Uchaguzi wa Guinea: Rais Alpha Conde awania muhula wa tatu
18 Oktoba 2020Hatua ya Conde ya kuwania muhula mwingine wa urais imesababisha ghasia na chuki miongoni mwa watu wa Guinea. Rais Alpha Conde mwenye umri wa miaka 82 anagombea muhula wa tatu baada ya katiba kubadilishwa. Kwa mujibu wa shirika la haki za binadamu la Amnesty International, takribani watu 50, wengi wao wakiwa wapinzani, waliuawa mnamo mwaka uliopita kwenye maandamano ya kupinga kubadilishwa kwa katiba nchini Guinea. Amnesty International imesema vurugu zilitokea kwa mfululizo katika kipindi cha wiki za hivi karibuni wakati wa kampeni.
Conde, aliwaambia wafuasi wake katika mkutano wake wa mwisho wa kampeni siku ya Ijumaa uliofanyika kwenye uwanja wa mpira katika mji mkuu, Conakry kwamba mageuzi ya katiba yaliyoidhinishwa katika kura ya maoni mnamo mwezi Machi yalikuwa ya haki na ya kidemokrasia, amesema anahitaji muda zaidi madarakani kuweza kumaliza mipango mikubwa katika sekta ya madini makubwa na miradi ya kuboresha miundombinu.
Guinea imepiga maendeleo katika kukuza utajiri wake wa madini, ambapo pato la taifa hilo limeimarika maradufu chini ya utawala wa rais Conde lakini raia wengi wanalalamika kwamba kuongezeka ufanisi huo katika sekta ya madini bado hakujaleta tija ya kumalizika tatizo kubwa la ukosefu wa umeme pamoja na ukosefu wa ajira nchini humo.
Taifa hilo la Afrika Magharibi limekumbwa na vipindi kadhaa vya machafuko ya kisiasa tangu lilipopata uhuru wake kutoka kwa Ufaransa mnamo mwaka 1958, mara nyingi machafuko hayo huchochewa na migogoro ya kikabila.
Alpha Conde anakabiliwa na wapinzani 11, pamoja na mpinzani wake wa muda mrefu Cellou Dalein Diallo. Diallo, waziri mkuu wa zamani alishindwa na rais Conde kwenye chaguzi za mwaka 2010 na 2015, ametahadharisha kuhusu matokeo ya udanganyifu kwenye uchaguzi na wakati huo huo amesema hatosita kupinga matokeo ya uchaguzi wa leo iwapo kutajitokeza kasoro yoyote katika zoezi la upigaji kura.
Wakati ambapo hakuna kura ya maoni inayoaminika nchini Guinea, wachambuzi wengi wa siasa wanatarajia kuwa rais Conde atashinda baada ya kupata idhini kwa kiwango kikubwa kwenye kura ya maoni juu ya kubadili katiba ya mwezi Machi ingawa upinzani ulisusia kura hiyo.
Umoja wa Mataifa ulitoa tahadhari juu ya kuchochea migawanyiko ya kikabila kwenye mikutano ya kampeni. Conde na Diallo wote wawili wanategemea zaidi uungwaji mkono kutoka kwa wapiga kura wa makabila yao.
Vyanzo:/RTRE/AFP