1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchaguzi wa bunge waghubikwa na machafuko nchini Mali

Saleh Mwanamilongo
20 Aprili 2020

Duru ya pili ya uchaguzi wa bunge nchini Mali ilighubikwa na ghasia ambazo zilisababisha baadhi ya wapigaji kura kutojitokeza.Licha ya makundi ya kigaidi na ugonjwa wa Corona nchini humo.

Zoezi la kuhesabu kura za uchaguzi wa bunge nchini Mali.
Zoezi la kuhesabu kura za uchaguzi wa bunge nchini Mali.Picha: imago images/Afrikimages/A. Keita

Duru ya pili ya uchaguzi wa bunge nchini Mali ilighubikwa na ghasia ambazo zilisababisha baadhi ya wapigaji kura kutojitokeza. Licha ya makundi ya kigaidi na ugonjwa wa Corona nchini humo,viongozi walishikilia kuitisha uchaguzi huo ambao matokeo yake yanatarajiwa kutolewa katikati mwa wiki hii. 

Idadi ya waliojitokeza kupiga kura Jumapili imekadiriwa kuwa ni asilimia 23.2 kwa mujibu wa mashirika ya kiraia yaliyowasilisha wachunguzi wake kote nchini. Uchaguzi huo ulighubikwa na machafuko kwenye mji wa Ouro-Mody, kwenye jimbo la Mopti katikati mwa nchi ambako kiongozi wa kituo kimojawapo cha kupigia kura alitekwa nyara huku wanachama wengine wa tume huru ya uchaguzi wakifukuzwa na watu walioshikilia silaha.

Kwenye miji ya SoSobe na Togorougoumbe katikati mwa nchi, vituo vyote havikufungua kufuatia vitisho vya magaidi wanaodhibiti maeneo hayo dhidi ya wapigaji kura. Ni kwenye eneo hilo hilo ambako kiongozi wa upinzani Soumaila Cisse alitekwa nyara tarehe 25 Machi wakati alipokuwa akiendesha kampeni ya uchaguzi. Inaaminika kwamba ni kundi la kigaidi linaloongozwa na Amadou Kouffa ambalo lilimteka nyara. Kwa mujibu wa chama chake cha kisiasa mazungumzo yanaendeshwa kwa ajili ya kuachiwa huru.

Vifaa vya uchaguzi viliharibiwa mkesha wa uchaguzi kwenye mji wa Gossi, jimboni Gao, kaskazini mwa Mali, alisema mmoja wa wabunge wa mji huo.

Rais wa Mali Ibrahim Boubacar Keita (left) na kiongozi wa upinzani Soumaila Cisse.

Kasoro za uchaguzi

Wapigakura hawakujitokeza pia kwenye miji ya Talataye na Ouatagouna jimboni Liptako kwenye mpaka wa Mali na Niger pamoja na Burkina Faso, yalielezea mashirika ya kiraia kwenye taarifa yao. Kwenye vijiji kadhaa vya jimbo la Timbouctou, huko kaskazini mwa Mali pia vituo vya kupigia kura havikufunguliwa.

Mashirika ya kiraia yanaelezea kwamba kulikuweko visa vya wizi wa kura kwenye vituo vingi vya kupigia kura. Baadhi ya wanasiasa waliunga mkono hatua ya kuitishwa uchaguzi huo ambao uliakhirishwa mara kadhaa kutokana na usalama mdogo.

Uchaguzi unalenga kuweko na bunge jipya kufuatia uchaguzi wa mwaka 2013 na ambao muhula wa wabunge walioko hivi sasa ulitakiwa kumalizika 2018. Uchaguzi huo ni mojawapo pia ya vipengee muhimu vya mkataba wa amani uliotiwa saini mjini Algiers mwaka 2015 baina ya serikali na makundi ya waasi.

 Kwenye duru ya kwanza ya uchaguzi huo zaidi ya vituo elfu mmoja miongoni mwa vituo 22 elfu havikufunguliwa. Katika mji mkuu Bamako idadi ya waliojitokeza kwenye duru ya kwanza ya uchaguzi huo ilikuwa ni asilimia 12 ya wapigakura. Bunge la Mali lina viti 147 na tayari wabunge ishirini na mbili walichaguliwa kwenye duru ya kwanza ya uchaguzi huo akiwemo kiongozi wa upinzani Soumaila Cisse.