Uchaguzi wa rais nchini Guinea
7 Novemba 2010Matangazo
Raia nchini Guinea wameombwa kubakia shwari watakapopiga kura hii leo katika duru ya pili ya uchaguzi wa rais ulioahirishwa mara kadhaa. Hii ni mara ya kwanza kwa raia nchini Guinea kumchagua rais wa kiraia katika uchaguzi wa kidemokrasia wa kwanza baada ya zaidi ya miaka 50.
Duru hiyo ya pili ya uchaguzi inawapambanisha wagombea wanatoka katika makabila mawili makubwa nchini humo na hiyo imezusha ghasia na hali ya kutoaminiana. Hata hivyo Cellou Dalein Diallo na Alpha Conde walijitokeza pamoja na kutoa mwito wa utulivu katika taifa hilo la Afrika Magharibi. Kumekuwepo na uhasama katika pande zote mbili tangu kufanyika kwa duru ya kwanza ya uchaguzi Juni 27 ambapo hakuna aliejitokeza mshindi.