Lebanon yamchagua rais katikati mwa mizozo ya kikanda
8 Januari 2025Miongoni mwa wagombea ni pamoja na kamanda Jenerali Joseph Aoun, ambaye kulingana na wanasiasa wa Lebanon, anaungwa mkono pakubwa na Marekani. Mwengine ni Jihad Azour, afisa wa ngazi ya juu wa Shirika la Fedha Duniani IMF, na ambaye awali alihudumu kama waziri wa fedha nchini Lebanon. Meja Jenerali Elias al-Baysari, ambaye ni mkuu wa shirika la Usalama Lebanon pia yumo mbioni kuwania urais.
Kura hiyo ni mtihani wa kwanza wa nguvu ya kisiasa kwa Lebanon tangu, kundi la Kishia la wanamgambo wa Hezbollah kushindwa vibaya kwenye vita kati yake na Israel. Kundi hilo linaloungwa mkono na Iran ndilo awali lilimsaidia Michel Aoun kuchukua urais mwaka 2016.
Uchaguzi huo unafanyika wakati kuna mabadiliko ya kihistoria katika Mashariki ya Kati, ambapo serikali ya Syria iliyoongozwa na familia ya Assad na ambayo kwa miongo mingi ilikuwa na ushawishi mkubwa dhidi ya Lebanon iliangushwa
Kiti hicho cha urais ambacho kimehifadhiwa kukabidhiwa Mkristo wa madhebu ya Maronite nchini humo kufuatia mfumo wao wa kugawana madaraka kati ya makundi ya kidini nchini humo, kimekuwa wazi tangu muhula wa rais wa zamani Michel Aoun ulipokamilika mnamo Oktoba 2023.Israel yafanya mashambulizi makubwa nchini Lebanon
Hakuna kundi lolote la kisiasa lenye idadi ya kutosha ya wajumbe kumchagua wamtakaye katika bunge la nchi hiyo lenye jumla ya viti 128. Hadi sasa makundi hayo hayajafikia makubaliano yoyote kuhusu mgombea yeyote.
Kufuatia mabadiliko yanayokumba kanda hiyo, makundi yanayoshirikiana Hezbollah na vuguvugu la Amal linaloongozwa na spika wa bunge hilo Nabin Berri, wameacha kumuunga mkono Suleiman Frangieh ambaye wamekuwa wakimuunga mkono kwa miaka miwili sasa. Badala yake wamesema wako tayari kumuunga mkono mgombea asiyesababisha mgawanyiko. Hayo ni kulingana na vyanzo vitatu.
Kulingana na taarifa ya Waziri Mkuu wa mpito Najib Mikati, anahisi kuwa na furaha kwa sababu nchi hiyo itampata rais mpya leo. Mshindi ni lazima apate kura 85 katika duru ya kwanza na 65 katika duru ya pili.
Soma: Umoja wa Mataifa wataka dola milioni 371.4 kwa Lebanon
Hata hivyo kulingana na vyanzo viwili vya habari na wachambuzi, haiko wazi kama kuna mgombea yeyote atachaguliwa.
Nabil Boumonsef, naibu mhariri mkuu wa jarida la kila siku la Annahar, amesema hadi sasa si wazi kwamba kuna mgombea anayeweza kushinda moja kwa moja, licha ya mabadiliko makubwa ya kisiasa ambayo yameshuhudiwa Lebanon, hasa kuzingatia kwamba Kundi lenye silaha la Hezbollah limekuwa chanzo kikubwa cha mgawanyiko.
Akielezea ushawishi ambao Hezbollah ingali nao, Amal amesema njia pekee ambapo rais anaweza kuchaguliwa ni ikiwa watakubaliana kumuunga mkono Aoun au Azour.
Soma pia: Maelfu ya Walebanon warejea nyumbani baada ya kusitishwa kwa vita
Kwa kuzingatia masilahi ya nchi za magharibi na kanda hiyo kwenye uchaguzi huo, mabalozi wa Ufaransa na Saudi Arabia walikutana na wanasiasa mjini Beirut siku ya Jumatano. Hayo ni kulingana na duru kutoka kwa wanasiasa wanne wa Lebanon waliokutana na balozi wa Saudia Yazid bin Farhan, wamesema balozi huyo aliashiria nchi yake kumuunga mkono Aoun.
Wakati mmoja, Saudi Arabia ilikuwa mshirika mkubwa nchini Lebanon, ikishindana na Tehran kwa ushawishi, lakini ushawishi wake ulififia na kupitwa na Iran na kundi la Hezbollah.