1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchaguzi nchini Msumbiji: Je, upinzani una nafasi?

8 Oktoba 2024

Jumatano ya tarehe 9 Oktoba, wananchi wa Msumbiji watachagua mkuu mpya wa nchi, wawakilishi wa bunge la kitaifa, pamoja na wabunge wa majimbo na magavana. Je, kuna mgombea anaeweza kushinda chama tawala cha FRELIMO?

Mabango ya kisiasa katika Wilaya ya Boane, Msumbiji
Matangazo ya uchaguzi na chama tawala cha FRELIMO: mwanzo mpya na wagombeaji wapyaPicha: ALFREDO ZUNIGA/AFP/Getty Images

Mji mkuu wa Msumbiji Maputo, umepambwa kwa rangi kali nyekundu kwa wiki kadhaa. Nyekundu ni rangi ya FRELIMO, chama ambacho kimeongoza nchi hiyo tangu uhuru wa nchi hiyo karibu miaka 50 iliyopita. Bendera za FRELIMO ziko kila mahali, hasa tangu tarehe 24 Agosti, siku ambayo kampeni za uchaguzi zilifunguliwa rasmi katika nchi hii ya kusini mashariki mwa Afrika. Mgombea anaepigiwa upatu ni Daniel Chapo kutoka chama tawala.

Anaepigiwa upatu: mgombea wa serikali Daniel Chapo

Rais Filipe Nyusi, ambaye ameiongoza Msumbiji kwa miaka kumi, hakuwa na haki ya kugombea tena kutokana na ukomo wa mihula miwili. Hivyo, FRELIMO ilimteua mgombea mpya, Daniel Chapo, mwenye umri wa miaka 47, ambaye katika miaka minane iliyopita kama gavana wa mkoa wa Inhambane amefanya "kazi nzuri" kulingana na waangalizi wasioengemea upande.

Sasa picha ya mgombea huyo aliyekuwa mtangazaji wa redio na mhadhiri wa sheria inaonekana kila mahali kwenye mitaa ya Maputo, Beira, Nampula, Quelimane na miji mingine ya Msumbiji: kwenye mabango yanayotundikwa kila mahali kwenye nyumba na kuta, kwenye skrini kubwa na majukwaa mengi ya maonesho. Pembeni ya picha ya Daniel Chapo mara nyingi kuna ngoma na mahindi, alama ya chama cha FRELIMO.

Soma pia: Rais wa Msumbiji Filipe Nyusi aanza ziara ya siku tatu nchini Tanzania

Anawania dhidi ya wapinzani watatu katika uchaguzi wa urais unaofanyika leo Jumatano:  Ossufo Momade, Lutero Simango na Venâncio Mondlane. Katika mbio za kupata viti 250 vya bunge, pamoja na FRELIMO, vyama vingine 36 vya kisiasa vimekubaliwa kushiriki. Hata hivyo, kampeni zao hazionekani sana katika maisha ya kila siku. Propaganda yao inaenezwa kupitia mabango machache katika miji mikubwa, kwa kiasi kikubwa ikionyesha sura za wagombea wa urais wanaowaunga mkono.

Daniel Chapo (katika mwonekano wa kampeni mjini Maputo): Je, ni mwenye kiburi na jeuri?Picha: ALFREDO ZUNIGA/AFP/Getty Images

Chapo, mgombea wa FRELIMO, anajitokeza kwa kujiamini katika kampeni. Katika tamko wakati wa kampeni kwenye mkoa wa Niassa, alikabiliwa na shutuma za ufidhuli na dhana. Kwa mfano, alitaja sekta ya elimu, lakini pia, na zaidi, huduma za afya za umma: Watu wanakwenda hospitali na wanasahau kuwa hospitali imejengwa na FRELIMO, wanakunywa dawa na kusahau kuwa dawa hizo ziliagizwa na FRELIMO, na wakipata nafuu na kupona wanasema FRELIMO haijafanya lolote kwa nchi yetu. Hicho nakiita ukosefu wa shukuran.

Maneno hayo kwa vyama vingi vya upinzani yanaeleza jinsi taasisi za serikali zinavyotumika kwa utaratibu - na kinyume cha sheria - kwa manufaa ya chama tawala cha FRELIMO.

Kulingana na Tume ya Uchaguzi ya Taifa, CNE, zaidi ya watu milioni 17 wa Msumbiji wamejiandikisha kama wapiga kura, wakiwemo 333,839 wanaoishi nje ya nchi. Kabla ya siku ya uchaguzi, msemaji wa CNE, Paulo Cuinica, alikiri katika mahojiano na DW kwamba kumekuwa na matatizo kadhaa kabla ya uchaguzi - ikiwemo utolewaji wa fedha za kampeni zilizopangwa na serikali, hasa kwa vyama vidogo, lakini alisema kwa ujumla maandalizi yamewenda vizuri.

Ossufo Momade

Mgombea wa chama kikuu cha upinzani cha RENAMO, Ossufo Momade anachukuliwa kuwa mgombea mwenye nafasi bora zaidi ya upinzani: vyama vidogo vinane pia vimesimama nyuma yake katika kinyang'anyiro cha urais. Hata hivyo, Momade anakabiliwa na changamoto kubwa: kampeni yake haionyeshi shauku yoyote.

Ossufo Momade (akiwa Chinhambudzi mwishoni mwa Septemba): Hakukuwa na hamasa katika kampeni za uchaguzi.Picha: Bernardo Jequete/DW

Mnamo mwaka 2018, alichukua nafasi ya kiongozi aliyefariki Afonso Dhlakama katika chama cha zamani cha waasi cha RENAMO. Lakini Momade hakuweza kutatua migogoro ya ndani ya chama ambayo ilijitokeza baada ya kifo cha Dhlakama. Kinyume chake, wanachama wengi wa chama walionekana kutengwa na uongozi mpya wa chama na kuunda vyama vipya vinavyoshindana na RENAMO.

Soma pia: Uchaguzi wa rais nchini Msumbiji unakutanisha wagombea wanne

Hata ndani ya chama, kuna kutokuridhika fulani kuhusu Ossufo Momade. Wapinzani wa ndani wanasema hana ari ya kutosha. Inaonekana kana kwamba ameridhika na jukumu la kuwa kiongozi wa upinzani. Katika kampeni hii, Momade alikuwa alionekana kuwa alietulizwa na hakuonyesha ujasiri.

Ni mara chache alikosoa chama cha serikali kwa maneno makali, kama mwanzoni mwa Septemba. Katika mji wa Nampula, Momade aliwaambia wapiga kura kuwa "chama cha FRELIMO kinachokifanya kuwa na udhibiti na chenye nguvu ni kwa sababu kinatumia taasisi za serikali, ikiwa ni pamoja na polisi, kuimarisha na kudhibiti upinzani.

Lutero Simango

Lutero Simango ni mgombea wa Movimento Democrático de Moçambique, MDM, chama cha tatu kwa ukubwa bungeni. Chama hicho kinataka hasa mabadiliko ya mfumo wa kisiasa nchini Msumbiji. Katika kampeni, Simango alisisitiza mara nyingi kwamba nchi haisogei kwa sababu katiba ya Jamhuri hailindi uhuru wa taasisi: "Hatuwezi kuendelea kuwa na katiba inayompa rais wa jamhuri mamlaka yasio kikomo. Zaidi ya hayo, kuna chama, FRELIMO, kinachotawala kwa kila ngazi, wakati vyama vingine vinanyanyaswa. Msumbiji ilipata uhuru mwaka 1975, lakini bado tuna serikali ya chama moja, inayoongozwa na chama kimoja. Hali hiyo haiwezi kuendelea. Tunataka kuunda jamii shirikishi, na ya kidemokrasia zaidi," aliahidi kwa wapiga kura.

Lutero Simango pamoja na wafuasi wake huko Manica: Mabadiliko kama ahadi ya uchaguziPicha: Bernardo Jequete/DW

Soma pia: Mashambulizi ya wapiganaji yawahamisha maelfu Msumbiji

Hata hivyo, waangalizi huru wanasema chama cha MDM hakina uhamasishaji na nguvu ya shauku inayohitajika kwa ushindi wa uchaguzi. Lutero Simango hajawahi kuweza kujitoa kwenye kivuli cha kaka yake aliyefariki Daviz Simango, ambaye alikuwa sura kuu ya chama cha MDM na ambaye alimrithi kama mwenyekiti wa chama mwaka 2021.

Venâncio Mondlane

Venâncio Mondlane ndiye mgombea mtata zaidi kati ya wagombea wanne wa urais nchini Msumbiji. Wakosoaji wanamwita msemaji huyo wa zamani wa RENAMO kuwa mpopulisti asiyetabirika. Lakini vijana hasa katika miji mikubwa wanamuona kama taa ya matumaini.

Mondlane alijiondoa katika RENAMO mwezi Juni 2024 na kuacha wadhifa wake wa uwakilishi bungeni. Muda mfupi baadaye alitangaza kuanzisha chama chake cha Muungano wa Shirikisho la Demokrasia - na kutangaza kwamba atagombea urais katika uchaguzi wa tarehe 9 Oktoba 2024.

Hata hivyo, chama chake kipya kiliondolewa na Tume ya Uchaguzi ya CNE kwenye uchaguzi wa bunge - kwa madai ya makosa ya utaratibu. Hiyo si haki, alisema mgombea huyo: "Tuna haki za kisiasa katika mfumo wetu wa kidemokrasia, na tunataka kuzitumia," alisema Venâncio Mondlane katika mahojiano na DW.

Venâncio Mondlane (picha ya maktaba): "Hatutakubali hali iliyopo iendelee."Picha: Cristiane Vieira Teixeira/DW

Na alihitimisha kwa kusema: "Tutapigana na hatutakubali kunyamazishwa na mifumo ya madaraka iliyopo.

Mondlane anaungwa mkono na vyama vidogo vilivyo na wabunge, vya "Povo Otimista para o Desenvolvimento deMoçambique" (PODEMOS) na "Revolução Democrática" (RD).