Uchaguzi wa Nigeria waingia dosari
16 Aprili 2007Magazeti ya Nigeria yanakadiria kwamba watu 50 wameuwawa katika ghasia zinazohusishwa na udanganyifu katika uchaguzi wa hapo Jumamosi wa mgavana wa majimbo 36 ambao unapaswa kuipa Wanigeria kidokezo nini cha kutarajia katika uchaguzi wa rais uliopangwa kufanyika hapo tarehe 26 mwezi wa April.
Chama tawala cha PDP kimeshikilia majimbo 11 kati ya 14 wakati matokeo yalipotangazwa na tume ya uchaguzi.Vyama vya upinzani vimejishindia majimbo matatu ukiwemo mji mkubwa kabisa nchini Nigeria wa Lagos ambao tayari ulikuwa ngome kuu ya wapinzani.
Msemaji wa chama cha upinzani cha Action Congress Lai Mohamed amekaririwa akisema chama tawala kimejizawadia karibu kila jimbo.
Katika jimbo la kusini lenye kuzalisha mafuta la Delta ambapo chama cha PDP kilitangazwa kuwa mshindi vijana wakiwa na mapanga na bunduki wameziunguza nyumba na kuzifunga barabara katika mji wa Wariri wakati mamia ya wanawake na watoto wakiukimbia mji huo wakiwa wamepakiwa kwenye pikipiki.
Viongozi wa jamii wanasema kulikuwa hakuna upigaji kura karibu katika jimbo hilo zima ambapo kampeni za uchaguzi zilichochea mfarakano wa kikabila.
Mashambulizi kadhaa ya wanamgambo katika vituo vya mafuta katika jimbo la Delta mwaka jana yaliwalazimisha maelfu ya wafanyakazi wa kigeni kukimbia na kupunguza uzalishaji wa mafuta wa nchi mwanachama wa nchi zinazozalisha mafuta kwa wingi duniani OPEC kwa asilimia tano.
Demokrasia ilirudi tena katika taifa hilo lenye idadi kubwa kabisa ya watu barani Afrika hapo mwaka 1999 baada ya miongo mitatu ya takriban utawala wa kijeshi mfululizo na chaguzi hizi zinapaswa kupelekea kukabidhiana madaraka kwa utawala wa kwanza wa kiraia kwa utawala mwengine wa kiraia tokea uhuru wa nchi hiyo hapo mwaka 1960.
Rais Olesegun Obasanjo lazima an’gatuke mwezi ujao baada ya kutumikia vipindi viwili vya miaka minne minne katika mdaraka.
Chama cha PDP kilishinda majimbo 28 kati ya 36 katika uchaguzi wa mara ya mwisho hapo mwaka 2003 na kuna kama majimbo manane ambapo udhibiti wake unatishiwa.
Kwa mujibu wa mashahidi uchaguzi wa Jumamosi ulivurugwa kutokana pamoja na dosari nyengine kuchelewa kuwasili au kutokuwasili kabisa kwa makaratasi ya kupigia kura, kuibiwa kwa masanduku ya kura, kutekwa nyara kwa maafisa wa uchaguzi,vitisho kwa wapiga kura,nyaraka bandia za matokeo, makosa katika daftari la kupiga,kura zenye makosa na wapiga kura wenye umri mdogo wasiostahiki kupiga kura.
Rais wa senate wa bunge la Nigeria Ken Nnamani anasema iwapo watu wanajilazimisha kwa wapiga kura kunakuwa hakuna tafauti na utawala wa kijeshi amesema hayo akiwa kwenye jimbo lake la Enugu ambapo pia amesema kwamba karibu kulikuwa hakuna kabisa upigaji kura.
Makundi ya upinzani katika mjimbo kadhaa yanasema udangayifu ulikuwa kila mahala kiasi cha kufanya kuhitajike uchaguzi mpya.
Vijana wameziwekea vizuizi ofisi za uchaguzi katika majimbo mawili Ondo na Bauchi ambapo serikali ya jimbo ya PDP inakabiliwa na upinzani mkali.Kulikuwa na maandamano ya upinzani katika jimbo la kusini mafgharibi la Osun ambapo PDP imetangazwa kuwa mshindi.
Madarzeni ya watu wameuwawa katika ghasia za kisiasa miezi kadhaa kabla ya uchaguzi wanadiplomasia wanasema kuaminika kwa zoezi hilo tayari kunatiliwa mashaka kwa sababu madarzeni ya wagombea wa upinzani wamepigwa marufuku kugombania kwa kushtakiwa kwa madai ya udanganyifu.