Uchaguzi wa katikati ya muhula wa utawala wa Marekani
5 Novemba 2018Rais wa Marekani Donald Trump na rais wa zamani Barrack Obama wamekuwa wakisisitiza hoja zao kwa wapiga kura katika muda wa majeruhi wa kampeni za uchaguzi wa katikati ya muhula nchini Marekani ambazo zinafikia ukingoni kabla ya kufanyika uchaguzi huo hapo kesho Jumanne. Trump ametoa wito kwa wapiga kura katika jimbo la Tennessee na Georgia na kuwahimiza wamuunge mkono mgombea wa chama cha Republican huku akiwaonya dhidi ya kumpigia kura mgombea wa chama cha Demokratik ambaye anasema chama chake kina mpango wa kuwaongezea mzigo wa kulipa kodi wananchi na kwamba kinashabikia uhamiaji haramu.
Trump ambaye mwenyewe hayumo katika kinyang'anyiro hicho kitakachoamua juu ya hatima ya wabunge na maseneta wa Republican anaendesha kampeni ya kuwapigia debe wajumbe wa chama chake cha Republican.
Kwa upande wake chama cha Demokratik kupitia rais wa zamani Barack Obama aliwahutubia wapiga kura katika majimbo ya Indiana, na baadaye Chicago. Obama amewasihi wanaokiunga mkono chama cha Democrats kuwa wasidanganyike na uongo na hofu wanazowekewa.
Pana ishara zinazoenyesha kwamba huenda wagombea wa chama cha Demokratik wakafanikiwa kulichukua tawi mojawapo la bunge-baraza la seneti au baraza la wawakilishi. Hata hivyo miaka 2 baada ya kuifanyika uchaguzi uliothibitisha kwamba uchunguzi wa maoni pamoja na utabiri wa matokeo ya uchaguzi, ni mambo yanayoweza kwenda mrama, hakuna linaloweza kusemwa kwa uhakika kabla ya uchaguzi wa hapo kesho nchini Marekani ambao ni wa kwanza kufanyika katika nchi nzima tangu DonaldTrump aingie madarakani.
Baada ya vituo vya kwanza vya kupigia kura kufungwa katika eneo la mashariki mwa Marekani, zoezi la kuhesabu kura litaanza mara moja na hapo dalili zitaanza kuonekana ni wapi waliposimama wamarekani katika mwaka huu wa 2018 juu ya masuala ya uhamiaji, huduma za afya, usawa wa kijinsia hasa katika katika zama hizi za kampeni inayojulikana kama #MeToo - , wakati wakipigania kuwachagua wanaowataka kuwawakilisha katika mabaraza mawili ya bunge la Marekani Congress- Baraza la wawakilishi na lile na Seneti. Wachambuzi wanasema wapiga kura wanatayamiwa kujitokeza kwa idadi kubwa kabisa katika uchaguzi huu wa katikati ya muhula wa utawala .
Mwandishi: Zainab Aziz/APE/AFPE
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman