1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchaguzi wa mitaa Tanzania wanukia

16 Agosti 2024

Uchaguzi wa serikali za mitaa nchini Tanzania unakaribia kufanyika karibuni huku vyama vya upinzani katika taifa hilo, vikijipanga kwenda mahakamani kuishitaki serikali kwa kukiuka sheria.

Afrika Tansania Dar es Salaam Wahlen
Picha: Emmanuel Herman/REUTERS

Wanaituhumu serikali kuruhusu uchaguzi huo kusimamiwa na wizara ya tawala za mikoa na serikali za mitaa badala ya tume ya uchaguzi. Hata hivyo wamesisitiza hawataususia na kwamba wapo tayari kuingia ulingoni wakitegemea nguvu ya umma.

Vyama vya upinzani nchini Tanzani vimejinasibu kuwa vitashiriki kikamilifu uchaguzi wa serikali za mitaa licha ya madai yao mengi ya kutozingatiwa kwa sheria huku wakijipanga kupinga mahakamani, kanuni mpya za uchaguzi huo  zilizopitishwa 2024 kwa madai kuwa zinapingana na sheria mpya ya uchaguzi.

Mahakamani kupinga kanuni za uchaguzi

Jana, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa,(TAMISEMI) alitoa tangazo la kufanyika kwa uchaguzi huo, mnamo Novemba 27, na taarifa hiyo ikaeleza kuwa kampeni zitaanza Novemba 20 hadi 26.

Raia akishiriki zoezi la upigaji kura TanzaniaPicha: Ericky Boniphace/DW

DW imezungumza na Katibu Mkuu wa Chadema, John John Mnyika, ambaye amesema, chama hicho kitashiriki lakini wanakwenda mahakamani kupinga baadhi ya kanuni za uchaguzi.

Miongoni mwa  mabadiliko makubwa katika kanuni za mwaka 2024 za uchaguzi wa serikali za mitaa ni kuondolewa kwa kifungu cha kupita bila kupingwa, ambacho awali wapinzani walikilalamikia.

Katika uchaguzi wa 2019, viongozi wengi wa CCM walipita bila kupingwa baada ya vyama vya upinzani, ikiwamo CHADEMA, CUF, NLD, NCCR na ACT Wazalendo, kususia uchaguzi huo.

Hata hivyo kwa mujibu wa CHADEMA, wanapinga sheria inayoruhusu TAMISEMI iendelee kusimamia uchaguzi huo, ilhali sheria mpya ya tume ya uchaguzi kifungu cha 10(1) imesema TUME ya uchaguzi ndiyo itakayosimamia uchaguzi huo.

TAMISEMI haifai kusimamia uchaguzi

Kwa upande wao, ACT Wazalendo kama ilivyo kwa Chadema, wanasema  wanatarajia Kwenda mahakamani kuishtaki TAMISEMI kwa kuwa haipaswi kusimamia uchaguzi huu na ni kinyume cha sheria mpya ya uchaguzi. Esther Thomas ni  Naibu Katibu wa Oganaizesheni, Mafunzo na Uchaguzi wa ACT Wazalendo.

Jaji Jacobs Mwambegele mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi TanzaniaPicha: Courtesy of Independent National Electoral Commission of Tanzania

Kwa mujibu wa tangazo la uchaguzi huo, upigaji wa kura utaanza saa 12:00 asubuhi na kumalizika saa 10:00 jioni na nafasi zitakazogombewa ni mwenyekiti wa kijiji au mtaa , wajumbe wa halmashauri ya kijiji, wajumbe wa halmashauri ya kijiji na wenyeviti wa vitongoji katika mamlaka za wilaya.

Kadhalika, uteuzi wa waandikishaji na waandaaji orodha ya wapigakura kwa mujibu wa kanuni hizo, utafanywa na msimamizi wa uchaguzi atakayeteua watumishi wa umma watakaoandikisha na kuandaa orodha ya wapigakura siku 52 kabla ya siku ya uchaguzi.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW