1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaGabon

Uchaguzi wa rais Gabon: Bongo kuchuana na wagombea 18

29 Julai 2023

Kiongozi wa Gabon Ali Bongo Ondimba, anayewania muhula wa tatu, atachuana na wagombea 18 katika uchaguzi wa rais utakaofanyika mwezi ujao. Familia ya Bongo imetawala taifa hilo la Afrika Magharibi kwa miaka 55.

Gabun Ali Bongo
Picha: Julien de Rosa/AFP

Ali Bongo mwenye umri wa miaka 64 na ambaye alichukua nafasi ya baba yake Omar Bongo Ondimba mwaka 2009, alitangaza rasmi mwezi Julai kuwa atawania tena urais wa nchi hiyo. Tume ya Uchaguzi ya Gabon iliidhinisha maombi 19 kati ya 27 ya wagombea, ikiwa ni ongezeko la wagombea watano ukilinganisha na mwaka 2016.

Wapinzani wakuu wa Bongo katika nafasi hiyo ya juu ni pamoja na Alexandre Barro Chambrier wa chama cha upinzani cha Rally for Fatherland and Modernity (RPM) pamoja na mkuu wa Umoja wa Kitaifa Paulette Missambo.

Upinzani hata hivyo ulishindwa kuafikiana kuhusu mgombea mmoja atakayepambana na Bongo katika uchaguzi wa Agosti 26, lakini wagombea wote wawili ni mawaziri wa zamani na wamejumuika katika muungano unaotaka mabadiliko wa "Alternance 2023".

Rais wa Gabon Ali Bongo akihutubia mjini London kwenye sherehe za Jumuiya ya Madola (17.10.2023)Picha: ISABEL INFANTES/AFP

Eddy Minang, mwendesha mashtaka wa umma ameliambia shirika la habari la AFP kwamba, siku ya Jumapili, mkutano wa chama cha Chambrier katika mji wa mashariki wa Franceville ulivamiwa na "kundi la watu wasiojulikana" ambalo liliwashambulia wanaharakati na kuwasababishia majeraha kadhaa.

Katika taarifa iliyotolewa Jumatatu (24.07.2023), chama cha RPM kiliwataja washambuliaji kuwa "wazusha ghasia wanaoungwa mkono na serikali".

Soma pia: Rais wa Gabon Ali Bongo kugombea tena urais

Mwezi Aprili, Bunge la Gabon lilipiga kura kurekebisha katiba na kupunguza muhula wa rais kutoka miaka saba hadi mitano. Vyama vya upinzani vimekosoa mabadiliko hayo, hasa kipengele cha kumalizika kwa duru ya pili ya upigaji kura ambavyo wanahisi ni kama mbinu ya kumwezesha Bongo kuchaguliwa tena.     

Huku zikiwa zimesalia takriban wiki tano kabla ya uchaguzi kufanyika, muungano wa upinzani wa "Alternance 2023" umekosoa marekebisho ya kanuni za uchaguzi, ikiwa ni pamoja na hatua ya kuruhusu waangalizi wasiozidi watatu pekee katika kila kituo cha kupigia kura.

Soma pia: Rais Ali Bongo apelekwa Morocco kwa matibabu

Mwangalizi mmoja kutoka chama tawala, mmoja wa upinzani na mwengine wa wagombea huru. Wakati hapo awali kila mgombea angeliweza kumteua mwangalizi katika kila kituo cha kupigia kura.

Francois Ndong Obiang, mkuu wa chama cha Reagir, aliumbia mkutano wa vyama wa Alternance siku ya Ijumaa kwamba madai ya usawa kati ya chama tawala na upinzani ni udanganyifu wa kisiasa. Hali hiyo inavinufaisha vyama vya upinzani vinavyodhaniwa kuwa na wagombea wachache mno au visivyo na wagombea kabisa.

Mji mkuu wa Gabon LibrevillePicha: Massassa B. Claude/AP/picture alliance

Wiki iliyopita, Waziri Mkuu Alain-Claude Bilie-By-Nze aliandika ujumbe kwenye ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twiter akiwaambia wapinzani kuwa ili kufanya uchaguzi katika mazingira bora, ni lazima wadau wote wawe waangalifu na kutochochea hali ya mvutano.      

Chama chenye nguvu cha Ali Bongo cha Gabon Democratic Party (PDG) kinashikilia viti vingi katika mabunge yote mawili. Hata hivyo Bongo alishinda uchaguzi wa mwaka 2016 kwa kura chache tu 5,500 zaidi ya mpinzani wake Jean Ping ambaye alidai kulikuwepo udanganyifu katika uchaguzi huo.

Soma pia: Wanajeshi wajaribu kuchukuwa madaraka Gabon, serikali yasema bado ipo

Kauli hiyo ya Ping ilizusha ghasia katika mji mkuu Libreville na kusababisha vifo vya watu watano, kwa mujibu wa serikali. Lakini upinzani ulisema kuwa watu 30 waliuawa kwa kupigwa risasi na vikosi vya usalama.

Bongo alipatwa na kiharusi mwaka 2018 na kuwa nje ya uwanja wa kisiasa kwa miezi kadhaa na hivyo kupelekea wapinzani kuhoji na kutilia mashaka iwapo anafaa kuliongoza taifa hilo.

Mji wa Libreville, Gabon

03:35

This browser does not support the video element.

Hadi sasa bado ana matatizo ya mkono na mguu na huwa na shida ya kutembea lakini katika miezi ya hivi karibuni amefanya mikutano kadhaa kote nchini na kufanya ziara rasmi nje ya nchi, ikiwa ni pamoja na kuhudhuria mikutano ya kilele.     

Uchaguzi wa rais utaambatana na uchaguzi wa Bunge na ule wa wakuu wa mikoa na viongozi wa serikali za mitaa.

Gabon ni mojawapo ya nchi tajiri zaidi barani Afrika kutokana na kutegemea mapato yake ya mafuta na idadi ndogo ya watu milioni 2.3. Lakini kulingana na Benki ya Dunia, theluthi moja ya watu nchini humo bado wanaishi katika umaskini mkubwa.

(AFPE)

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW