1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchaguzi Zimbabwe unaelekea kuwa mgumu

21 Julai 2013

Viongozi kutoka jumuiya ya maendeleo ya nchi za kusini mwa Afrika SADC jana Jumamosi (20.07.2013) wameonya kuwa utayarishaji wa uchaguzi mkuu ujao nchini Zimbabwe utakuwa mgumu kutokana na muda mfupi wa maandalizi.

A Zimbabwean police officer casts his vote, at a polling station in Harare, Monday, July, 15, 2013. Officials of Zimbabwe's election commission said Sunday early voting started for police and security personnel who will be on duty during the nation's crucial elections on July 31. (AP Photo/Tsvangirayi Mukwazhi)
Wanajeshi wakipiga kura kwanza katika uchaguzi wa Zimbabwe2013Picha: picture-alliance/AP Photo

Mataifa 15 wanachama wa jumuiya hiyo ya SADC mwezi uliopita yameitaka Zimbabwe kuchelewesha uchaguzi huo uliopangwa kufanyika Julai 31 kwa kiasi wiki mbili zaidi ili kuruhusu muda wa kutosha kuweza kutekeleza mageuzi kadha ambayo yatahakikisha uchaguzi huru na wa haki.

Lakini mahakama kuu ya nchi hiyo imeidhinisha tarehe ya uchaguzi ambayo ilitangazwa na rais Robert Mugabe.

Rais Robert Mugabe wa ZimbabwePicha: Reuters

Muda mfupi mno

"Tungependelea iwapo ushauri wetu ungekubalika," rais wa Tanzania Jakaya kikwete amewaambia waandishi habari jana Jumamosi(20.07.2013) baada ya mazungumzo ya nusu siku ya kamati ya SADC ya ulinzi na usalama. Kutayarisha uchaguzi katika muda wa mwezi mmoja, "ni kazi ngumu" na "kuweza kufanikisha kila kitu, unajua ni kazi kubwa mno," amesema.

"Ndio sababu tunaona hata matukio ya upigaji kura wa mwanzo, ambapo nusu ya watu wanaostahili kupiga kura hawakuweza kufanya hivyo, kwa upande mmoja kutokana na muda mfupi mno."

Rais wa Tanzania Jakaya KikwetePicha: DW

Maelfu ya majeshi ya usalama ambao watalazimika kufanyakazi wakati wa uchaguzi hapo Julai 31 wameshindwa kupiga kura zao katika muda wa siku mbili za kuanza kupiga kura wiki iliyopita kutokana na upungufu wa karatasi za kupigia kura, wino na masanduku ya kura.

"kwa hiyo utakuwa uchaguzi mgumu mno kuuendesha," Kikwete amesema baada ya mazungumzo ambayo yamehudhuriwa pia na rais wa Afrika kusini Jacob Zuma na Armando Guebuza wa Msumbiji.

Lakini SADC , ambayo tayari imeweka waangalizi wa uchaguzi 360 nchini Zimbabwe, imeapa kuwa pamoja na nchi hiyo kuhakikisha uchaguzi unakuwa wa kuaminika kwa kiasi cha kutosha.

"Tumeamua kufanyakazi pamoja na watu wa Zimbabwe na kuona iwapo tunaweza kuhakikisha katika muda uliobaki wa siku 11, kuwa tunaweza kuwa na uchaguzi ambao utakuwa unaaminika kwa kiasi cha kutosha" amesema. "Naamini tunaweza."

Matatizo ya fedha.

Nchi hiyo yenye matatizo ya fedha pia haijaweza kupata fedha inazohitaji kuweza kufanya uchaguzi huo. Uchaguzi huo unaosubiriwa kwa hamu nchini Zimbabwe una lengo la kufikisha mwisho serikali ya kugawana madaraka yenye mivutano kati ya rais Robert Mugabe na hasimu wake mkubwa waziri mkuu Morgan Tsvangirai, iliyoundwa miaka minne iliyopita kama sehemu ya mpago wa kumaliza mauaji ya kisiasa nchini humo.

Waziri mkuu wa Zimbabwe Morgan TsvangiraiPicha: Reuters

Zuma anaongoza kundi la upatanishi kutoka jumuiya ya SADC kuhusu Zimbabwe, ambayo imekuwa ikihimiza uchaguzi huo.

Kundi hilo la mataifa limetoa mbinyo kwa Mugabe kutoa muda ili kutekelezwa kwa mageuzi kadha ambayo yatapunguza jukumu ya jeshi la ulinzi katika siasa, kuzuwia wapiga kura hewa kuandikishwa katika daftari la wapiga kura na kuhakikisha kuwa kila mtu anayestahili kupiga kura anandikishwa.

Mugabe anguruma

Lakini mkutano wa Jumamosi umekuja huku kukiwa na mashambulio mapya ya Mugabe dhidi ya mshauri mkuu wa masuala ya mambo ya kigeni wa rais Zuma , Lindiwe Zulu.

Rais wa Afrika kusini Jacob ZumaPicha: picture-alliance/dpa

Akizungumza katika mkutano wa kampeni jana Jumamosi, Mugabe amesema Zuma anapaswa kumdhibiti Zulu na kwamba SADC haipaswi kudanganya juu ya hali ya Zimbabwe. Zulu amesema siku ya Ijumaa(19.07.2013) kuwa bado kuna changamoto kubwa kuelekea uchaguzi wa Zimbabwe. Lakini Mugabe amesema, "Namtolea wito rais Zuma kumzuwia mwanamke wao huyu kuzungumza kuhusu Zimbabwe."

Wakati uchaguzi unatarajiwa kufanyika katika muda wa chini ya wiki mbili, Zimbabwe bado inajaribu kuchangisha kiasi cha dola milioni 132 kwa ajili ya uchaguzi huo. Waziri wa fedha Tendai Biti amesema kuwa serikali itapata fedha hizo katika muda muafaka kwa ajili ya uchaguzi huo. SADC imesema haijapata ombi lolote kwa ajili ya kuchangia uchaguzi huo kutoka Zimbabwe.

Mwandishi : Sekione Kitojo / afpe

Mhariri : Sudi Mnette

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi
Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW