Uchaguzi Zimbabwe wazua maoni tofauti
5 Agosti 2013"Robert Mugabe achaguliwa tena kuwa rais!" Kichwa hicho cha habari kilitawala magazeti mengi ya Kiafrika hapo jana baada ya tume ya uchaguzi ya Zimbabwe kutangaza kuwa Mugabe amepata asilimia 61 ya kura na hivyo kumwacha mbali kabisa mpinzani wake wa karibu Morgan Tsvangirai wa chama cha MDC. Yeye aliambulia asilimia 34 tu ya kura.
Miongoni mwa viongozi wa kwanza kumpongeza Mugabe, mwenye umri wa miaka 89, alikuwa rais wa Afrika Kusini Jacob Zuma. Alitoa pongezi zake za dhati na kuzitaka pande zote kukubali matokeo ya uchaguzi kama matakwa ya wananchi wa Zimbabwe.
Lakini kutoka nchi za Magharibi, Mugabe hakupokea pongezi. Wengi wanashuku uhalisia wa matokeo kutokana na shutuma za wizi wa kura zilizozushwa na wafuasi wa chama cha MDC na vile vile mashirika yasiyo ya kiserikali yaliyokuwa yakifuatilia maandalizi ya uchaguzi kwa karibu.
"Shutuma za wizi zichunguzwe"
Waziri Mkuu wa Ujerumani, Guido Westerwelle, amesema kwamba shutuma hizo za hitilafu katika uchaguzi zinaweka giza katika mustakabali wa kisiasa na wa kiuchumi wa Zimbabwe. Westerwelle amekosoa pia kukosekana kwa uwazi katika mchakato wa kupiga na kuhesabu kura. Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon ametaka shutuma za wizi wa kura zichunguzwe mara moja.
Naye waziri wa mambo ya nje wa Australia, Bob Carr, ametaka uchaguzi urudiwe. Awali, waangalizi wa Jumuiya ya maendeleo ya nchi za Kusini mwa Afrika, SADC, walisema kuwa uchaguzi ulikuwa huru na wa haki. Hata hivyo, baadaye mwangalizi mkuu wa SADC na waziri wa mambo ya nje wa Tanzania, Bernard Membe, alisahihisha tamko hilo. Membe alisema: "Hatukusema kuwa uchaguzi ulikuwa wa haki. Hatukutaka kutoa tamko la mwisho haraka hivyo."
ZANU-PF yashinda bungeni
Ushindi wa Mugabe unamaliza muda wa serikali ya mseto kati ya chama chake cha ZANU-PF na kile cha MDC cha Morgan Tsvangirai. Hii ni kwa sababu katika uchaguzi wa bunge, ZANU-PF imepata theluthi mbili ya viti, jambo linalokiwezesha chama hicho kutawala chenyewe.
Mpaka kufikia Jumamosi, MDC inapaswa kuwasilisha ushahidi wa wizi wa kura katika mahakama ya katiba ya Zimbabwe. Hata hivyo, wachambuzi wanasema kwamba itakuwa vigumu kwa MDC kupata ushahidi wa kutosha.
Mwandishi: Elizabeth Shoo/afp
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman