Uchaguzi wa Baba Mtakatifu unaendelea:
19 Aprili 2005Vatikani:
Makadinali 115 wa Kanisa Katoliki kutoka nchi 52 leo wanaendelea na jukumu lao muhimu la kumchagua Baba Mtakatifu mpya wa 265 atakayechukua mahali pa hayati Baba Mtakatifu Yohana Paulo II. Jana wameshindwa kumchagua Baba Mtakatifu mpya. Makadinali hao, wanaojifungia ndani ya Kanisa la Mtakatifu Sisilia wakiwa hawana mawasiliano na ulimwengu wa nje, kuanzia leo watalazimika kupiga kura mara nne kwa siku. Leo asubuhi watapiga kura mara mbili. Ikiwa hawatampata Kiongozi mpya wa Kanisa Katoliki kwa wingi wa theluthi mbili watalazimika kupiga kura tena mara mbili leo mchana. Matokeo ya uchaguzi wao yanafahamishwa kwa ishara ya moshi. Ikiwa moshi mweusi utatokea juu ya paa la Kanisa la Mtakatifu Sisilia utaonyesha kuwa Baba Mtakatifu bado hajachaguliwa. Lakini ikiwa moshi mweupe utaonekana na kengele za Kanisa la Mtakatifu Petro zitapigwa itamaanisha kuwa Kiongozi mpya wa Wakatoliki Billioni moja na nukta moja amechaguliwa.