1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchaguzi mkubwa zaidi duniani waanza India

Admin.WagnerD7 Aprili 2014

Raia chini India leo wameanza kupiga kura katika uchaguzi mkuu mkubwa zaidi duniani ambao unabashiriwa kukiondoa madarakani chama tawala kinachoshutumiwa kwa kushindwa kushughulikia uchumi,ufisadi na uhasama wa kidini

Picha: Reuters

Wapiga kura takriban milioni 814 wanatarajiwa kushiriki katika uchaguzi mkuu unaopiga upatu wa kukiangusha chama tawala cha Congress ambacho kimekuwa madarakani kwa miaka 10 kwa kumchagua mgombea uwaziri mkuu Narenda Modi wa chama cha Bharatiya Janata BJP.

Zoezi hilo la kupiga kura limeanza saa moja asubuhi saa za India katika majimbo yaliyoko kaskazini mashariki mwa nchi hiyo ya Assam na Tripura.Upigaji kura huo unatarajiwa kufanyika kwa awamu tisa kwa wiki tano zijazo hadi tarehe 12 mwezi Mei.

Zaidi ya wapiga kura milioni 814 kushiriki

Uchaguzi huo unasemekana kuwa mkubwa zaidi katika historia na itakuwa kibarua kigumu kwa waandalizi wake huku wapiga kura wakisafiri kupiga kura katika vituo zaidi ya milioni licha ya kuwa mfumo unaotumika ni wa kieletroniki.

Mgombea wa chama cha upinzani BJP Narenda ModiPicha: Reuters

Idadi ya raia nchini India imeongezeka maradufu na zaidi ya wapiga kura milioni 100 wapya wamesajiliwa kushiriki katika uchaguzi huo wa mwaka huu ongezeko kubwa kutoka uchaguzi uliopita miaka mitano iliyopita.

Nusu ya idadi ya raia wa nchi hiyo bilioni 1.2 wako chini ya umri wa miaka 25 na mgombea mkuu wa upinzani Modi mwenye umri wa miaka 63 ana umaarufu mkubwa miongoni mwa vijana kuliko mgombea wa chama tawala Rahul Gandhi mwenye umri wa miaka 43.

Mgombea wa upinzani abashiriwa kushinda

Wapiga kura hao watawachagua pia wabunge 543 na shughuli ya kuanza kuhesabiwa kwa kura itaanza tarehe 16 mwezi ujao na matokeo yanatarajiwa kutangazwa siku hiyo hiyo.

Kwa miaka mingi hakuna chama kimoja cha kisiasa nchini India ambacho kimeweza kujipatia wingi wa wabunge katika bunge ambapo sharti chama kiweze kupata wingi wa wabunge 272 kuunda serikali.

Mpiga kura apiga kura katika kituo cha kupigia kura IndiaPicha: Reuters

Vyama vyote vikuu katika kinyanganyiro hiki, chama tawala cha Congress na BJP vimeungana na vyama vingine vidogo.Waziri mkuu Manmohan Singh amesema hatahudumu kwa kipindi kingineiwapo muungano wa Progressive unaoongozwa na Congress utarejea madarakani, baada ya kuongoza kwa awamu mbili

Kura za maoni kabla ya uchaguzi huo zimenyesha kuwa chama tawala kitapata pigo kufuatia kashfa za ufisadi ambazo zimekisonga na kushukua kwa uchumi katika miaka ya hivi karibuni.BJP ambacho kimeahidi kuufufua uchumi wa India kinabashiriwa kufanya vizuri.Mgombea wake Modi amesifiwa kwa kuukuza uchumi wa jimbo la magharibi mwa India Gujarat ambako amekuwa waziri wake mkuu kwa miaka 11.

Hata hivyo wakereketwa wanatiwa wasiwasi na rekodi yake iliyoingia doa kwa kuhusishwa na uhasama wa kidini uliotokea katika jimbo lake mwaka 2002 ambapo watu zaidi ya 1,000 waliuawa.

Mwandishi:Caro Robi/afp/dpa/ap

Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW