1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchaguzi wa India na Hofu za Jamii za Wachache

Oumilkheir Hamidou
17 Mei 2019

Maprofesa 6 wastaafu wa India wakiwa katika kikao chao cha kawaida cha usiku wanabishana kuhusu mkosi utakaowasibu watu wa jamii yao pindi Narendra Modi akichaguliwa kuendelea na muhula wa pili kama waziri mkuu wa India.

Indien Varanasi Modi Doppelgänger
Picha: DW/O. S. Janoti

 

"Tuko ukingoni mwa kugeuka raia wa tabaka ya pili," anasema Muhiuddin Azad alipohojiwa na shirika la habari la AFP mjini Azamgarh katika jimbo la Uttar Pradesh, mji wa kaskazini mwa India uliojipatia sifa kubwa kutokana na watunzi wake na wasomi wa Kiislam.

"Modi akipata muhula wa pili, tumekwisha" anaashiria profesa huyo wa zamani wa lugha ya Kiarabu katika wakati ambapo nchi hiyo kubwa ya kanda ya kusini mwa Asia yenye wapigakura milioni 900 inaitisha uchaguzi mkuu tangu katikati ya mwezi uliopita wa April hadi Jumapili hii. Zoezi la kuhesabu kura litaanza Mei 23.

Wafuasi wa chama cha wazalendo wa Kihindu cha Bharatiya Janata Party (BJP) cha Narendra Modi wanaojifakharisha kuwa wao ndio bora zaidi katika taifa hilo la mchanganyiko wa jamii tofauti, waliongoza katika uchaguzi wa mwaka 2014 na wanataraji kupata muhula wa pili wa miaka mitano kufuatia uchaguzi huo mkubwa kabisa uliowahi kuitishwa.

"Muhula wa kwanza lilikuwa jaribio kwa chama cha BJP. Mara tu watakaporejea madarakani watatekeleza mpango ulioandaliwa muda mrefu uliopita," anasema kwa upande wake Hassan Khalid Azmi, ambaye ni profesa wa zamani wa kemia.

India, yenye wakaazi bilioni 1.3 ambapo asilimia 80 kati yao ni Wahindu, ina jamii kubwa kabisa ya Waislamu - watu milioni 170 ikiwa idadi ya pili kwa ukubwa ulimwenguni.

Wafuasi wa itikadi kali za kihindu wakipakana zafarani huko Uttar PradeshPicha: picture-alliance/AP Photo/B. Armangue

Kitisho cha kufutwa ushahidi wote wa kiislam nchini India

Tangu Modi alipoingia madarakani miaka mitano iliyopita, jamii hiyo ya wachache wako mashakani. Miji kadhaa iliyokuwa na majina yanayotokana na urithi wa Kiislamu imebadilishwa majina, baadhi ya vitabu vya shule vimebadilishwa pia ili kufifisha mchango wa Waislamu katika historia ya nchi hiyo.

Kati ya Mei 2015 na Desemba 2018, watu 44, wengi wao ni Waislamu, wameuliwa kwa kisingizio cha kuwalinda ng'ombe-ambae wahindu wanamuabudu. Hayo ni kwa mujibu wa shirika la Human Rights Watch.

Waislamu wa India hawajawahi kuwa na kiu cha kuunda chama kwa msingi wa kidini, wakiamini vyama vilivyokuwepo vinawawakilisha pia. Lakini hali hiyo inaweza kubadilika.

"Tangu uhuru mwaka 1947 kutoka Uingereza, Waislamu hawajawahi kuwa na kiongozi," anaeleza Asaduddin Owaisi, mbunge mashuhuri kabisa wa Kiislamu na pekee anayekiwakilisha chama cha All India Majlis-e-Ittehadul Muslimeen.

Vyama vikuu vya kisiasa nchini India, anasema katika mahojiano na shirika la habari la AFP nyumbani kwake mjini New-Delhi, haviwaruhusu wasilam kuwa na usemi. Na hilo ni tukio linalotia wasi wasi kwa mustakbali wa demokrasia nchini India, anasema.

Rahul Gandhi,kiongozi wa chama kikuu cha upinzani cha CongressPicha: Ians

"Ufanisi wa demokrasia ya India umejengeka chini ya msingi wa demokrasia ya kushirikishwa na sio demokrasia ya walio wengi"

Bunge linalomaliza muhula wake lina wabunge 24 tu wa Kiislamu kutoka jumla ya viti 545 -idadi ndogo kabisa tangu nchi hiyo ilipojipatia uhuru wake kutoka kwa Muingereza.

BJP kimewaorodhesha wagombea saba tu wa Kiislamu - idadi ile ile kama mwaka 2014 na hakuna hata mmoja aliyeshinda. Chama kikuu cha upinzani, Congress cha Rahul Gandhi, kimewaorodhesha  wagombea 30 wa kiislam.

Kwa maoni ya Sarvar Ahmad, sheikh wa mji wa kakazini wa Azamgargh, mbinu za kuwatenga Waislamu zimekua zikifuatwa hatua baada ya hatua na serikali zote zilizoingia madarakani.

 

Mwandishi: Hamidou Oummilkheir/AFP

Mhariri: Mohammed Khelef

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW