1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchaguzi wa rais nchini Libya uko mashakani

22 Desemba 2021

Tume ya uchaguzi nchini Libya imeagiza kuvunjwa kwa kamati za uchaguzi nchini humo na kutilia mashaka uwezekano wa kuandaliwa kwa uchaguzi wa rais uliopangwa kufanyika mnamo Disemba 24.

Libyen | Protest gegen Präsidentschftskandidat Saif al-Islam al-Gaddafi
Picha: Hamza Alahmar/AA/picture alliance

Ijumaa ya Disemba 24, ndio siku ambayo huenda ingekuwa muhimu kwa Walibya kwani kwa mara ya kwanza wangepata nafasi ya kuchagua Rais wao. Hata hivyo, kuvunjwa kwa kamati hizo za uchaguzi moja kwa moja kunamaanisha kuwa uwezekano wa kufanyika kwa uchaguzi ni mdogo mno.

Muda mfupi baada ya tangazo la tume hiyo ya uchaguzi, Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Libya UNSMIL ulitoa taarifa na kuonyesha wasiwasi wake juu ya hali ya usalama katika mji mkuu Tripoli.

Soma pia: Makundi yenye silaha yashika doria Tripoli

Ujumbe huo wa Umoja wa Mataifa nchini Libya umesema kujihami kwa baadhi ya makundi kunatishia kuleta mvutano na kusababisha uwezekano wa kuzuka upya kwa mapigano. Ujumbe huo umeongeza kuwa, mizozo ya kisiasa inapaswa kutatuliwa kwa njia ya mazungumzo.

Picha zilizochapishwa mitandaoni zimeonyesha vifaru na malori ya kijeshi katika wilaya ya Fornaj huku watu waliojihami kwa silaha wakishika doria katika baadhi ya barabara. Wakaazi wamesema shule na vyuo vikuu mjini Tripoli vimefungwa kama tahadhari.

Kujihami kwa makundi hayo kunatokea wakati Walibya wenyewe wakisuburi tangazo rasmi la kuahirishwa kwa uchaguzi huo uliopangwa kufanyika Ijumaa wiki hii.

Uchaguzi huo ulikusudia kuhitimisha mpango wa amani unaoongozwa na Umoja wa Mataifa uliolenga kurejesha utulivu na kuiingiza madarakani serikali iliyochaguliwa kidemokrasia na kumaliza mzozo wa muongo mmoja.

Wagombea 80 wamejitosa katika kinyang'anyiro cha Urais

Saif al-Islam al-Gaddafi akijiandikisha kama mgombea wa UraisPicha: Khaled Al-Zaidy/REUTERS

Mjumbe Maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu Libya Stephanie Williams licha ya kutotangaza rasmi kufutwa kwa uchaguzi huo, amekuwa akikutana na wagombea wa Urais wiki hii wakati 17 kati ya yao, wakisema kwa jinsi hali ilivyo, uchaguzi huo hauna budi ila kuahirishwa.

Kwa ujumla wagombea wapatao 80 akiwemo mtoto wa Moamer Gadaffi, Saif al-Islam, walikuwa wamejitosa katika kinyang'anyiro cha Urais katika taifa hilo lililogawika kwa vita.

Soma pia: Kansela wa Ujerumani ataka mamluki waondoke Libya

Jana Jumanne, mbabe wa kivita Khalifa Haftar alikutana na wagombea wengine wawili wa Urais, aliyekuwa waziri wa mambo ya ndani Fathi Bashagha na naibu waziri mkuu wa zamani Ahmed Maiteeq mjini Benghazi.

Naibu waziri mkuu huyo wa zamani amewaambia waandishi wa habari, "Mkutano huu unatoa ishara ya matumaini kwa Walibya. Daima, Walibya wanaweza kuiongoza nchi katika hali ya utulivu. Libya ina uwezo wa kukabiliana na changamoto ili kuisaidia kusonga mbele."

Hata hivyo, haikuwa bayana ni kipi hasa kilichowakutanisha watatu hao lakini mshauri wa Bashagha ameliambia shirika la habari la AFP kuwa, sababu ya ziara yao mjini Benghazi ilikuwa ni kuondoa vikwazo na kuuonyesha ulimwengu kwamba wanaweza kuungana.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW