Uchaguzi muhimu katika jimbo la Ujerumani
14 Mei 2017Kampeni za uchaguzi huo wa jimbo , zilimalizika Ijumaa jioni wakati chama cha Kansela wa Ujerumani Angela Merkel cha Christian Democratic Union kikionekana kuwa mbele ya mahasimu wao wa chama cha Social Democratic SPD katika uchunguzi wa maoni ya wapiga kura.
Waziri mkuu wa jimbo hilo kutoka chama cha SPD Hannelore Kraft amekuwa akiongoza katika maoni ya wapiga kura katika uchaguzi huo unaofanyika leo. Lakini maoni kadhaa yaliyochapishwa katika muda wa siku mbili zilizopita yanaonesha chama cha kansela Merkel CDU kimekipita chama cha siasa za wastani za mrengo wa kushoto katika kile kinachojitokeza kuwa kinyang'anyiro cha vuta nikuvute.
Wapigakura milioni 13 ambao wameandikishwa kupiga kura watapiga kura katika uchaguzi unaoshindaniwa na vyama 31 ikiwa ni pamoja na makundi yanayowakilisha haki za wanyama, mrengo mkali wa kushoto na mrengo mkali wa kulia, wahamiaji na watu ambao hawapendelea kula nyama.
Baada ya kufikia asilimia 40 mwezi Machi kufuatia uchaguzi wa chama cha SPD wa kumchagua spika wa zamani wa bunge la Ulaya Martin Schulz kuwa kiongozi wa chama hicho kitaifa, uungwaji mkono wa chama hicho umepungua hadi asilimia 31 kwa mujibu wa maoni ya wapiga kura yaliyotayarishwa na kituo cha televisheni ya taifa cha ZDF na kutolewa siku ya Alhamis.
Matarajio yapanda
Wakati huo huo , chama cha CDU kimepanda na kukipita chama cha SPD na kufikia asilimia 32 katika jimbo hilo, maoni ya wapiga kura kupitia kituo cha televisheni ya ZDF yameonesha , ambayo yanafanana na maoni ya wapiga kura yaliyotayarishwa na kituo kingine cha televisheni cha Sat 1. Uchunguzi mwingine yanayoelekeza katika matokeo ya uchaguzi yanaonesha mpambano wa karibu.
Ushundi kwa CDU katika jimbo la North Rhine Westphalia utakuwa ni msukumo mkubwa kwa Merkel wakati akiingia katika hatua za kujiweka tayari kwa uchaguzi wa taifa mwezi Septemba baada ya ushindi muhimu katika majimbo mengine mawili hivi karibuni.
Kushindwa kwa chama cha SPD kutakuwa pigo kubwa kwa chama hicho na Schulz , ambaye anatoka katika jimbo la North Rhine Westphalia.
"Iwapo SPD itatokea namba mbili , mporomoko utakuwa vigumu kuuzuwia," mtaalamu wa sayansi ya kisiasa Oskar Niedemayer aliliambia shirika la habari la Ujerumani dpa. "Hii itakuwa na maana Martin Schulz anaweza kuzika ndoto zake za kuwa kansela," Niedermayer amesema.
Kansela aiponda serikali ya jimbo
Katika kampeni kansela wa Ujerumani Angela Merkel alisema muungano unaounda serikali ya jimbo hilo unaoendeshwa na wapinzani wao unaendesha serikali kwa "mkopo".
Deni jipya katika jimbo hilo liko juu kuliko katika majimbo mengine nchini Ujerumani, Merkel amesema mbele ya waungaji wake mkono katika mji wa Aachen jana Jumamosi.
"Kuna kitu haikiendi vizuri hapa ," amesema , akidokeza kwamba licha ya deni hilo jipya, idadi ya watoto kwa darasa ni juu katika jimbo hilo kuliko jimbo lolote katika taifa hilo.
CDU inaahidi kitu mbadala kuliko muungano wa SPD na chama cha walinzi wa mazingira The Greens ," Merkel alisema , akitoa wito kwa kiasi wageni 1,200 kwenda kupiga kura leo Jumapili.
Mwandishi: Sekione Kitojo / dpa
Mhariri: Yusra Buwayhid