1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kwa nini India haipigii debe mabadiliko ya tabianchi?

13 Mei 2024

Suala la mabadiliko ya tabianchi halijapewa uzito mkubwa miongoni mwa masuala yaliyohanikiza ajenda za kampeni katika uchaguzi wa nchini India, licha ya kitisho kilichopo kutokana na mabadiliko hayo.

India | Uchaguzi wa bunge 2024 | Waziri Mkuu wa India Narendra Modi
Waziri Mkuu wa India Narendra Modi akionyesha kidole baada ya kupiga kura kwenye uchaguzi unaoendelea nchini humoPicha: Ajit Solanki/AP Photo/picture alliance

Wakati Mto Yamuna unaopita katika eneo la mji mkuu wa India ulipofurika na kupasua kingo zake mwaka uliopita, mji huo wa New Delhi ulijikuta ukikabiliwa na dharura ya mafuriko. Ni katika hali hiyo ya janga, ndipo Bhagwati Devi aliyekuwa akilima kijibustani  kidogo cha mboga katika eneo la tambarare la Yamuna kwenye viunga vya New Delhi alihamishwa na kupelekwa kwenye maeneo ya miinuko.

"Tulilazimika kuning'inia kwenye miti kwa usiku mzima kabla ya kuokolewa," anasema mwanamama huyo wa miaka 37 na kuongeza kuwa wiki zilizofuata zilikuwa ngumu mno kwake na hasa baada ya kibanda alichokuwa akiishi kusombwa na maji, pamoja na mali zilizokuwemo, na hata mazao yake pia yalisombwa.

Wataalamu wa mazingira walisema haya yote yamesababishwa na mvua kubwa katika majimbo ya kaskazini mwa India pamoja na mpango wa hovyo wa makazi kwenye jiji la New Delhi.

Mwaka huu, Devi atapiga kura yake kwenye uchaguzi unaoendelea nchini humo. Lakini, kwa kuwa hana taarifa za namna sayansi ya mabadiliko ya hali ya hewa, inavyosababisha hasara kwenye maisha yake ya kila siku, hili halitaathiri kura yake.

Soma pia: Raia wapiga kura India

Na si kwa Devi peke yake kwa sababu suala hili la mabadiliko ya tabianchi limepuuzwa hata katika siasa za uchaguzi nchini India.

Magari yakiwa yamezama kwenye maji baada ya mafuriko yaliyosababishwa na mvua kubwa ya ghafla iliyonyesha katika mji wa Rangpo huko Sikkim, India, Oktoba 5. 2023.Picha: Prakash Adhikari/AP Photo/picture alliance

Kwa nini suala la mazingira halijapigiwa upatu kwenye uchaguzi?

Wataalamu wanasema suala la hali ya hewa huwa halikosekani katika mijadala nchini India, lakini huwa linazungumzwa kwa namna tofauti. Mtaalamu kutoka taasisi ya masuala ya mazingira ya Sustainable Futures Collaborative yenye makao yake mjini New Delhi Valiathan Pillai anasema wanasiasa huwa hawayazungumzii moja kwa moja mabadiliko ya tabianchi kama "mabadiliko ya tabianchi" lakini anasema hii haimaanishi kwamba suala hilo halimo kwenye ajenda za kisiasa za India.   

Soma pia:Indian yarejea kwenye uchaguzi katikati ya kitisho cha joto 

Amesema tofauti iliyopo kwa India ni kwamba kwa kiasi kikubwa wanasiasa wanajishughulisha zaidi kutatua athari zilizotokana na mabadiliko ya tabianchi badala ya kiini cha tatizo lenyewe la kupanda kwa kiwango cha joto kwenye uso wa dunia.

Lakini Aarti Khosla, mwanzilishi wa taasisi ya Climate Trends iliyojikita katika tafiti kwa upande wake amesema watu wengi bado wanalichukulia kirahisi suala la mabadiliko ya tabianchi. Ila huliona kama ni tatizo wakati linapoibua changamoto nyingine.

Mchakato wa uchaguzi nchini India umeathiriwa na joto kali kama inavyoonekana pichani mgombea kwenye uchaguzi akiwa anakunywa maji ya dafu huku akiwa ametota kwa jasho kutokana na joto kaliPicha: Satyajit Shaw/DW

Wapiga kura wa India wanaonaje mabadiliko ya hali ya hewa?

Waangalizi hata hivyo wanaamini kwamba kuna ongezeko la ufahamu kuhusu mabadiliko ya hali ya hewa nchini India.

Uchunguzi uliofanyika mwaka 2022 umeonyesha asilimia 9 ya Wahindi walisema wanafahamu mengi kuhusu ongezeko la joto ulimwenguni. Lakini walipopewa ufafanuzi japo kidogo tu kuhusu ongezeko hilo, asilimia 84 walikiri kwamba kuna ongezeko la joto.

Utafiti huo lakini ulionyesha asilimia 81 ya Wahindi bado wana wasiwasi sana juu ya ongezeko la joto duniani. Lakini licha ya wasiwasi huo kuongezeka, bado suala hili halijapewa uzito wa kipekee katika siasa za uchaguzi. Na hata katika Bunge la India, mazungumzo kuhusu mabadiliko ya hali ya hewa yamepuuzwa kwa kiasi kikubwa.

Soma pia:Dunia yashuhudia miezi 12 ya kwanza ya joto kuvuuka nyuzi 1.5C. 

Utafiti huo wa 2022 uligundua pia kuwa kati ya 1999 na 2019, ni asilimia 0.3 tu ya maswali yaliyoulizwa na wanasiasa yalihusiana na mabadiliko ya hali ya hewa.

Rajeev Gowda, mgombea kutoka chama cha Congress kinachowania mji wa Bengarulu ulioko kusini mwa India, ambao pia unakabiliwa na tatizo la maji, anasema hotuba zinazohusiana na mabadiliko ya hali ya hewa huwasogeza mbali na watu labda kama kuna suala tete. Akasema watu wengi huwa wanawakimbia wanapianza kuzungumzia mabadiliko ya hali ya hewa.