1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchambuzi: Utata kwenye ushindi wa waandamanaji Lebanon

30 Oktoba 2019

Hatimaye Waziri Mkuu Saad Hariri wa Lebanon amejiuzulu kufuatia maandamano dhidi yake, lakini uchambuzi wa Kersten Knipp anasema ushindi huu wa waandamanaji haumaanishi kuuangusha mfumo wa utawala wanaoupinga.

Ishara ya maandamano dhidi ya serikali nchini Lebanon
Ishara ya maandamano dhidi ya serikali nchini LebanonPicha: picture-alliance/AP Photo/B. Hussein

Licha ya wanamgambo wa Kishia wa kundi liitwalo Amal na wale wa Hizbullah kujaribu kadiri wawezavyo kuyasambaratisha maandamano kabla ya kujiuzulu kwa Hariri hapo jana, kwa kuwashambulia mitaani na kuvunja mahema yao katika Uwanja wa Mashahidi, waandamanaji waling’ang’ania madai yao kwamba uongozi mzima wa kisiasa lazima uporomoke.

Katika taifa ambalo uongozi wake unaundwa kwa misingi ya kidini na kimadhehebu, madai haya yalimaanisha kwamba viongozi wa dini na madhehebu hizo wamekataliwa na umma. Waandamanaji walikuwa wanatuma ujumbe kwamba sasa taifa limegundua kuwa mfumo uliopo unajenga ufuasi wa kufuata mkumbo na utawala wa upendeleo na hivyo kulea ufisadi miongoni mwao.

Maandamano haya yaliwaunganisha wafuasi wa Kishia, Kisunni na Kikristo. Si hayo tu, bali kwa namna ya pekee kabisa, safari hii tabaka la kati na wanafunzi wakajihusisha moja kwa moja na upinzani dhidi ya serikali. 

Lakini je, maandamano haya kweli yameweza kuukomesha mfumo huu wa utawala? Mchambuzi wa masuala ya kisiasa kutoka Chuo Kikuu cha Haigaizan mjini Beirut, Maximilian Felsch, anatilia shaka jambo hilo.

"Hata kama raia wengi hawaridhishwi na muundo wa serikali kwa mujibu wa dini na madhehebu, lakini endapo utafanyika uchaguzi hivi leo, raia hao hao watavipigia kura ambavyo vitasema vinawawakilisha na kulinda maslahi ya dini au madhehebu yao", anasema Felsch akiongeza kwamba "hata uchaguzi mpya ukiitishwa hautakuja na matokeo tafauti, badala yake watu wale wale watarejea madarakani."

Iraq kama Lebanon

Waandamanaji mjinji Baghdad, Iraq, wakikabiliana na vikosi vya serikali.Picha: picture-alliance/AA/M. Sudani

Kama ilivyo kwa Lebanon, nchini Iraq nako hivi sasa vijana wengine wako mitaani wakiandamana dhidi ya ufisadi wa serikali yao. Siku chache zilizopita, Waziri Mkuu Adel Abdul Mahdi alijaribu kuwatuliza kwa kutangaza mpango wa mageuzi, kuunda upya baraza la mawaziri na msaada kwa raia masikini. Lakini badala ya kuwatuliza, ndio kama aliwachomoa, kwani waandamanaji hao walilichukulia tangazo hilo kama ni kuwapotezea muda wao.

Kiongozi mashuhuri wa jamii ya Kishia, Muqtadha al-Sadr alijitolea kutuma wafuasi wake mitaani kwenda kuwalinda waandamanaji, lakini msemaji wa maandamano hayo alikataa, akisema mwenye Sadr ni sehemu ya matatizo yanayoikumba Iraq kutokana na ushawishi wake serikalini. Wanamlaumu pia kiongozi huyo kwa kushindwa kupambana na nguvu ya Iran ndani ya Iraq.

Kwenye maandamano hayo, waandamanaji kadhaa wamepigwa risasi na kuuawa. Waandamanaji wanawahusisha wanamgambo wanaoegemea upande wa Iran kwa mauaji hayo.

Kitu kimoja kilicho wazi ni kwamba kote, Lebanon na Iraq, wafuasi wa madhehebu ya Shia na Sunni walishiriki maandamano kwa pamoja. Wanaungana kwenye hasira zao dhidi ya mifumo ya kisiasa kwenye mataifa yao, ambayo yote ina muundo wa kimadhehebu na kidini.

"Lakini hata kwa Iraq, ambako ni suala la ama Shia au Sunni, wote waumini wa dini moja, bado hakuna uhakika kuwa wanaweza kuuangusha mfumo huu," anasema mchambuzi Maximilian Felsch.