Uchaguzi Tanzania: Gharama za kampeni kwa walemavu
10 Oktoba 2025
Hamasa na shamrashamra ndio wakati wake muda huu wa kampeni, ambapo wagombea wanaingia wiki za lala salama kuwashawishi wapigakura. Lakini kwa wengine, wamesalia kuwa wasindikizaji wa macho katika kunadi sera zao.
Changamoto kubwa zaidi kwa wagombea wenye ulemavu ni kupungukiwa na rasilimali ikiwamo fedha, jambo linalowatia shaka wagombea wa kundi hili iwapo wanaweza kuvuna chochote wakati wapiga kura watapoteremka katika vituo vya kupigia kura hapo Oktoba 29.
Kondo Adulsheif, mgombea mwenye ulemavu anayewania nafasi ya ubunge kupitia Chama cha Wananchi, CUF, wilayani Kisarawe, anasema hadi sasa hajapanda katika majukwaa ya kampeni kuzungumza na wapiga kura na kwamba hali hiyo inamzidishia wasiwasi iwapo ataweza kutimiza ndoto yake ya kwenda bungeni:
Katika chaguzi za mara zote, makundi yanayojulikana kama maalumu ambayo ni vijana, wanawake na watu wenye mahitaji maalumu yamekuwa yakipewa msukumo kujitokeza kwa wingi kwa ajili ya kuwania nafasi za uongozi, na kwenye uchaguzi huu wameitikia shinikizo hilo.
Kilio cha wagombea walemavu kinapaswa kutizamwa kwa karibu
Katika kampeni zao, makundi hayo yanapigwa jeki na kaulimbiu kwamba kuyawezesha makundi hayo ni kuinua jamii kutokuwa tegemezi.
Lakini Ndonge Said Ndonge ambaye amejitokeza kuwania ubunge, anashangaa kuona kwamba vyama vya siasa vinasaidiwa na Tume Huru ya Uchaguzi, kwa mfano wale wagombea wa urais waliopewa magari, ilihali watu wenye mahitaji maalumu kama yeye wakiendelea kuachwa:
Hata kama sheria hailazimishi mamlaka wala taasisi kuwasaidia kifedha na rasilimali wagombea kama hawa wenye mahitaji maalum, wafuatiliaji wa mambo wanasema kilio cha wagombea hao kinapaswa kutizamwa kwa jicho la pili, wakiamini kuwa mchakato wa kidemokrasia unapaswa kuanzia ndani ya vyama vyenyewe.
Makwaya Shija ambaye amekuwa akifuatilia kampeni za uchaguzi huu anasema mzigo wa lawama unapaswa kutupwa kwa vyama vyenyewe kwa kushindwa kufanya maandalizi ya kuwawezesha wagombea hao, hasa kwa vile vyama vinavyopokea ruzuku:
Hivi sasa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) iko mbioni kuanza kutoa machapisho yatakayowatambulisha wagombea watakaopigiwa kura, lakini kwa hali hii, wako ambao watakuwamo kwenye karatasi za kura ilhali wenyewe hawajahipo kwenda mitaani kuomba kura hizo.