1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchaguzi Malawi mgombea wa upinzani aongoza matokeo ya awali

26 Juni 2020

Matokeo ya awali ya uchaguzi wa rais uliorudiwa nchini Malawi yanaonyesha kuwa mgombea wa upinzani Lazarus Chakwera anaongoza kwa asilimia 60, dhidi ya mgombea wa chama tawala na rais wa sasa Peter Mutharika.

Malawi Lilongwe  | Lazarus Chakwera der Malawi Congress Party
Picha: Getty Images/AFP/A. Gumulira

Hayo ni kulingana na ujumuishaji wa kura ambao umefanywa na kituo cha televisheni kinachomilikiwa na serikali MBC. 

Kituo cha televisheni cha MBC kimesema ujumuishaji wao waliofanya siku ya Alhamisi, ni wa kura kutoka katika vituo vyote isipokuwa vitatu tu katika wilaya 28. Kulingana na takwimu zao, Rais Peter Mutharika amepata asilimia 39 ya kura.

Mapema siku ya Alhamisi, chama cha upinzani kilimtangaza mgombea wao Lazarus Chakwera mshindi. Lakini tume inayosimamia uchaguzi imewaambia waandishi wa habari kwamba itawachukua siku mbili au tatu zaidi ndipo waweze kuyatangaza matokeo ya uchaguzi huo uliorudiwa, baada ya mahakama kufutilia matokeo ya uchaguzi wa mwanzo uliofanyika mwaka uliopita kutokana na visa vya udanganyifu. Mwenyekiti wa tume ya uchaguzi Chifundo Kachale ameeleza zaidi kuwa:

"Tume inatambua umuhimu wa kutangaza matokeo kamili na tunafanya kila tuwezalo kuhakikisha tumemaliza mchakato kwa muda ufaao. Lakini hii haitafanywa kwa kugharimu uhalali wa hatua zetu za kuhakikisha ubora wa matokeo."

Rais Peter Mutharika (kushoto) na mgombea wa upinzani Lazarus Chakwera (kulia)Picha: Getty Images/AFP/A. Gumulira

Ikiwa Chakwera mwenye umri wa miaka 65 atatangazwa mshindi, basi ushindi wake, utakuwa pigo kwa Rais Mutharika aliye na umri wa miaka 79 na ambaye amekuwa akiliongoza taifa hilo tangu mwaka 2014.

Uchaguzi wa Malawi, mtihani kwa mahakama za Afrika?

Mahakama ya Malawi ilimkasirisha Mutharika baada ya kuyafuta matokeo yaliyompa ushindi wa uchaguzi wa mwaka 2019. Uamuzi huo pamoja na uchaguzi uliorudiwa Jumanne, ulitizamwa kama mtihani wa uwezo wa mahakama za Afrika kukabiliana na visa vya udanganyifu katika uchaguzi, suala ambalo si geni barani humo.

Mgombea wa upinzani Lazarus Chakwera amesema kwenye taarifa kwamba maadamu kura zote zimehesabiwa na kujumuishwa, ni bayana kuwa Wamalawi wameupa muungano wa upinzani ushindi mkubwa na hatamu ya kuliongoza taifa kwa muhula wa miaka mitano.

Hata hivyo msemaji wa Rais Mutharika hakuzungumza waandishi wa habari walipotaka kujua kauli yake au ya rais.

Matokeo ya uchaguzi wa mwaka jana ambao ulikumbwa na utata, yalisababisha maandamano ya miezi kadhaa ya kuipinga serikali. Jambo ambalo ni nadra sana kutokea nchini Malawi. Awali shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch lilitoa wito kwa Malawi kuhakikisha uchaguzi unaorudiwa unakuwa wa haki.

Hofu ya kutokea machafuko matokeo rasmi yakichelewa

Kumekuwa na maandamano ya miezi kadhaa nchini Malawi tangu uchaguzi wa 2019 ambao ulikumbwa na utata.Picha: Getty Images/AFP/A. Gumulira

Japo Wamalawi wamekuwa na subra kusubiri matokeo rasmi, kumekuwa na hofu ya machafuko zaidi kutokea endapo matokeo rasmi yatachelewa kutangazwa.

Rais wa zamani wa Malawi Bakili Muluzi, ambaye chama chake kinashirikiana na Mutharika, amewahimiza wale watakaoshindwa kuyakubali matokeo na wawapongeze washindi ili kuondoa hofu watu wanaposubiri matokeo kamili.

Uamuzi wa mahakama ya kikatiba Malawi kuubatilisha ushindi wa rais na mahakama ya juu pia kufanya uamuzi kama huo, umefanana na uamuzi uliotolewa na mahakama ya juu nchini Kenya ambapo ushindi wa Rais Kenyatta katika uchaguzi wa mwaka 2017 ulibatilishwa na kurudiwa.

Matukio hayo mawili katika bara la Afrika ambalo mara nyingi korti hazikabiliani vilivyo na marais wanaomiliki nguvu na madaraka makubwa, yaliwashangaza wengi.

Chanzo: RTRE