1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchaguzi wa bunge la Ulaya wafikia kileleni

Mohamed Dahman25 Mei 2014

Wananchi wa Ulaya Jumapili (25.05.2014) wanapiga kura katika uchaguzi wa bunge la Umoja wa Ulaya ikiwa ni kilele cha mchakato mkubwa unaotarajiwa kuviimarisha vyama vyenye mashaka na Umoja wa Ulaya.

Bunge la Umoja wa Ulaya mjini Brussels.
Bunge la Umoja wa Ulaya mjini Brussels.Picha: DW/A. Noll

Nchi wanachama ishirini na moja wa Umoja wa Ulaya zikiwemo Ujerumani,Ufaransa na Italia zinashiriki uchaguzi huo leo hii kukamilisha siku nne za uchaguzi ulioanza nchini Uingereza na Uholanzi hapo Alhamisi.

Ugiriki,Romania na Lithuania zimeanza kupiga kura saa sita mchana saa za Ulaya ya Kati lakini hakuna matokeo yatakayotangazwa kutoka nchi hizo hadi hapo kura zitakapomalizika kupigwa saa tano za usiku.

Iwapo uchunguzi wa maoni utakuja kuwa sahihi vyama vyenye mashaka na kupinga Umoja wa Ulaya vinaweza kuzidisha uwepo wao mara tatu zaidi kufikia viti 100 katika bunge hilo jipya la Umoja wa Ulaya lenye viti 751.

Nchini Denmark,Ufaransa na Italia vyama vyenye kupinga Umoja wa Ulaya vinatazamiwa kushika nafasi ya pili katika uchaguzi huu wa Jumapili na kutibua siasa za kitaifa na kujiandaa kupambana na Umoja wa Ulaya ndani ya taasisi hiyo.

Nchini Uingereza chama chenye mashaka na Umoja wa Ulaya cha UK Independence (UKIP) kinachoongozwa na Nigel Farage chama ambacho hakina hata kiti kimoja katika bunge la taifa kimeibuka kwa nguvu hapo Alhamisi katika uchaguzi wa serikali za mitaa ambao umefanyika sambamba na ule wa Umoja wa Ulaya na kuutingisha utawala.

Idadi ndogo ya wapiga kura

Kujitokeza kwa idadi ndogo ya wapiga kura yumkini kukaonyesha kukatishwa tamaa kunakongezeka na Umoja wa Ulaya ambapo idadi hiyo inaweza kupunguwa zaidi kuwa hata chini ya asilimia 43 ambayo ni rekodi iliyowekwa hapo mwaka 2009.

Zoezi la kupiga kura Athens,Ugiriki. (25.05.2014)Picha: SARIS MESSINIS/AFP/Getty Images

Mkurugenzi wa Carnegie Europe Wakfu wa Kimataifa wa Amani kwa Ulaya Jan Techau ameliambia shirika la habari la AFP kwamba "kuna tatizo la uhalali".

Lakini amesema ushindi kwa vyama hivyo vya pembeni hautokwamisha au kubadili njia ya jinsi bunge la Umoja wa Ulaya linavyofanya kazi.

Uchunguzi wa maoni unadokeza kwamba vyama vikuu vya kisiasa vilivyozoeleka,vyama vya kihafidhina vya sera za mrengo wa wastani kulia na vile vya sera za wastani za kisoshalisti vitashikilia asilimia sabini ya viti katika bunge jipya.

Wachambuzi wanasema kwa desturi vimekuwa vikishirikiana kwa muda wote huo na vinapaswa kuendelea kufanya hivyo.

Mapungufu ya demokrasia

Kutokana na kukabiliwa na kuongezeka kwa uhasimu dhidi ya urasimu wa Umoja Ulaya na sera za kubana matumizi zilizopitishwa ili kukabliana na mzozo wa madeni,viongozi wa kisiasa wa Umoja Ulaya wamejitahidi kusahihisha kile kinachoitwa "mapungufu ya demokrasia."

Kwa mara ya kwanza makundi matano makuu bungeni yamewatangaza wagombea wao kuwania nafasi ya kuwa mkuu mpya wa Halmashauri yeye nguvu ya Umoja Ulaya na kuwanadi katika mkondo wa kampeni.

Waziri Mkuu wa Ubelgiji Elio Di Rupo (kulia) akipiga kura yake. (25.05.2014)Picha: Benoit Doppagne/AFP/Getty Images

Pia iliandaliwa midahalo ya televisheni baina ya wagombea hao na kuwapambanisha moja kwa moja na masuala magumu ya wananchi.

Likijumuisha matumaini ya kuwasiliana upya na wananchi milioni 500 wa umoja huo, tangazo kubwa lililotundikwa makao makuu ya Umoja Ulaya mjini Brussels Ubelgiji linasomeka "Huu ni wakati tafauti---Kura yako ni muhimu."

Hata wachambuzi wana mashaka na kipengele hicho.

Jean - Dominique Giullani wa Wakfu wa Robert Schuman anasema jaribio la bunge la Ulaya kulifanya suala hilo la kura kuwa la kisiasa na la mtu binafsi halikufanikiwa.

Badala yake wale wenye mashaka na Umoja Ulaya na makundi zaidi ya misimamo mikali wameunga mkono masuala ya kupinga uhamiaji na Umoja wa Ulaya yaliokuja kuwa nyeti wakati watu milioni 26 walipokuwa hawana kazi wakiwemo zaidi ya nusu walio na umri wa chini ya miaka 25 katika nchi kama vile Ugiriki na Uhispania.

Techau anasema ni jambo la wazi kwamba uchaguzi huu hauwezi tu kwenda kama ulivyo kwa sababu watu hawalioni bunge la Ulaya kuwa na uzito wa kisiasa. Anasema "Inabidi kuwepo na mageuzi makubwa sana."

Hofu Mashariki mwa Ulaya

Kinyume na hali ilivyo mashariki mwa Ulaya,mzozo wa Ukraine na hofu ya kuibuka upya kwa Urusi inaonekana kumeimarisha mvuto wa kuwa na uhusiano na Umoja Ulaya na usalama inaoutowa.

Rais Dalia Grybauskaite wa Lithuania akipiga kura yake Vilnius. (25.05.2014)Picha: Reuters

Nchini Lithuania, mtumishi wa serikali mwenye umri wa miaka 44 Jurate Kiserauske amesema Umoja Ulaya "ni muokovu na mustakabali wetu pekee.Ikiwa hatutokuwepo kwenye umoja huo,hatutobakia hapa tulipo hivi sasa bali tutarudishwa tena Urusi katika Muungano wa Kisovieti."

Miongoni wa wapiga kura waliojitokeza kupiga kura zao na mapema leo hii nchini Romania ambayo imejiunga na Umoja Ulaya hapo mwaka 2007 ni mstaafu Didina Nicolae mwenye umri wa miaka 78.

Ameliambia shirika la habari la AFP "Nimekwenda kupiga kura kwa sababu nataka Romania iwe nchi ya Umoja Ulaya ikiwa na hali nzuri ya maisha."

Hapo Jumamosi,wapiga kura katika Jamhuri ya Czech waliviunga mkono vyama vitatu vyenye kupendelea Umoja Ulaya wakati nchini Latvia chama cha sera kali za mrengo wa kulia cha Wananchi wa Ulaya (EPP) kilishika nafasi ya tatu katika uchaguzi.

Kwa mfano uchunguzi wa maoni uliofanywa hivi karibuni na Kituo cha Utafiti cha Pew umeonyesha asilimia 72 wanaunga mkono Umoja Ulaya nchini Poland.

Utabiri wa jumla

Kwa jumla uchunguzi wa maoni wa hivi karibuni kabisa uliofanywa na taasisi ya PollWatch umetabiri ushindi kwenye visanduku vya kura wa viti 217 kwa chama cha Wananchi wa Ulaya (EEP) cha sera za mrengo wa wastani kulia dhidi ya 201 kwa Wasoshalisti na Wanademokrasia (S&D).

Bango la uchaguzi wa bunge la Ulaya nchini Ujerumani.Picha: picture-alliance/dpa

Matokeo ya uchaguzi wa bunge hilo la Umoja wa Ulaya ambalo linatarajiwa kuwa litakuwa limegawika sana yatatangazwa Jumatatu usiku.

Viongozi wa bunge watakutana Mei 27 asubuhi kujadili matokeo ya uchaguzi huo na Urais wa Halmashauri ya Umoja wa Ulaya wakati viongozi wa umoja huo watafanya hivyo hivyo katika mkutano wao wa kilele utakaofanyika pia siku hiyo wakati wa jioni.

Inatazamiwa kuchukuwa wiki kadhaa kabla ya viongozi hao kuamuwa juu ya mgombea wa kupigiwa kura bungeni kushika wadhifa wa kuwa mkuu mpya wa Umoja wa Ulaya.

Mwandishi : Mohamed Dahman/AFP/Reuters

Mhariri : Bruce Amani