1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchaguzi wa rais waendelea Malawi

John Juma Mhariri: Sekione Kitojo
21 Mei 2019

Wachambuzi wanatarajia ushindani kuwa mkali kati ya Rais Peter Mutharika, makamu wake Saulos Chilima na kutoka kwa Lazarus Chakwera ambaye anaongoza kundi la vyama vya upinzani.

Malawi Wahlen Präsident Peter Mutharika
Picha: picture-alliance/AP/T. Chikondi

Malawi inafanya uchaguzi wake mkuu leo kumchagua rais mpya pamoja na wabunge. Shughuli za upigaji kura zilianza mapema leo katika vituo vya upigaji kura. Rais wa nchi hiyo Peter Mutharika aliye na umri wa miaka 78 anawania muhula wa pili huku akikabiliwa na ushindani mkali kutoka kwa makamu wake na mgombea wa chama kikuu cha upinzani.

Vituo vya upigaji kura vilifunguliwa mwendo wa saa kumi alfajiri majira ya nchi hiyo, na inatarajiwa kuwa wapiga kura milioni 6.8 waliosajiliwa watashiriki kwenye uchaguzi huo wa rais, wabunge na madiwani.

Wapiga kura wameelezea matumaini ya kuwachagua viongozi wanaowapenda kuleta maendeleo.

Wachambuzi wanatarajia ushindani kuwa mkali kati ya rais Peter Mutharika, makamu wake Saulos Chilima na kutoka kwa Lazarus Chakwera ambaye anaongoza kundi la vyama vya upinzani Malawi Congres Party.

Wapiga kura kwenye foleni katika kituo cha kupiga kura karibu na mji mkuu Blantyre.Picha: picture-alliance/AP/T. Chikondi

Rais Mutharika mwenye umri wa miaka 78 alitekeleza maendeleo ya miundombinu na alipunguza viwango vya mfumuko wa bei ya bidhaa nchini humo katika muhula wake wa kwanza madarakani. Lakini wakosoaji wanamshutumu kwa kuendeleza ufisadi na upendeleo, madai ambayo Mutharika hukanusha.

Chilima mwenye umri wa miaka 46 na ambaye ni mkuu wa zamani wa kampuni ya mawasiliano, alijiondoa kwenye chama cha Mutharika Democratic Progressive Party mwaka uliopita na akaanzisha chama chake ili kushindana na Mutharika. Chilima amewaambia waandishi wa habari kuwa anatumai watu wengi watajitokeza kupiga kura na amani itadumu katika kipindi cha upigaji kura. 

"Ninatumai kwamba watu watajitokeza kwa wingi. Kufikia sasa watu wengi wamejitokeza na tunatumai wengi watajitokeza zaidi katika vituo vyote vya kupiga kura nchini kote siku ya leo.” Amesema Chilima.

Chilima haswa amewalenga vijana ambapo aliimarisha kampeni zake kupitia mitandao ya kijamii huku akichapisha video za muziki aina ya kufoka au hip-hop. Asilimia 54 ya wapiga kura Malawi ni vijana wenye umri wa kati ya miaka 18 na 34, huku wanawake wakiwa ni asilimia 56. Licha ya asilimia kubwa ya wapiga kura kuwa wanawake, hakuna mgombea yeyote wa urais ambaye ni mwanamke.

Tume inayosimamia uchaguzi Malawi imesema mfumo wao wa uchaguzi upo imara na hauwezi kudukuliwa. Picha: AFP/A. Gumulira

Chakwera ambaye ana umri wa miaka 64 alishindwa na Mutharika katika uchaguzi uliopita mwaka 2014. Wakati huu amejiunga na rais aliyekuwa mtangulizi wa Mutharika Joyce Banda kwa lengo la kushinda. Chilima pamoja na Chakwera wameahidi kupambana na ufisadi nchini Malawi.

Tume inayosimamia uchaguzi Malawi imewaahidi wananchi kuwa mfumo wao wa upigaji kura upo salama na hauwezi ukadukuliwa. Mwenyekiti wa tume hiyo Jane Ansa amesema kuwa hakuna mitandao ya mawasiliano ambayo itafungwa wakati wa kipindi cha uchaguzi.

Malawi hutegemea pakubwa misaada ya kigeni na mara kwa mara hukumbwa na ukame ambao hutishia maisha ya maelfu ya watu.

Vyanzo: AP, RTRE, AFPE

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW