1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Joe akubali kung'atuka

21 Julai 2024

Baada ya wiki kadhaa za uvumi, Rais wa Marekani Joe Biden amethibitisha kuwa hatogombea tena katika uchaguzi wa rais wa mwezi Novemba dhidi ya Donald Trump, baada ya shinikizo kuzidi ndani ya chama chake cha Democratic.

Joe Biden
Picha: Susan Walsh/AP/dpa/picture alliance

Rais wa Marekani Joe Biden ametangaza Jumapili kuwa anakaa kando kutoka kwenye kinyang'anyiro cha urais wa Marekani 2024. "Imekuwa heshima kubwa maishani mwangu kuhudumu kama rais wenu," alisema kwenye chapisho la mtandaoni.

"Na ingawa imekuwa nia yangu ya kutaka kuchaguliwa tena, naamini ni kwa manufaa ya chama changu na nchi yangu mimi kukaa pembeni."

Soma pia: Biden akataa kujitowa kinyang'anyiro cha urais Marekani

Rais huyo mwenye umri wa miaka 81 amekuwa akikabiliwa na wito wa kusitisha kampeni tangu mdahalo dhidi ya Donald Trump wiki tatu zilizopita, ambapo alionekana kuwa dhaifu, akipambana kueleweka. 

Kabla ya taarifa ya Jumapili, hata hivyo, Biden alijaribu kuonyesha ukaidi na kutupilia mbali miito hiyo.

Rais Joe Biden amekuwa akishinikizwa na chama chake kujiondoa kwenye uchaguzi kufuatia wasiwasi kuhusu uwezo wake wa kiakili na kiafya.Picha: Susan Walsh/AP Photo/picture alliance

Wakati akithibitisha kuwa hatashindana na Trump katika uchaguzi wa Novemba, Biden ameashiria kuwa atasalia kama rais hadi mwisho wa muhula wake.

Biden amuunga mkono Kamala Harris

Baada ya kuthibitisha kuwa anajiondoa katika kinyang'anyiro cha urais, Biden alimuidhinisha Makamu wa Rais Kamala Harris kuchukua nafasi yake. Alisema kumchagua Harris kama makamu wa rais ulikuwa "uamuzi bora zaidi ambao nimefanya"

"Leo nataka kumuunga mkono kikamilifu na kumuidhinisha Kamala kuwa mteule wa chama chetu mwaka huu. Wanademokratii - ni wakati wa kuja pamoja na kumshinda Trump," aliandika Biden. "Hebu tufanye hivi."

Harris mwenye umri wa miaka 59 alijitosa katika siasa baada ya kupanda vyeo na kuwa mwendesha mashtaka mkuu wa California. Wakati wake katika Ikulu ya White House, hata hivyo, hakufanya mengi kuinua wasifu wake wa umma.

Biden ametangaza kumuunga mkono kikamilifu Kamala Harris kuwa mteule wa chama cha Democratic.Picha: Tierney L. Cross/newscon/picture alliance

Alionekana kuwa katika kivuli cha Biden na kushambuliwa na chama cha Republican kuhusiana na juhudi zake za kuzuia mmiminiko wa wahamiaji wanaowasili kutoka Mexico.

Soma pia: Shinikizo la kumtaka Biden kutowania muhula wa pili laongezeka

Harris, hata hivyo, ana faida zaidi ya wagombeaji wengine wanaowezekana kwa sababu ya uwezo wake wa kuzitumia fedha za kampeni ambazo tayari amechangisha na Biden.

Kampeni hiyo hivi karibuni iliripoti kuwa na kiasi cha dola milioni 91 fedha zake yenyewe, huku kamati za kampeni za washirika zikifanya kiwango jumla kuwa zaidi ya dola milioni 240. Pesa hizo zinaweza kuwa muhimu katika mbio dhidi ya kampeni ya Trump-Vance.

Schummer: Biden ametanguliza maslahi ya nchi, chama na mustakabali

Kiongozi wa Wengi katika Baraza la Seneti Chuck Schumer ametoa pongezi kwa Rais wa Marekani Joe Biden baada ya uamuzi wake wa kutowania muhula wa pili katika uchaguzi wa rais wa Novemba.

"Joe Biden amekuwa sio tu rais mzuri na kiongozi mzuri wa sheria, lakini ni binadamu wa ajabu sana," Schumer alisema katika taarifa yake.

Soma pia: Biden asema hang'oki licha ya makosa ya aibu

Mdemokrati huyo alisema uamuzi wa Biden "haukuwa rahisi, lakini aliweka tena nchi yake, chama chake, na mustakabali wetu mbele. Joe, leo inaonyesha wewe ni mzalendo wa kweli na Mmarekani halisi."

Pamoja na wabunge wengine kadhaa wa Democratic, mapema wiki hii, Schumer alimwambia Biden kwa faragha kuwa itakuwa bora kwa nchi na Chama cha Democratic ikiwa atahitimisha kampeni yake ya kuchaguliwa tena.

Kiongozi wa wengi katika Baraza la Seneti Chuck Schumer amemsifu Biden kwa kuchukua maamuzi magumu.Picha: Annabelle Gordon/CNP/abaca/picture alliance

Trump: 'Biden hakufaa kugombea'

Rais wa Marekani Joe Biden "hakuoaswa kugombea" muhula wa pili, mpinzani wake wa chama cha Republican Donald Trump aliandika kwenye mtandao wa kijamii.

Trump alitoa maoni hayo muda mfupi baada ya Biden kusema kuwa anajiondoa katika kinyang'anyiro cha kuwa rais ajaye wa Marekani na kumuidhinisha Makamu wa Rais Kamala Harris kuwa mgombea wa Democrat.

Soma pia:Biden aboronga wakati Trump akitoa uongo mdahalo wa urais 

Mrepublican huyo alikwenda mbali zaidi, akihoji uwezo wa Biden kusalia kwa muda uliobakia wa muhula wake.

"Joe Biden mpotovu hakufaa kugombea Urais, na kwa hakika hafai kuhudumu na hakuwahi kamwe! ... Tutateseka sana kwa sababu ya urais wake, lakini tutarekebisha uharibifu ambao amefanya haraka sana," Trump aliandika. kwenye mtandao wake wa kijamii wa Truth Social.

Trump akubali kuwa mgombea wa Republican 2024

02:32

This browser does not support the video element.

Trump pia alifanya mahojiano na CNN, na kuliambia shirika hilo la utangazaji la Marekani kwamba anadhani ni rahisi zaidi kumshinda Makamu wa Rais Kamala Harris kuliko ambavyo ingekuwa kumshinda Biden.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW