1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchaguzi wa Rais Nigeria waahirishwa

Caro Robi
16 Februari 2019

Uchaguzi wa rais wa Nigeria uliokuwa ufanyike Jumamosi hii (16.02.2019) umeahirishwa hadi tarehe 23 mwezi huu.

Kombobild Muhammadu Buhari und Atiku Abubakar

Mwenyekiti wa tume huru ya kitaifa ya uchaguzi Mahmood Yakubu amewaambia waandishi habari kuwa uchaguzi hauwezi kufanyika Jumamosi hii kama ilivyokuwa imepangwa akiongeza kuwa kucheleweshwa kwa uchaguzi huo hadi Jumamosi ijayo, kunahitajika ili kuandaliwa uchaguzi huru na wa haki.

Tangazo hilo la tume ya uchaguzi linakuja saa chache kabla ya vituo vya kupiga kura kufunguliwa kote nchini kwa uchaguzi wa rais na bunge katika taifa hilo imara zaidi kiuchumi barani Afrika na lenye idadi kubwa zaidi ya watu barani humo. Vituo 120,000 vilikuwa vifunguliwe saa moja Asubuhi.

Uchaguzi sasa 23 Februari

Yakubu amesema uamuzi huo mgumu wa kuchelewesha chaguzi umefikiwa baada ya kutathmini kwa makini utekelezaji wa mipango kiufundi ili kuhakikisha uchaguzi huru, wa haki na unaoaminika, na kuongeza sasa watakuwa na muda na fursa ya kushughulikia changamoto hizo za kiufundi ili kuhakikisha uchaguzi unaendeshwa upasavyo.

Afisa wa Tume ya Uchaguzi ya Nigeria akibeba vifaa vya kupiga kuraPicha: picture alliance/AP Photo/S. Alamba

Rais wa Nigeria Muhamadu Buhari mwenye umri wa miaka 76, anawania muhula wa pili madarakani lakini anakabiliwa na kinyang'anyiro kikali kutoka kwa kiongozi mkuu wa upinzani Abubakar Atiku ambaye ni makamu wa zamani wa rais na mfanyabiashara tajiri.

Kwa jumla, kuna wagombea 73 wa kinyang'anyiro hicho cha urais. Chaguzi za bunge na kuwachagua maseneta wapya pia sasa zitafanyika tarehe 23 Februari. Tume ya uchaguzi imesema chaguzi za ugavana na za udiwani zimeahirishwa hadi tarehe 9 Machi.

Hii si mara ya kwanza Nigeria inaahirisha uchaguzi katika dakika za mwisho. Katika uchaguzi wa mwisho mwaka 2015, uchaguzi nchini humo uliahirishwa wiki moja kabla ya kufanyika kutokana na matatizo ya kiusalama kutokana na uasi wa kundi la waasi la Boko Haram.

Aidha katika uchaguzi wa mwaka 2011 uchaguzi uliahirishwa kwasababu za changamoto za kiufundi.

Nigeria taifa ambalo lina utajiri wa mafuta linakabiliwa na matatizo ya kiusalama hasa kaskazini mashariki mwa nchi hiyo ambako mashambulizi ya Boko Haram yamesababisha mamilioni ya watu kuyahama makazi yao.

Ufisadi, umasikini na ukosefu wa ajira pia ni baadhi ya changamoto inazoikabili nchi hiyo yenye zaidi ya watu milioni 190.

Mwandishi: Caro Robi/Afp/Reuters/ap

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW