1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchaguzi wa Jimbo la Saarland mtihani kwa Merkel na Schulz

Caro Robi
26 Machi 2017

Wajerumani katika jimbo dogo la Saarland lililoko magharibi mwa Ujerumani wanapiga kura leo Jumapili katika uchaguzi wa majimbo ambao unaonekana kuwa kipimo cha umaarufu wa Kansela wa Ujerumani Angela Merkel.

Frankreich Angela Merkel und Martin Schulz in Verdun
Picha: Getty Images/S. Gallup

Uchaguzi wa jimbo la Saarland ndiyo wa kwanza kati ya chaguzi tatu za majimbo zitakazofanyika kabla ya uchaguzi wa huo wa Septemba 24.

Kwa maana hiyo unatoa fursa kwa vyama kujenga au kupoteza kasi katika jitihada zao za kuibuka mshindi katika ngazi ya kitaifa. Kwa sasa jimbo la Saarland linaongozwa na muungano wa chama cha kihafidhina cha Merkel CDU na chama cha msimamo wa wastani wa mrengo wa kulia Social Democrat SPD.

Matokeo ya maoni ya wanachi yaliyotolewa na kituo cha televisheni cha serikali ZDF yanaonyesha CDU ikiungwa mkono kwa asilimia 37 dhidi ya SPD inayoungwa mkono kwa asilimia 32. Chama cha di Linke kinachotarajiwa kuungana na SPD kina asilimia 12.5.

Saarland kipimo cha mambo yatakavyokuwa Septemba

Uchaguzi wa Saarland ndiyo mtihani wa kwanza kwa mgombea Ukansela wa chama cha SPD Martin Schulz ambaye amekipiga jeki chama hicho tangu kutangazwa kuwa mgombea wake dhidi ya Merkel. Schulz ameahidi kushughulikia suala la kukosekana kwa usawa, ambalo wapiga kura wengi wanalichukulia kwa uzito.

Ramani ya Jimbo la Saarland

Licha ya kuwa jimbo hilo la Saarland liliko mpakani na Ufaransa lina wakaazi takriban milioni moja, uchaguzi wake wa leo unachukulika kuwa muhimu sana katika kupima umaarufu wa Merkel dhidi ya Schulz.

SPD imejiongezea umaarufu kwa alama 10 kitaifa tangu Schulz kutangazwa mgombea mwezi Januari akiapa kuufikisha kikomo utawala wa Merkel wa miaka 12 madarakani. Ushawishi wa Schulz umewavutia hasa wapiga kura vijana katika nyanja ya kitaifa na katika jimbo la Saarland.

Merkel aliuambia mkutano wa hadhara alipokuwa akikifanyia chama chake kampeni katika mji wa Sankt Wendel ulioko mpakani kati ya Ujerumani, Ufaransa na Luxembourg kuwa kipindi hiki kila kura ina uzito mkubwa.

Kura za maoni zinabashiri muungano wa SPD, chama cha mrengo wa kushoto cha die Linke na chama cha wanamazingira wanaoegemea mrengo wa kushoto cha kijani au muungano wa SPD na Die Linke iwapo chama cha kijani kitashindwa kupata kura za kutosha katika uchaguzi huo.

Ni CDU au SPD?

Kura nyingine ya maoni iliyotolewa wiki iliyopita inaonyesha kuwa SPD na vyama vya kihafidhina CDU na CSU vinaungwa mkono kitaifa kwa asilimia 32. Lakini kura za maoni za Deutschlandtrend zinaonya asilimia 44 ya wapiga kura wanataka SPD kuongoza serikali ijayo ikilinganishwa na asilimia 33 ya wanaotaka chama cha Merkel kuongoza.

Mabango yanayoonesha wagombea wa SaarlandPicha: Getty Images/S. Gallup

Chini ya utawala wa Merkel Ujerumani imeshuhudia kuimarika kwa uchumi wake na idadi ya walioajiriwa ikiwa juu lakini pengo kati ya matajiri na masikini imezidi kuongezeka.

Schulz rais wa zamani wa bunge la Ulaya mwenye umri wa miaka 61 anajaribu kuwavutia wapiga kura walio katika tabaka la walioajiriwa, kupitia ujumbe wa matumaini wa kuwepo usawa na haki za kijamii.

Kura za maoni zinabashiri kinyang'anyiro kikali kati ya waziri mkuu wa sasa wa Saarland Annegret Kramp Karrenbauer mwenye umri wa miaka 54, mgombea wa CDU kwa jina la utani AKK, na naibu wake Anke Rehlinger mwenye umri wa miaka 40 mgombea wa chama cha SPD.

Vituo vya kupigia kura vinafunguliwa saa mbili asubuhi na matokeo ya awali yanatarajiwa kutangazwa na vyommbo vikuu vya habari vya Ujerumani baada ya vituo kufungwa saa kumi na mbili jioni.

Mwandishi: Caro Robi/Reuters/Afp

Mhariri: Yusra Buwahyid

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW