1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchaguzi wa rais nchini Cameroon wakabiliwa na vurugu

7 Oktoba 2018

Ghasia zimezuka katika sehemu za Cameroon zinazotumia lugha ya kiingereza mara baada ya uchaguzi wa rais kuanza nchini humo. Kwa mujibu wa mbunge mmoja katika mji wa Bamenda, watu wawili wameuawa kwa kupigwa risasi.

Kamerun Präsidentschaftswahlen l Anhänger der MRC
Picha: Getty Images/AFP/M. Longari

Waandishi wa habari hata hivyo wamearifu kwamba kwenye majimbo ya nchi hiyo ya Afrika ya kati yanayotumia lugha ya Kifaransa zoezi la uchaguzi limeendelea bila ya mushkeli wowote. Rais Paul Biya anawania muhula wa saba huku nchi yake ikiwa inakumbwa na vurugu katika mikoa inayotumia lugha ya Kiingereza. Biya amekuwa madarakani tokea mwaka 1982 na ameahidi kuumaliza mgogoro ambao umesababisha vifo vya watu zaidi ya 400 Kusini-magharibi na Kaskazini-magharibi mwa nchi hiyo.

Upinzani uliogawanyika umeshindwa kusimamisha mgombea mwenye nguvu ya kuweza kuchuana na Biya mwenye umri wa miaka 85 na mmoja wa watawala wa muda mrefu zaidi barani Afrika. Hayo ni kwa sababu wapinzani wawili wakuu nchini Cameroon waliounda muungano wa kwanza wa vyama vya upinzani mnamo 1992, walishindwa kufikia makubaliano na vyama vingine vya upinzani ili kuunda ushirikiano wenye nguvu dhidi ya rais Biya.

Rais wa Cameroon Paul BiyaPicha: picture-alliance/AP Photo/L. Zhang

Rais Biya na mke wake Chantal, walipiga kura zao kwenye shule ya umma ya Bastos iliyo katika mji mkuu wa Yaounde chini ya ulinzi mkali. Kiongozi wa chama kikuu cha upinzani cha Democratic Front Joshua Osih alipiga kura katika mji wa Douala na ametoa mwito wa kuzingatiwa uwazi katika zoezi la kuhesabu kura.

Raia wa Cameroon wapatao milioni 6.5 wameshiriki katika uchaguzi huo huku Rais Paul Biya akitarajiwa kushinda awamu nyingine ya uongozi katika uchaguzi huo wa rais. Ushindi wa Biya hata hivyo hautakuwa na mamlaka yenye nguvu kwavile wananchi wengi wameyahama makazi yao katika eneo linalozungumza Kiingereza ambalo limekumbwa na ghasia.

Wakati huo huo upande unaotaka kujitenga umetishia kufanya fujo vurugu. Zaidi ya watu 200,000 wameyahama makazi yao kutokana na vurugu zinazofanywa na upande unaotaka kujitenga pamoja na wanajeshi katika maeneo hayo. Kulingana na jopo la kimataifa linaloshughulikia migogoro (ICG), takriban raia 420, askari 175 wa vikosi vya usalama na idadi isiyojulikana ya watu wanaotaka kujitenga wameuwawa katika vurugu hizo.

Wafuasi wa mgombea wa upinzani nchini CameroonPicha: Getty Images/AFP/Seyllou

Mara tu baada ya shughuli za kupiga kura kuanza, vikosi vya usalama viliwaua kwa kuwapiga risasi  watuhumiwa watatu wanaodaiwa kuwa ni watu kutoka kwenye kundi la wanaotaka kujitenga ambao walikuwa kwenye pikipiki. Watu hao waliwafyatulia risasi wapita njia katika mji wa Bamenda, kaskazini magharibi.

Wakati huo huo katika mji mkuu wa kusini-magharibi Buea, wapiganaji watatu wa kundi linalo taka kujitenga la Ambazonia  Republic walipigwa risasi na kuuawa mnamo siku ya Ijumaa. Kwa mujibu wa mashahidi kasisi mmoja pia liuawa na askari siku ya Alhamisi.

Maeneo ya kaskazini ya mbali yamekumbwa na ukosefu wa usalama, kutokana na mashambulio ya wapiganaji wa Boko Haram wa nchini Nigeria  licha ya jitihada za Marekani za kuwapa silaha wanajeshi wa Cameroon pamoja na kuwapa mafunzo na mafunzo jinsi ya kupambana na wapiganaji hao wa jihadi.

Waangalizi wa uchaguzi, ikiwa ni pamoja na wa kutoka Umoja wa Afrika, wamesema hawatafanya kazi yao katika maeneo ya kusini magharibi na kaskazini magharibi kutokana na maeneo hayo kukumbwa na migogoro.

Mwandishi: Zainab Aziz/APE/AFPE

Mhariri: Yusra Buwayhid

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW