1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchaguzi wa Bavaria magazetini

16 Septemba 2013

Mada moja tuu imehodhi vichwa vya habari magazetini.Ushindi mkubwa wa chama cha kihafidhina CSU katika uchaguzi wa jimbo la kusini la Bavaria na matokeo yake kwa uchaguzi mkuu wa september 22 ijayo nchini Ujerumani.

Waziri mkuu wa zamani na mpya wa jimbo la Bavaria Horst SeehoferPicha: Reuters

Gazeti la "Braunschweiger Zeitung" linaandika:"Horst Seehofer hajashinda uchaguzi tu,amepanda kileleni mwa chama cha CSU.Baada ya wana Christian Social Union kuporomoka katika uchaguzi wa jimbo mwaka 2008,Seehofer amekirejeshea chama hicho wingi mkubwa wa viti bungeni-na hilo marafiki zake kokote kule waliko kamwe hawatalisahau.Kudhibiti peke yao madaraka ni muhimu zaidi kwa chama hicho kuliko kujikuta katika hali ya kutamani nani washirikiane nae.Wanajiamini wana CSU na kufika hadi ya kuamini hata Mungu anawaamini.

Waziri wa mambo ya nchi za nje Guido Westerwelle na waziri wa afya Daniel Bahr,wote wa chama cha FDP-wameduwaa baada ya matokeo ya uchaguzi wa Bavaria kutangazwaPicha: picture-alliance/dpa

Kishindo Kwa CDU

Ushindi mkubwa wa chama cha CSU huko Bavaria ni kishindo kwa chama ndugu cha CDU cha kansela Angela Merkel linaandika gazeti la "Donaukurier" na kuendelea:"Hata kama watu hawatamtaja Horst Seehofer kuwa "mwokozi wa chama cha CSU-kimoja hakuna anaeweza kukibisha: amekirejeshea chama hicho dira yake ya kisiasa.Na zaidi kuliko yote,Seehofer amekirejeshea nguvu zake za jadi chama hicho katika jukwaa la kisiasa mjini Berlin.Anaranda madarakani kusini mwa Ujerumani na wakati huo huo kushawishi mkondo wa mambo katika siasa za serikali ya kansela Merkel mjini Berlin.


Ushindi mkubwa wa CSU unamkosesha usingizi kansela Angela Merkel wiki moja kabla ya uchaguzi mkuu,linaandika gazeti la Badische Zeitung:"Angela Merkel ameupokea ushindi wa CSU kwa furaha na huzuni.Kwa furaha kwasababu hali imara ya kiuchumi ya Bavaria ndio sababu kwanini wapigakura wengi wameona bora mambo yaendelee kama yalivyo.Na huzuni kwasababu Seehofer,pindi vyama ndugu vya CDU/CSU vikishinda uchaguzi mkuu september 22 ijayo,atakuwa mshirika shupavu zaidi kuliko namna alivyo hivi sasa.Halafu kuna tatizo la chama cha FDP.Kwamba waliberali wameshindwa kukiuka kiunzi cha asili mia tano kuweza kuwakilishwa katika bunge la mjini Munich,inaifanya hali ya kansela Merkel izidi kuwa ngumu.Hivi sasa FDP wanataka kujaribu kunyakua kura ya pili ya vyama ndugu vya CDU/CSU.Wakifanikiwa basi hali hiyo inaweza kukiathiri chama cha kansela na kuyamwagia mchanga matumaini ya kuendelea na muungano wa vyama vya CDU/CSU na waliberali.

Ukweli utajulikana september 22

Gazeti la Hannoversche Allgemeine Zeitung linatathmini matokeo ya uchaguzi wa Bavaria kwa kuzingatia vyama vya upinzani vya SPD na walinzi wa mazingira die Grüne.Gazeti linaendelea kuandika:"

SPD na walinzi wa mazingira de Grüne wanasherehekea kupigwa kumbo chama cha FDP katika bunge la Bavaria kana kwamba ni ushindi wao katika pambano dhidi ya CDU/CSU na FDP.Si chengine isipokuwa dhihaka.Kwasababu ukiangalia kindani ndani hutakosa kugundua matokeo ya uchaguzi wa Bavaria hayatoi matumaini kwa yeyote si SPD na wala si walinzi wa mazingira die Grüne ya kufanya vyema uchaguzi mkuu utakapoitishwa wiki moja kutoka sasa.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir(Inlnadspresse

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW