimo na kuhakikisha kila mkenya kujumuishwa kifedha.

Raila Odinga, Mgombea UraisPicha: Tony Karumba/AFP

Raila Odinga mwenye umri wa miaka 77, aliyefungwa jela mara kadhaa wakati alipokuwa akipigania demokrasia ya vyama vingi cnhini Kenya miongo kadhaa iliyopita, ameahidi kuwazesha kifedha watu masikini na kuhakikisha huduma za afya zinawafikia wakenya wote.

Maswala muhimu kwa Wakenya

Mfanyabiashara, Raia wa KenyaPicha: DW

Masuala muhimu katika kila uchaguzi nchini Kenya huwa ni rushwa na ufisadi Pamoja na uchumi. Wakenya wanakabiliwa na hali ngumu kutokana na kupanda kwa bei ya vyakula na mafuta hali inayochangiwa na vita vya nchini Ukraine na pia hali yao ya kifedha iliyozidi kudhoofika baada ya janga la COVID-19. Zaidi ya theluthi moja ya vijana wa nchi hiyo hawana ajira.

Mshindi wa Urais atatangazwa lini?

Matokeo rasmi yatatangazwa ndani ya wiki moja baada ya zoezi la kupiga kura. Ili kushinda moja kwa moja, mgombea anahitaji kupata zaidi ya nusu ya kura zote na angalau asilimia 25 ya kura katika zaidi ya nusu ya kaunti 47 za nchini Kenya. Iwapo hakutakuwepo na mshindi wa moja kwa moja maana yake ni uchaguzi wa marudio utakaofanyika ndani ya siku 30.

Soma zaidi: Kenya yadhamiria kudhibiti vurugu za uchaguzi

Wagombea au watu wengine huwa na wiki moja ya kuwasilisha pingamizi mahakamani baada ya matokeo kutangazwa. Iwapo mahakama itabatilisha matokeo ya uchaguzi na kuamuru kura mpya basi zoezi hilo litafanyika ndani ya siku 60 baada ya uamuzi wa mahakama

Manmo mwaka 2017 makama kuu ya Kenya ilitoa uamuzi wa kihistoria ilipobatilisha matokeo ya uchaguzi wa rais na kuamuru kura kufanyika mpya.

Vyanzo: AFP/AP

Mhariri: Bakari Ubena

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW