1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchaguzi wa Ufaransa yumkini matokeo yakawa ya kushangaza

Admin.WagnerD20 Aprili 2017

Wagombea wa urais Ufaransa wameendelea kuwatolewa miito wapiga kura ikiwa ni siku nne kabla ya duru ya kwanza ya uchaguzi huku matokeo ya uchunguzi wa maoni yakionyesha kwamba mchuano ni mkali.

Frankreich Wahlkampfplakate in Paris
Picha: picture-alliance/abaca/A. Alain

Marine Le Pen mgombea wa urais wa chama cha sera kali za mrengo wa kulia cha National Front amejitangaza kwamba yeye ni chaguo la wazalendo nchini Ufaransa.

Akizungumza na wafuasi wake katika mji wa Marseille hapo Jumatano amewahimiza wafuasi wake hao kujitokeza kwa wingi katika uchaguzi huo wa Jumapili kwa kusema kwamba ni muhimu kwa kiongozi huyo wa sera kali za mrengo wa kulia kujipatia ushindi iwapo ataingia duru ya pili.

Amesema "Nahitaji dhamira kamili na kuungwa mkono na wazalendo wa Ufaransa. Haipaswi kukosekana hata kura moja ya mzalendo hapo Jumapili,haipasi hata mtu mmoja kubabaishwa na mikakati ya uchaguzi.Nahitaji kura nyingi kadri inavyowezekana hapo Jumapili zinahitajika kwa ajili ya ushindi duru ya pili."

Sakama wahamiaji

Marine Le Pen mgombea wa chama cha sera kali za mrengo wa kulia.Picha: Reuters/P. Rossignol

Katika kampeni yake hiyo ya mwisho ameendelea kulisakama suala la wahamiaji kwa kuapa kwamba hatua yake ya kwanza baada ya kuchaguliwa itakuwa ni kurudisha udhibiti wa mipaka ya nchi hiyo mikononi mwa taifa.

Amedai kwamba uhuru pekee iliobakishiwa Ufaransa ni kuona wadukuzi kutoka kila mahala duniani wakiingia nchini humo.

Amesema wanataka kuigeuza Ufaransa kuwa skwata kubwa na kwamba wananchi wa Ufaransa ni wamiliki wa Ufaransa na ni wajibu wao kuamuwa nani anayepaswa kuhamia nchini humo.

Kupiga vita ugaidi

Emmanuel Macron mgombea wa kujitegemea wa sera za wastani.Picha: Getty Images/S. Lefevre

Katika mji wa magharibi wa Nantes mgombea wa kujitegemea wa sera za wastani Emmanuel Macron amejaribu kujinadi kama mgombea ambaye atakuwa anaweza kuaminiwa kwa usalama wa nchi hiyo.

Amemshutumu mgombea wa sera za mrengo wa kushoto Jean-Luc Melenchon ambaye amejinadi kama mgombea wa amani na kutaka Ufaransa ijitowe katika jumuiya kujihami ya NATO.

Amesema wakati mgombea huyo anapopendekeza kuindolea silaha nchi hiyo anamaanisha anapendekeza amani kwa Urusi jambo ambalo yeye halitaki.Akizungumza na maelfu ya wafuasi wake Macron ameahidi kulifanya suala la kupambana na ugaidi kuwa mojawapo ya vipau mbele vyake.'

Amesema "Kile tunachokipitia sasa,chaguo tutaloamuwa katika kipindi cha siku nne ni kwa ajili ya kizazi kizima ni kwa ajili ya ustaarabu wote.Ndio kwa sababu magaidi wameamuwa kutushambulia katika wakati wa mashaka,katika wakati muhimu,wakati tunapopitia mabadiliko makubwa yenye kututia kwenye changamoto jambo ambao limaanisha kwamba kila mmoja wetu ana wajibu wa aina yake masaa na siku zinazokuja."

Inaonekana kampeni hiyo ya uchaguzi wa Ufaransa iliodumu kwa miezi kadhaa inazidi kutanuka na kutokuwa na uhakika nani atakuwa mshindi wakati siku ya uchaguzi ikikaribia.Ajira kwa ajili ya familia ambayo imetibuwa kampeni ya Francois Fillon imewafanya wapiga kura kukosa imani na wawakilishi wao wanaowachaguwa.

Mwandishi : Mohamed Dahman

Mhariri : Iddi Ssessanga

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW