Uchaguzi wa rais Nigeria
24 Aprili 2007Tokea mwanzo kabisa uchaguzi huo uliandamana na vitimbi kadhaa ikiwa pamoja na kuondoa jina la mgombea wa chama muhimu cha upinzani , makamu wa rais bwana Atiku Abubakar.
Pia kulikuwa na malalamiko juu ya kucheleweshwa masunduku ya kupigia kura katika sehemu mbalimbali na hasa mashambani.
Licha ya uamuzi wa mahakama kuu kumruhusu bwana Abubakar kusimama katika uchaguzi , hakuwa tena na muda wa kutosha kufanya kampeni.
Pia palikuwa na ghasia zilizosababisha vifo vya mamia ya watu.
Lakini tume ya uchaguzi ilimtangaza mjumbe wa chama kinachotawala bwana Yar- Adua kuwa mshindi wa uchaguzi kwa kupata kura zaidi ya asilimia 70.
Vyama vya upinzani vimesema kuwa vitapinga matokeo hayo.
Lakini rais mtuele bwana Yar-Adua amesema hayo hayamuhusu. Amesema yeye hakuendesha uchaguzi huo.
Hatahivyo mjumbe wa Umoja wa Ulaya alieshuhudia uchaguzi huo bwana Max van den Bergh amesema kuwa uchaguzi huo haukutimiliza matarajio ya watu wa Nigeria na hivyo basi haiwezekani kusema kuwa ulikuwa wa haki. Amesema uchaguzi huo haukufikia viwango vya kimataifa ili kustahiki kuitwa wa kidemokrasia.
Lakini rais mteule bwana Yar- Adua amesema kuwa uchaguzi huo sasa umeshapita . Ameeleza kwamba tofauti za watu wa Nigeria pia zinapaswa kuondoka baada ya uchaguzi.
Uchaguzi huo ulipaswa kuwa wa kwanza ambapo serikali ya kiraia ingelikabidhi madaraka kwa serikali nyingine ya kiraia.
Lakini kutokana na mapungufu yaliyojitokeza itakuwa vigumu kusema iwapo zoezi hilo litafanyika kwa nia njema.
ABDU MTULLYA