Uchaguzi wa kumrithi Blatter utafanyika Februari mwakani
20 Oktoba 2015Kamati hiyo imekutana kwa mara ya kwanza tangu kupigwa marufuku kwa rais wa shirikisho hilo Sepp Blatter na rais wa shirikisho la soka barani Ulaya – UEFA Michel Platini kwa tuhuma za kushiriki ufisadi. Blatter na Platini wamekanusha madai hayo yaliyotolewa na kamati ya uadilifu na nidhamu ya FIFA.
Shirikisho hilo pia limethibitisha kuwa litaendelea mbele na kikao chake maalum wakati huo huo. Rais anayeondoka madarakani Blatter, amekuwa uongozini tangu mwaka wa 1988.
Mapendekezo mengine yaliyopitishwa ni kuwa shirikisho hilo litakuwa wazi zaidi katika nia yake ya kupambana na ufisadi na ulaji rushwa miongoni mwa maafisa wake wakuu. Aidha uwazi huo unatoa fursa kwa majina ya maafisa wanaochunguzwa kutajwa hadharani. Kikao hicho kimependekeza kuwa rais atakayekiongoza asizidi umri wa miaka 74.
Kamati maalum ya mageuzi katika FIFA imependekeza kuwa rais atakayeteuliwa asizidishe miaka 12 akiliongoza shirikisho hilo linalosimamia soka kote duniani. Kauli hii ya kamati kuu ya FIFA inaelekea kuathiri vibaya nia ya Michel Platini kuwania urais ambaye anatumikia marufuku ya siku 90 kwa madai ya ufisadi.
Licha ya kuwasilisha nyaraka zake zote za kuomba kura mapema mwezi huu kamati kuu ya FIFA imepuuzilia mbali kwani tayari amepigwa marufuku kushiriki vikao vyake mbali na kuwa hawezi kuendesha kampeni yake. FIFA imesema itamruhusu kushiriki uchaguzi huo iwapo tu marufuku yake itaisha kabla ya siku ya uchaguzi.
Mwandishi: Bruce Amani/Reuters
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman