Uchaguzi wa Israel: Benjamin Netanyahu awania muhula wa nne
17 Septemba 2019Watu nchini Israel wameanza kupiga kura katika uchaguzi utakaoamua iwapo Waziri Mkuu wa sasa Benjamin Netanyahu ataendelea kuwemo madarakani huku akiwa katika wasiwasi wa kufikishwa mahakamani kujibu tuhuma za kuhusika na ufisadi.
Waziri Mkuu huyo ambaye amekuwamo madarakani kwa muda mrefu zaidi kuliko mwengine yeyote anakabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa jenerali mstaafu Benny Gantz. Chama cha jenerali huyo mstaafu cha Buluu na Nyeupe kiko sambamba na chama cha Netanyahu cha Likud. Hata hivyo vyama hivyo vitalazimika kuunda mseto na vyama vidogo itakapobidi kuunda serikali. Leo asubuhi Rais wa Israel Reuven Rivlin alipiga kura katika mji wa Jerusalem na alisema kuwa leo ni israel inasherehekea demokrasia.
Waziri Mkuu Netanyahau amejaribu kujinadi kuwa yeye ni kiongozi mwenye sifa za kipekee za kuiongoza nchi katika nyakati za changamoto. Lakini mshindani wakejenerali mstaafu Benny Gantz anamzungumzia Netanyahu kuwa Waziri Mkuu anayeigawanya nchi na pia mwanasiasa anayeandamwa na kashfa. Gantz anajinadi kama mtu mtulivu na mwadilifu.
Gantz alipokwenda kupiga kura alisema waisraeli leo hii wanapiga kura ya mabadiliko. Kiongozi huyo wa chama cha Bluu na Nyeupe, amesema chama chake kitafanikiwa kuleta matumaini, bila rushwa na bila kuwepo misimamo mikali.
Netanyahu na jenerali huyo mstaafu leo wanapambana kwa mara ya pili mnamo mwaka huu baada ya kutoka sare katika uchaguzi uliofanyika mnamo mwezi wa Aprili. Hata hivyo Waziri Mkuu Netanyahu ameonyesha matumaini ya kuendelea kuwamo madarakani kutokana na kuungwa mkono na washirika wake wa jadi wa vyama vya mrengo mkali wa kiyahudi vinayvodhibiti viti vingi bungeni, lakini mshirika wake wa hapo awali ambaye sasa amekuwa hasimu wake Avigdor Lieberman alikataa kujiunga na serikali mpya ya mseto na hivyo kupungza viti vya serikali ya Netanyahu bungeni. Waziri mkuu huyo alilazimika kulivunja bunge na kuitisha uchaguzi mpya.
Uchunguzi wa maoni umebainisha kwamba matokeo ya uchaguzi wa leo yanatarajiwa kuwa kama ya hapo awali. Chama cha bwana Liebermann ndicho kinachotarajiwa kuwa muhimu kabisa katika hesabu za kuunda serikali. Baada ya kupiga kura bwana Lieberman alisisitiza ahadi ya kuwezeshwa kuundwa kwa serikali ya umoja baina ya chama cha Bluu na Nyeupe na chama cha Likud. Amesema haitafanyika duru ya tatu ya uchaguzi.
Katika uchaguzi wa leo mfungamano wa vyama vinavyowawakilisha waarabu wa Israel pia vinatarajiwa kuwa muhimu kama jinsi iliyvokuwa katika uchaguzi wa mwaka wa 2015 ambapo vilishika nafasi ya tatu kwa idadi ya viti bungeni. Na ikiwa utabiri utakuwa sahihi vyama hivyo vinaweza kuzima ndoto ya Waziri Mkuu Netanyahu ya kuchaguliwa kwa mara ya tano.
Vyanzo:/AP/DPA/AFP