1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUganda

Uchaguzi: Macho ya Tanzania yaelekezwa Uganda

14 Januari 2026

Tanzania inafuatilia mwenendo wa uchaguzi wa Uganda, hatua inayochochewa na ukweli kwamba taifa hilo limetoka hivi karibuni kwenye uchaguzi wake mkuu uliogubikwa na sintofahamu na shutuma za ukiukwaji wa haki za kisiasa.

Uganda | Uchaguzi l Kampala | Robert Kyagulanyi | Yoweri Museveni
Mabango ya wagombea wakuu wa uchaguzi nchini UgandaPicha: Baz Ratner/REUTERS

Nchi jirani ya Tanzania inaufuatilia kwa karibu uchaguzi wa Uganda, hasa ikizingatiwa kuwa hivi karibuni taifa hilo limetoka kwenye uchaguzi wake mkuu uliogubikwa na mazingira ya kutatanisha. Wengi wanaona kuwa baadhi ya matukio yanayojitokeza Uganda yanafanana kwa kiasi kikubwa na yale yaliyoshuhudiwa wakati wa uchaguzi wa Oktoba 29 nchini Tanzania. 

Kwa kawaida, wananchi wa Afrika Mashariki huwa na shauku ya kufuatilia mwenendo wa chaguzi katika nchi wanachama wa jumuiya hiyo.

Hata hivyo, safari hii uchaguzi wa Uganda umevutia macho ya makundi mbalimbali nchini Tanzania kwa namna ya kipekee.

Wananchi wanaujadili uchaguzi huo kwa kuulinganisha na yaliyotokea wakati wa uchaguzi wa Oktoba 29, wakisema Uganda inaonekana kuelekea katika mwelekeo ulioshuhudiwa Tanzania kabla na baada ya uchaguzi mkuu, uliomalizika huku chama tawala Chama Cha Mapinduzi kikiendelea kubaki madarakani.

Uganda na Tanzania katika kioo kimoja

Kubinywa kwa vyama vya upinzani, waandishi wa habari kutiwa msukosuko, pamoja na kuzimwa kwa mtandao wa intaneti ni miongoni mwa sababu zinazowafanya wengi waone kufanana kati ya uchaguzi wa Uganda na ule wa Tanzania.

Wakitoa maoni yao, baadhi ya raia wa Tanzania wanasema kuwa licha ya siasa za Uganda kuamuliwa na Waganda wenyewe, bado kuna wasiwasi kuhusu athari zinazoweza kujitokeza iwapo hali haitakuwa shwari.

Uganda inaelezwa kuwa na idadi kubwa ya vijana, ambao wanatajwa kuwa na nafasi muhimu katika kuamua mwelekeo wa siasa za taifa hilo. Hali hii pia ilikuwa sehemu ya mjadala mpana wakati wa hekaheka za uchaguzi mkuu wa Tanzania uliopita.

Bobi Wine: Hatutavumilia hujuma zozote kwenye uchaguzi

02:12

This browser does not support the video element.

Kwa mujibu wa mtaalamu wa masuala ya maendeleo na uwekezaji kwa vijana, Bob Yona, mara nyingi sauti za vijana hupuuzwa wakati wa kuelekea chaguzi, jambo linalowafanya kukosa fursa ya kuchagua viongozi wanaokidhi mahitaji yao.

Mamlaka nchini Uganda pia zimewekewa lawama kwa kuwabana waangalizi wa kimataifa na kuweka vikwazo kwa vyombo vya habari vya nje kuangazia uchaguzi huo, hali inayofanana na iliyoshuhudiwa wakati wa uchaguzi wa Tanzania.

Akizungumzia hali hiyo, mchambuzi wa siasa Butiku Adamu anasema Uganda inaweza kujiweka katika hatari ya kuathiri mustakabali wake iwapo haitasimamia vyema mchakato wa uchaguzi.

Ingawa hatma ya Uganda itabaki mikononi mwa Waganda wenyewe, mafungamano ya kisiasa, kiuchumi na kijamii ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki yanafanya chochote kitakachojitokeza katika uchaguzi huo kuwa na athari pana kwa wananchi wa jumuiya nzima.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW