1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchaguzi wa Jamhuri ya Afrika ya Kati wakabiliwa na vurugu

Zainab Aziz Mhariri: Rashid Chilumba
27 Desemba 2020

Wapiga kura nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati leo Jumapili wameshiriki kwenye uchaguzi wa rais na Bunge baada ya kipindi cha kampeni kukumbwa na vurugu kati ya waasi na vikosi vya serikali.

Zentralafrikanische Republik Bangui | Wahlen
Picha: ALEXIS HUGUET/AFP

Uchaguzi mkuu nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati unafanyika kwa mara ya kwanza tangu yalipofikiwa makubaliano ya amani yaliyotiwa saini kati ya serikali na makundi 14 ya waasi mnamo mwezi Februari mwaka 2019, ingawa mapigano bado yanaendelea nchini humo. Mashambulizi ya waasi yanatishia uthabiti wa mji mkuu, Bangui.

 Licha ya wito kutoka kwa wapinzani wa kuchelewesha zoezi hilo la kupiga kura kutokana na ukosefu wa usalama, Mahakama ya Katiba nchini humo ilikataa ombi la wapinzani la kuahirishwa uchaguzi. Rais Faustin-Archange Touadera anayewania muhula wa pili, amewahakikishia wagombea na wapiga kura kwamba zoezi hilo litafanyika kwa usalama na mara tu alipopiga kura yake alisema "Kupiga kura ni haki, ya wananchi wa Jamuhuri ya Afrika wa Kati". Amesema katiba inamruhusu kila raia kuchagua kwa uhuru viongozi anaowataka. Vituo vya kupigia kura vilifunguliwa mapema leo nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati kwa uchaguzi huo wa rais na Bunge.

Duru za habari zimesema kulikuwa na ucheleweshaji wa kama dakika 50 kabla ya vituo kufunguliwa katika mji mkuu, Bangui kutokana na vifaa vya kupigia kura kuchelewa kuwasilishwa kwa wakati.

Raia wa Jamuhuri ya Afrika ya Kati wakati wa kampeni za uchaguzi 2020Picha: Xinhua News Agency/picture alliance

Walinda amani wa Umoja wa Mataifa na wanajeshi wa Rwanda wameonekana wakishika doria kwenye mitaa ya mji mkuu huku magari ya kijeshi yenye silaha nzito yamewekwa nje ya vituo vya kupigia kura. Inakadikirwa ni sehemu ndogo pekee ya raia wa nchi hiyo ndiyo wataweza kupiga kura kwa kuwa theluthi mbili ya eneo la Jamhuri ya Afrika ya Kati liko chini ya udhibiti wa makundi ya wapiganaji kwa miaka minane iliyopita.

Rais wa zamani Francois Bozize, ambaye alitaka kushiriki kwenye kinyang'anyiro hicho lakini alizuiliwa na majaji kwa sababu anakabiliwa na vikwazo vya Umoja wa Mataifa, amewataka watu wasipige kura na badala yake waunge mkono muungano wa waasi.

Bozize alitoa ujumbe huo kwa njia ya sauti iliyochapishwa mitandaoni na ambao chama chake kilimeuthibitisha ujumbe huo kwa mujibu wa shirika la habari la AFP.

Rais wa Jamuhuri ya Afrika ya Kati Faustin Archange Touadéra anayegombea muhula wa piliPicha: Minusca

Muungano wa waasi mnamo siku ya Jumatano ulitangaza kuwa umekubali kusitisha mapigano kwa saa 72 kutoa nafasi ya zoezi la kupiga kura, lakini mnamo siku ya Ijumaa ukisema kuwa utaanza tena maandamano yake kwenye mji mkuu.

Siku ya Jumanne, mji wa nne kwa ukubwa nchini Jamuhuri ya Afrika ya Kati, Bambari, ulio kilomita 380 kaskazini mashariki mwa mji mkuu Bangui, ulishuhudia wingi wa watu waliojitokeza kwenye maandamano lakini vikosi vya usalama vikiungwa mkono na walinda amani wa Umoja wa Mataifa MINUSCA walifanikiwa kuidhibiti hali katika siku iliyofuata. 

Kulingana na rais wa kamati ya amani ya eneo hilo Jeannot Nguernendji, vituo vya kupigia kura katika mji huo wa Bambari havikufunguliwa mwendo wa asubuhi kwa sababu ya kuwepo majibizano ya risasi baina ya makundi yenye silaha.

Jamhuri ya Afrika ya Kati ni nchi yenye utajiri wa madini lakini inakabiliwa na umaskini mkubwa tangu ijipatie uhuru wake miaka 60 iliyopita. Maelfu ya watu wamekufa kutokana na vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyotokea mnamo mwaka 2013 na zaidi ya robo ya idadi ya jumla ya watu milioni 4.9 wamekimbia makazi yao. Kati ya hao, 675,000 ni wakimbizi katika nchi jirani na hawawezi kushiriki katika zoezi hilo la kupiga kura.

Vyanzo:/AFP/AP

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW